Tulianza kufanya biashara kwa takribani miaka miwili iliyoputa na tukajenga vibanda vyetu eneo hilo, tulitumia biashara hiyo kuendesha familia zetu kwa kipato ambacho tulikipata hapo.
Miezi ya hivi karibuni kukatokea mvutano baina ya pande mbili ambazo zote zilijitambulisha kuwa zinamiliki eneo hilo.
Upande wa kwanza ni Ofisi ya World Oil ambao walitutaka tuhame eneo hilo wakidai ni la kwao, tuliwapinga na tukawasilisha malalamiko yetu kwa Ofisi ya Katibu Tawala Kigamboni, akawaandikia barua ya wito ili kujadili suala hilo.
Mazungumzo yakafanyika kati yetu Wafanyabiashara na World Oil tukakubaliana nao kuwa watatulipa fidia ili kuondoka eneo hilo, japokuwa kulikuwa na upande wa pili wa mmiliki mwingine ambaye ni mfanyabaishara maarufu naye alidai lile eneo ni lake.
Wakati tunasubiri kujua hatma ya eneo hilo, tumekuta miundombinu ya biashara zetu yote imebomelewa usiku, hatujui aliyebomoa lakini taarifa tulizopewa ni kuwa World Oil ndio wamehusika kubomoa maeneo yetu.
Tunaomba Serikali itusaidie kwani, kama ni mgogoro ulikuwa unaendelea kutafutiwa utatuzi ila kuna Wahuni wamejitokeza na kuvunja, wameharibu mitaji yetu, tumebaki na majuto.
Huyu ni nani ambaye ana nguvu kiasi cha kubomoa bila kibali na bila taarifa huku vitu vyetu vingi vikiwa ndani, kuna hasara kubwa imepatikana, tunaomba msaada wa Serikali Kuu inaonekana aliyefunja ana nguvu kuliko hata mamlaka za Serikali nyingine zilizowekwa huku Kigamboni.