Tukibaki Hai, Tutasimulia

Tuko bega kwa bega[emoji123]
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 31


Na Steve B.S.M




SUV nyeusi iliposimama, mwanaume aliyevalia suti na tai nyeusi alishuka upesi akafuata mlango wa nyuma na kuufungua, akatoka bwana mkubwa. Kidogo mlango mwingine ukafunguka akatoka mwanaume maridadi ndani ya suti, alikuwa ni Babyface, na yule bwana mkubwa aliyefunguliwa hapo mwanzo alikuwa ni mkubwa wake wa kazi, mkubwa ambaye huwa anakuwa naye mara kwa mara, bwana huyo kwa sifa ni mtulivu na asiyeongea maneno mengi, pengine hekima za uzee zilimzidia, hutanguliza akili kuliko mdomo, hamna anayejua.

Bwana Babyface pamoja na bwana huyo waliingia ndani ya jengo ambalo kwa nje walipokelewa na maafisa wengine wa usalama, kwa haraka kama watano hivi, walikuwa wako 'alerted, wanatazama huku na kule kutazama na kuhakikisha usalama wa jengo hili, na hawakuwa wenyewe, kwa mbali pia walikuwapo wengine ambao ukiwatazama tu kwa jicho la umakini utabaini ni wana usalama, wanarandaranda huku na kule.

Babyface alipanda lifti ya jengo hili pamoja na mkuu wake, walikuwa wawili tu ndani ya lifti na huu ukawa wasaa wao mzuri wa kuzungumza baadhi ya mambo.

"Nategemea kila kitu kitaenda sawa," Mkuu akasema akivutavuta koti lake kwa kulitengenezea, "Kama jambo hili likikoma, basi nitastaafu kwa heshima, nikilishindwa itabaki kuwa fedheha maishani mwangu."

Aliposema hayo akamtazama Babyface na kumuuliza,

"Unadhani nitafanikiwa?"

Babyface hakujibu kwa kinywa, badala yake akainamisha kichwa chini, Mkuu akashusha pumzi ndefu na mara mlango wa lifti ukafunguka, wakatoka, wakaongozana mpaka kwenye chumba maalum, chumba kikubwa cha kufanyia mkutano, humo wakakuta kuna watu wawili waliovalia kombati za kiofisa wa jeshi, muda si mrefu baada ya kufika hapa, chumba hicho kikajawa na watu kadha wa kadha wenye wadhifu mkubwa katika mambo ya usalama, watu hao walikuwa wamekaa kuizingira meza kubwa lakini kiti cha mkubwa wa kikao hiki bado kilikuwa wazi.

Kidogo king'ora kikalia, gari lilimleta mtu, ndani ya muda mfupi mtu huyo akawa amefika, alikuwa ndo' mkubwa wa kikao hiki, waziri wa ulinzi wa taifa hili, bwana Logan Diff, mwanaume mrefu shupavu, nywele zake mchanganyiko wa rangi nyeupe na nyeusi, mwili wake mkakamavu na umenyooka kimazoezi, hatua zake ni kamilifu akitembea kuonyesha amepitia mafunzo ya jeshi, kisigino ndo' kinaanza kugusa chini kisha mguu mzima, amevalia shati la bluu bahari, amelikunja mikono yake.

Bwana huyo alipoingia katika ukumbi huu, wote wakasimama, ni mpaka alipoketi yeye ndipo na wengine wakaketi kisha kikao kikaanza, muhtasari wa kikao ulitajwa na mada iliyowakutanisha hapo.

Bwana Logan Diff alikabidhiwa faili lenye nyaraka za siri, faili lenye jalada la jeusi huku likiwa na chapa nyekundu ya neno CONFIDENTIAL, akalipitia faili hilo kwa umakini, uso mkavu, kwa dakika mbili, kisha akaliweka faili hilo pembeni na kumtazama bwana yule aliyekuja akiongozana na Babyface, kwenye meza yake kulikuwa na kijibao kilichoandikwa jina lake, na ilikuwa hivyo kwa kila mtu aliyeketi hapa, mbele yake kilisimama kibao kinachomtambulisha jina kamili, kwa mkuu wa kazi wa Babyface kibao chake kilisoma Brendan Garret, afisa mwandamizi wa taasisi ya CIA.

"Garret," Logan aliita kisha taratibu akaanza kuaeleza mambo yahusuyo oparesheni ambayo ilipatiwa jina la oparesheni BALTIKA.

"Bwana Garret, kwa sahihi yako mwenyewe mnamo mwaka 2005, ulihitaji serikali iidhinishe mkakati wako wa kuwatengeneza binadamu bora zaidi kwaajili ya mapambano ya nje ya nchi, kwa maelezo uliyoyatoa, watu hao watatumika kama mbadala wa taifa letu kupoteza wanajeshi lukuki katika uwanja wa mapambano, mkakati kabambe kabisa, serikali ikaidhinisha na kuupitisha mkakati huo baada ya mapitio, mabilioni ya dola yakatolewa kwaajili ya kuufadhili, lakini baada ya vita tano kubwa, huko Iraq, Afghanistan, Syria, Sudan na Somalia mkakati wako ukashindwa kuonyesha matunda baada ya watu wako kubadilika, haukuweza kuwamudu tena kama hapo mwanzo, ikabidi wateketezwe, sio?"

