Hoja ya Muungano yawagawa wabunge
2008-08-21 09:16:17
Na Beatrice Bandawe, Dodoma
Hoja ya Muungano jana iliwagawa wabunge wa kutoka Tanzania Bara na wale wa Visiwani huku wa Bara wakiiunga mkono kwa kutaka uongelewe U-Tanzania zaidi na wale wa Visiwani wakionyesha kutokubaliana nao.
Bila kujali itikadi zao za vyama, wabunge wa Visiwani walionekana kuwa na msimamo mmoja wa kung\'ang\'ania kuwepo kwa serikali tatu na baadhi kudiriki kusema Wazanzibari hawako tayari kuwa na serikali moja.
Hoja hiyo iliingiliwa kati na Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta, aliyesema kuna haja ya kutafuta nafasi ya kufanya semina kuhusu Muungano kwa kuwa dhana hiyo inapotoshwa na baadhi ya wabunge.
``Tunahitaji wazee wetu tusaidiane, kama mzee wetu Kingunge,`` alisema Spika Sitta.
Wakichangia mjadala wa hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Bw. Mohammed Seif Khatib, ambao uliendelea kwa siku ya pili jana, wabunge hao walionekana kupangwa kwa utaratibu wa kuchangia kwa mbunge wa Tanzania Bara kufuatiwa na kutoka mbunge kutoka Visiwani.
Mjadala huo pia ulihudhuriwa na mashuhuda wa Muungano wa mwaka 1964, ambao ndio waliobeba vibuyu vya udongo kutoka Tanganyika na Zanzibar na baadaye kuchanganywa na waasisi wa Muungano, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume.
Mashuhuda hao ni Bi. Khadija Abbas Rashid ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 16, Bw. Hassan Omar Mzee, naye alikuwa na miaka 16 na Bi. Sifael Shuma, aliyekuwa na miaka 30, wakati huo.
Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Bi. Anna Komu, alikataa kuunga mkono hoja ya wizara kwa madai kuwa mpaka aelezwe Zanzibar inasaidiwa vipi kiuchumi kwa kuwa maisha ya Wazanzibari ni magumu.
Bw. Job Ndugai, Mbunge wa Kongwa (CCM), alisema linapokuja suala la Muungano, upande mmoja kazi yake ni lawama tu na kuhoji hivi ni kweli Bara kazi yake ni kuionea Zanzibar.
``Kwa nini mnajidharau wenyewe, wakati Zanzibar ina maendeleo kushinda Bara,`` alisema.
Mbunge wa Nkasi (CCM), Bw. Ponsian Nyami, ambaye alikuwa akinukuu vifungu vya Katiba kila alipokuwa akitoa hoja zake, aliwataka Wazanzibari kuongelea U-Tanzania zaidi kwa kuwa Tanzania ni nchi moja tu na si vinginevyo.
Akipinga kuwepo kwa serikali moja, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, Bw. Aboubakar Khamis Bakar (CUF), alisema Wazanzibar hawako tayari kuwa na serikali moja.
Naye Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Dk. Samson Mpanda, alihoji wanachokitaka hawa (akimaanisha Wazanzibari) kipo.
``Mimi sijui ni kitu gani lakini kipo wenyewe wanakijua,`` alisema na kuongeza kuwa wasioutaka Muungano walie tu.
Hata hivyo, Mbunge wa Konde (CUF), Bw. Ali Tarab Ali, alisema wakati umefika wa kuwashirikisha wananchi kwa kuibua mijadala waeleze wanataka aina gani ya muungano.
Mbunge wa Mchinga (CCM), Bw. Mudhihir Mudhihir, alisema mtafaruku unaojitokeza ndani ya Bunge Watanganyika na Wazanzibari ni wa kawaida na kuonya kuwa hakuna sababu ya kugombea majina ya Tanganyika na Zanzibar bali jukumu la wabunge ni kuangalia wananchi wa pande zote mbili.
Alisema muingiliano wa watu wa Bara na Visiwani ulianza tangu mwaka 1964 ndio maana ukienda Zanzibar unawakuta Wamakonde na Wanyamwezi na ukienda Bara unawakuta Wazanzibari.
