Anaandika Dr. Christopher Cyrilo
Ulichofundishwa kwenye somo la uraia sio kweli. Kenge wewe!
Ulikuwa mwanafunzi bora darasani kuliko wengine, walimu wakakuita 'jiniasi'. Na wewe ukakenua meno na kuchekelea...utafikiri 'jiniasi' kweli!
Ulisoma kwa bidii zote, usiku na mchana - si kwa lengo la kuvuna maarifa bali kufaulu mitihani, ukafaulu bila maarifa. Sio kosa lako, ni mfumo wa elimu yetu unaomfanya mwanafunzi kuogopa mitihani zaidi kuliko kupenda kujifunza, anasema Mwl. Mabala.
Na sasa umekuwa mtu mzima, unashangaashangaa tu. Unachokishuhudia ni tofauti na kile ulichojaza kwenye mtihani wa Uraia uliyofaulu vema kuliko marafiki zako wengi.
Ulifundishwa eti Taifa linaundwa na mihimili mitatu, Serikali, Bunge na Mahakama, Uongo. Taifa linaundwa na Serikali, Serikali na Serikali. Spika wa bunge na jaji mkuu wote wanasujudu kwa kiongozi wa serikali, na wanaelekezwa cha kufanya na wao wanafuata bila hiyana. Wakikataa watakiona Cha mtemakuni. Kile ulichofundishwa eti mihimili mitatu inayojitegemea ni uongo mtupu.
Ukaambiwa eti viongozi wanachaguliwa na wapiga kura, Uongo.
Viongozi wanachaguliwa na wanaojumuisha mahesabu ya kura. Unapoacha shughuli zako kwenda kupanga foleni ya kupiga kura, sio kwamba ndio unachagua kiongozi - no - no - no, pale unawaongezea kazi wanaohesabu kura tu. Kura zikiwa nyingi ujue watachelewa kumtangaza mtu wanaomtaka wao. Hilo ulikuwa hujui? Wewe kweli ni pimbi.
Ukaambiwa Polisi ni walinzi wa raia na mali zao, na wewe ulivyo kilaza ukaamini kabisa! Kilaza mkubwa wewe!
Polisi ni walinzi wa viongozi wa nchi na matajiri dhidi ya masikini wasumbufu wanaojifanya kudai haki wakati hawana haki. Polisi ni ukuta unaotenganisha wananchi na 'WENYENCHI'. Na Kama hujui basi kuanzia leo ujue - masikini aliyekwapua kuku wa jirani anastahili adhabu kubwa hata kifo wakati tajiri aliyeibia serikali milioni 7 kwa kila dakika anasamehewa. Unakodoa macho?
Unasubiri mkuu mmoja wa mkoa atekwe - apotee uone jeshi la polisi litakavyohangaika? Sasa potea wewe! Watasema umejiteka au umekwenda kutembelea ndugu.
Halafu kuna lile suala la binadamu wote ni sawa! Na wewe uliamini kabisa?
Sikiliza, hata waasisi wa Taifa la Marekani, akina George Washington waliandika hivyo kwenye katiba yao, wakati huohuo wakiwa na mashamba makubwa yenye watumwa kibao wakiwafanyisha kazi za kitumwa. Bado unaamini binadamu wote ni sawa? Muone! wapo binadamu wengine ni sawa zaidi ya wengine - usipoelewa hapo sio tatizo langu.
Ndio maana kuna watu wanakunywa na kupikia tope huko Lindi kwa kukosa kisima cha Milioni 5, huku wengine wanapiga vigeregere mbele ya Dreamliner la Bilioni 500, na baadhi yao hawatalipanda hadi wazeeke wafe. Si binadamu wote ni sawa. Umeelewa we tumbili?
Elimu ni ufunguo wa maisha eti? He hee! Daah. Ungejua! Kuna profesa aliwahi kujizolewa umaarufu na kuonekana moja wa watu muhimu katika kuamua mustakabali wa nchi, leo ni mpumbavu mbele ya mtu aliyeghushi vyeti vya PhD! Unatoa macho? Jichunge na vumbi.
Elimu haiondoi ujinga, bali inampa mtu uwezo wa kuujua zaidi ujinga wake ili ajichunge, na hiyo haimaanishi kuwa elimu ni ufunguo wa maisha. Ujinga ndio ufunguo wa maisha na kadiri unavyokuwa mjinga ndivyo unavyofanikiwa zaidi- kama alivyosema mwandishi nguli wa zamani Mark Twain; "Ili ufanikiwe maishani unahitaji vitu viwili, Ujinga na kujiamini". Wajinga wengi wanaojiamini wametoka kwenye maisha kuliko wanaojifanya werevu... Ujinga ndio ufunguo wa maisha. Wewe endelea kujifanya mwerevu kwa sababu eti ulifaulu darasani! Faulu na maisha sasa! Ha haaa.
Tuache sisi wajinga tukomae na mapambio ya kusifu - kusifu - kusifu na kuabudu...na tukishateuliwa -nakwambia mtakoma. Mlijifanya sana kufaulu darasani sisi tukawa tunawachora tu... Eti wataalamu, utaalamu bongo!!! mapimbi wakubwa!
#JingaMimi