Garret akatikisa kichwa kukubali maelezo hayo yote, Waziri Logan akaendelea kutoa taarifa kwa kutumia kumbukumbu ya kichwa chake,

"Jambo hili ni la siri, Garret, lazima kila kitu kisafishwe huku chini, laiti nisingefanya hisani ya kiubinadamu basi unajua mambo yangekuwa magumu zaidi lakini shida ni kwamba unanifanya niwe katika wakati mgumu, wa kujutia hisani yangu ...."

Alipofikia hapo akaweka kituo kikubwa, akanyanyua glasi ya maji iliyokuwapo pembeni yake na kunywa mafundo mawili makubwa kutibu koo lake kavu, alipofanya hivyo akaendeleza maneno yake kwa utaratibu kabla ya kwenda kwenye hukumu,

"Katika vita ya mwisho, kwa maelezo ambayo taasisi yako iliyatoa, Bwana Garret, hao watu waliuawawa wote, hakuna aliyebaki, chanzo kikiwa milipuko mikubwa ya mabomu, lakini ...."

Akavuta faili jingine na kutazama, faili hilo lilikuwa limetokea upande wa kitengo cha Polisi, akafungua moja kwa moja ukurasa nambari sitini na mbili, hapo kulikuwa na picha kadhaa pamoja pia na maelezo, hakuyasoma, yalishakuwa kichwani, alishajua kilichopo hapo, akalisogeza faili hilo kwa Garret kisha akaendeleza maneno Garret akiwa anatazama faili alilosogezewa karibu,

"Sidhani kama maelezo yako yalikuwa sawa, Garret, kwa mujibu wa picha hiyo katika faili za polisi, mwanamke huyo yuko hai na yuko mtaani, nadhani unamfahamu sivyo?"

"Ndio."

Logan akaongezea, "huyo ni 00/89/31/12 CKM. Imekuaje bado yuko hai?"

"Tulibaini hili jambo si muda mrefu," Garret aliteta, "tulistaajabu yupo mtaani na ..."

"Na akawa tayari ameshaua!" Logan akamkatisha. "Si ndivyo?"

Garret hakujibu, alinyamaza akitazama meza.

"Alafu mnaleta hapa maelezo ambayo hayajitoshelezi kabisa, Garret, unafahamu wazi kuwa watu hawa ni hatari, kama mlishindwa kuwamudu, raia wa kawaida huko mitaani wataweza? Haya maafa tutambebesha nani lawama? Nani anayejua kitakachofuatia baada ya hiki? Na nani anayejua kama kuna wengine zaidi ya mwanamke huyu huko mtaani?"

Logan alifungua faili jingine toka polisi, akalipitia kwa ufupi kisha akampatia bwana Garret kwa kulitupia mezani, faili hilo lilijawa na picha nyingi sana, picha za mauaji kadha wa kadha, picha ya maiti ya Ronelle, Travis, pamoja pia na picha ya ajali mbaya iliyommaliza Mpelelezi huko San Fransisco, hapo Logan Diff akasema,

"Mpelelezi huyo alikuwa anafuatilia mauaji yaliyotokea The DL, mauaji aliyoyafanya 00/89/31/12 CKM. Huyo mwanamke Ronelle alikuwa katika orodha yake ya upelelezi, akaishia kufa, huyo Travis kwa mujibu wa maelezo yake ya mwisho ya simu, aliongea na Mpelelezi, bila shaka ni kuhusu kesi hiyo ya The DL, naye akafa, na mwisho wa siku Mpelelezi mwenyewe akapata ajali, hit and run, una lolote la kutuambia kuhusu haya? Huu ni mkakati wenu wa kuzuia taarifa zenu kwenda kwa umma? Kwahiyo watu wenu wanaua na nyie pia mnaua?"

Garret aliipotaka kufungua mdomo wake kujitetea Logan alibamiza meza kwanguvu kumkatiza kisha akamkodolea macho ya ukali na kusema, "ulifanya kazi kubwa sana, Garret, hamna asiyefahamu hilo katika nchi hii, lakini kwa hili, unaenda kufuta 'legacy' yako yote uliyoijenga kwa damu na jasho!"

Baada ya kitambo kidogo ya kikao kumalizika, Bwana Garret alikuwa kwenye gari lake akiwa amezama ndani ya fikra, kichwa chake alikiegamiza kwenye dirisha macho yake yakitazama nje, pembeni yake Babyface aliketi akimtazama, alifahamu muda ule haukuwa sahihi kumwongelesha mkuu wake wa kazi ijapokuwa alitamani sana, basi akaishia kujihifadhi kifuani.

Gari lilienda kwa mwendo wa kilomita chache, liliposimama kupisha taa nyekundu ya barabarani, bwana Garret akaongea akiwa bado amelaza kichwa chake kwenye dirisha,

"Unafahamu chochote kuhusu mauaji ya wale watu?"

Garret aliuliza akilenga vifo vya Travis, Ronelle pamoja na Mpelelezi, kuna jambo alikuwa analipambanua kichwani mwake, jambo ambalo bado lilikuwa na kiza kinene, kabla Babyface hajajibu swali hilo akanyanyuka upesi na kumtazama kwa kuyakaza macho, akaongezea swali,

"Ulishiriki kwenye hayo mauaji?"

Babyface akajikuta anayakodoa macho yake kwa mshangao, hakutarajia swali hilo ghafla kiasi hiko.


***


Metropolitan Hospital, New York, asubuhi ya saa nne.


"Unaweza kumwona hivi sasa, amesharuhusiwa," mhudumu aliposema hivyo Hilda akashika zake njia lakini kabla hajafika popote akamwona Richie akiwa anakuja, mwanaume huyo alikuwa amekunja sura yake kana kwamba ametoka kulamba ndimu kali, mwendo wake pia ulikuwa wa taratibu akijikongoja, basi Hilda akamfuata na kumshika mkono ili apate kumsaidia, Richie akamshukuru kwa kuja kumjulia hali, wakaongozana mpaka nje ya hospitali ambapo walisimamisha taksi kwaajili ya safari, walipokwea na kuondoka, Hilda alimtazama Richie kwa macho ya huruma akauliza,

"Richie, kwani nini kilitokea?"

Kabla Richie hajajibu, Hilda akaongeza, "Jamal alinipigia simu amekukuta umezidiwa, nini kilikukumba, Richie? Mbona imekuwa ghafla hivyo?"

Richie akatikisa kichwa, akahisi maumivu makali, haraka akatuliza kichwa chake akisonya mithili ya mtu anayeita paka, alafu akasema,

"Nikikwambia sijui unaweza kuniamini?"

"Hujui nini?"

"Sijui kilichotokea."

"Hujui kilichotokea?"

"Sikumbuki kitu chochote kile, nastaajabu sana, naweza kukumbuka vitu vya juzi ama juma lililopita lakini sikumbuki kitu chochote kuhusu jana usiku, kitu pekee ninachokumbuka ni kukutana na Jamal."

"Serious?"

"Serious, nakwambia kweli, lakini nahisi maumivu ya kichwa kweli, kadiri niongeavyo nahisi kuyatibua."

Baada ya hapo Hilda akajiepusha kumuuliza maswali bwana huyu kwa kuhofia kumsababishia maumivu, walipofika nyumbani wakamkuta Jamal akiwa hapo anawangoja, wakasaidizana kumpeleka Richie chumbani kwake kwaajili ya mapumziko kisha wakasogea kando kwaajili ya mazungumzo mafupi.

"Anasema hakumbuki kitu?"

"Ndio, nimemuuliza anasema hamna anachokumbuka, lakini wewe ulikuwa naye hapa jana, uliona nini?"

"Alikuwa vizuri kabisa, nilifanya naye mazungumzo kabla hajaniaga kwenda kuichukua simu yake, ajabu nilipomfuata baada ya kuona anakawia ndo' nikamkuta amelala chini, hana fahamu!"

"Hakuona dalili yoyote?"

"Hapana ... lakini kuna mtu fulani nilimwona, hisia zangu zinapata kumshuku sana kuwa si mtu mwema, huenda akawa alimfanyia kitu Richie."

"Nani huyo?"

"Simjui, alivalia nguo za kujificha hata gari lake halikuwa na namba za usajili!"

"Atakuwa anataka nini kwa Richie? Kuna kipi cha kumfanya awindwe na mtu?"

"Sijajua ... lakini nilikuja hapa kumwona Richie sababu ya matatizo yangu binafsi, kwasababu yupo katika hali ya kutokumbuka si mbaya nikakushirikisha wewe, pengine unaweza kunisaidia."

"Nini hiko?"

Jamal akaleza kinachomsibu, wakati huo wakiwa hawana hili wala lile, palikuwa na mtu aliyekuwa anawatazama kwa umakini akiwa ndani ya gari, mtu huyo alikuwa ameshikilia kalamu mkono wake wa kushoto na alikuwa anaandika kila alichokitambua kwa kupitia kusoma 'lips' za wahusika. Bwana huyu alikuwapo hapa kwa muda, na hakuwa mwingine bali yuleyule aliyekuwapo hapa jana yake na kumvamia Richie.


***
 
Yani wewe nilikutafutaga Sana Kumbe umewekeza huku siku hizi eeh ,.. malkia wa gosheni bado nangoja S3 [emoji23][emoji23]
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…