Alisema kuvunjika kwa Utanganyika kumezuia ukanda na ukabila na kwamba ingekuwepo Tanganyika leo watu wangeshuhudia yanayotokea Zanzibar na Pemba.
Alisema dawa ya kero ya Muungano si vurugu bali ni kuelekea kwenye serikali moja.
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Jang`ombe (CCM), Bw. Mohamed Rajab Soud, alisema anapendekeza Ofisi ya Makamo wa Rais (Muungano) ibadilishwe iwe Kamati ya kushughulikia Muungano.
Naye Mbunge wa Kitibi (CCM), Bw. Adul Marombwa, alisema hata watu wa Bara wana kero zao za Muungano na kutoa mfano kuwa wakati Mbunge wa Bara anawapiga kura 70,000, wa Zanzibar anawapiga kura 5,000 lakini posho inayotolewa kwa wabunge ni ile ile haijali kama unawapiga kura wengi au wachache.
Bw. Hafidh Ali Tahir, Mbunge wa Dimani (CCM), alisema kuna watu wanaojifanya wana hatimiliki ya Muungano.
``Muungano una matatizo kwa sababu kuna mambo ya kudanganya danganya,`` alisema.
Wakitoa maoni yao kuhusu mjadala huo, mashuhuda wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, walisema wao wanaona Muungano ni mzuri na uendelee.
Bw. Rashid, alisema tofauti zinazoonekana sasa hivi, ni mawazo tu ya watu lakini wakikaa pamoja na kutafuta suluhu wataelewana.
Alisema hivi sasa wabunge wana uhuru wa kusema na kutoa maoni yao na kwamba elimu ni muhimu ya kujua mazingira ya Muungano huo.
``Mimi sio mwanasiasa, siwezi kushauri kitu, isipokuwa kwa upande wangu Muungano ni mzuri uendelee,`` alisema.
Mapema juzi, kambi ya upinzani ilisema kuna haja ya kufikiria upya wazo la kurejesha serikali ya Tanzania Bara.
Akiwasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni, Waziri Kivuli wa wizara hiyo, Bi. Riziki Omar Juma, alisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania maana yake ni nchi mbili, Tanganyika na Zanzibar na kwamba katiba ya Tanzania ilipata pigo kubwa na hivyo kujeruhi mkataba wa Muungano.
``Pigo hilo ni mabadiliko ya 14 ya katiba yaliyomuondolea Rais wa Zanzibar nafasi ya kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania,`` alisema.
Alisema leo hii, Rais wa Zanzibar ni waziri wa kawaida katika Serikali ya Muungano na kwamba makubaliano ya Muungano yamevunjwa na kupotoshwa kwa kiwango alichoita ``cha kupindukia``.
Akizungumzia akaunti ya pamoja ya fedha, kama mfano wa hoja yake, alisema Ibara ya 133 cha Katiba inasema akaunti hizo za pamoja zinawekwa fedha za serikali mbili kwa viwango vitakavyowekwa na Tume ya Pamoja ya Fedha.
``Kwa hiyo, kikatiba ni Serikali ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zina wajibu wa kuchangia huduma na uendelezaji wa Muungano.
Tanzania Bara haichangii wala haiwajibiki kwa mujibu wa katiba,`` alisema na kuongeza: ``Ni hapa ndipo sasa unapoona kwamba kumbe kulitakiwa kuwepo na Serikali Tatu; Tanzania Bara, Muungano na SMZ.``
Kambi hiyo ilisema Bunge lina historia kuwa chombo kilichotumiwa na wabunge 55 wa Bara kudai Serikali ya Tanganyika.
``Ni maoni ya kambi kuwa hoja ile ilikuwa sahihi kama ilivyo sahihi leona itakavyokuwa sahihi kesho,`` alisema.
Aliongeza kuwa Tanzania inahitaji muungano wenye serikali tatu ili kuondoa manung`uniko yasiyokwisha, tume zisizokuwa na mwisho, vikao visivyokwisha, mambo alisema yanapoteza fedha za walipa kodi zinazowezesha kukaa na kujadili masuala ya maendeleo na mustakabali wa nchi.
``Tunajidanganya kuamini kuwa Tanzania Bara si serikali,`` alisema.
SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako