Tundu Antipas Lissu: Historia na harakati zake katika siasa za Tanzania...

Tundu Antipas Lissu: Historia na harakati zake katika siasa za Tanzania...

Tundu Lissu.
Aliwatesa alipokuwa Mwanafunzi,
Aliwatesa alipokuwa Mkufunzi,
Aliwatesa alipokuwa Mwanasheria,
Aliwatesa alipokuwa Mwanaharakati,
Aliwatesa alipokuwa Mwanasiasa,
Amewatesa akiwa Mbunge,
Anawatesa muda huu yu HOI MAHUTUTI,
Atawateseni hata atapokuwa mikononi kwa Baba.
Damu yake haitowaacha salama.

SOMA HISTORIA YA SHUJAA TUNDU ANTIPAS LISSU NA HARAKATI ZAKE NCHINI.
MH. TUNDU ANTIPASS MUGWAI LISSU NI MZALENDO AU MCHOCHEZI?

Kwa muda mrefu mjadala mkubwa usio rasmi umetamalaki nchini iwapo Mh. Lissu ni mzalendo au mchochezi. Nikaona nijaribu kufuatilia maisha yake ili kuona kama naweza kutengua kitendawili hiki.

Lissu alizaliwa tarehe 20 Januari 1968 na alisoma shule ya msingi Mahambe, Singida. Kabila myaturu .
Katika miaka yake yote saba shuleni hapo, Lissu hakukubali hata mara moja kuamka alfajiri saa 11 kuwahi namba na daima aligomea kulima mashamba ya walimu, kuwachotea maji na kazi za namna hiyo kwani kwake aliona haziko sahihi. Hii ilipelekea awe anatandikwa bakora mara kwa mara. Shuleni hapo, bakora na mwili wa Lissu vilikuwa ni kama uji na mgonjwa. Hata hivyo, kilichomsaidia ni akili yake. He was a very, very brilliant pupil.

Lissu alifaulu mtihani wa darasa la saba na kwenda shule ya sekondari ya Ilboru, Arusha. Shuleni hapo, yeye ndie aliyekuwa mwanafunzi mdogo kuliko wote. Licha ya udogo wake, alikuwa mwiba mkali kwa prefects na walimu. Akiwa kidatu cha tatu wenzake walimtaka awe prefect lakini alikataa kwani alizoea kuwaita "manyoka" kwa tabia yao ya kupenda kupeleka taarifa za wanafunzi kwa walimu.

Lissu alifaulu vizuri na kuingia kidato cha tano shule ya sekondari ya Galanosi, Tanga. Akiwa Galanosi, akapewa Uenyekiti wa Kamati ya Taaluma. Hata hivyo, akakorofishana vibaya mno na mwalimu wa taaluma na kuvuliwa cheo hicho.

Akiwa kidato cha sita mwaka 1988, kulikuwa na disko la graduation. Kidato cha sita wakaruhusiwa kwenda kucheza na Korogwe girls lakini kidato cha nne wakakataliwa na wakaambiwa wataletewa taarabu shuleni hapo. Lissu aliona huo ni uonevu na daima shuleni hapo alichukia mno mwanafunzi mwenzake kuonewa hata kama ni wa madarasa ya chini. Hivyo, akaandika Waraka "TAARAB FOR WHOSE INTEREST". Lissu hakuandika jina lake kwenye Waraka huo. Akaubandika kwenye ubao wa matangazo usiku. Walimu walipouona walichukia sana na wakachunguza na kuhisi mwanafunzi pekee aliyepinda shuleni hapo mwenye ubavu wa kuandika vitu kama vile ni Lissu tu hivyo wakamkamata. Walimu wakamwita Lissu mchochezi na hivyo akapewa suspension. Hata hivyo, baadae akarudishwa shuleni na kisha akafanya mtihani wa kidato cha sita.

Mwaka 1989 akaenda Mafinga JKT kisha Itende JKT kwa mwaka mmoja. Wakati huo, vuguvugu la vyama vingi lilikua limepamba moto nchini huku CCM ikiwa haitaki kabisa kuskia mambo ya vyama vingi. Katiba ya CCM ilikuwa inautambua Mkoa wa Majeshi hivyo ilituma viongozi wake kutembelea kambi zote na kuulezea msimamo wa CCM kutotaka kuskia takataka inayoitwa vyama vingi.

RPC Omary Mahita (Rukwa) na Kanali wa Andrew Shija wakitokea Mkoa huo wa Majeshi wakapangiwa kwenda Itende JKT kuwaelezea servicemen msimamo wa chama. Walipofika wakaitisha mkutano mkubwa na ukumbi ukawa umefurika. Katika mkutano huo, Mahita na Shija wakaeleza kwamba "Sisi haya mambo ya vyama vingi hayatuhusu. Haya ni mambo ya wazungu huko Ulaya mashariki hivyo tusiyashabikie".

Kitu ambacho viongozi hao hawakukijua ni kwamba miongoni mwa servicemen hao alikuwepo kijana mmoja very brilliant mwenye uelewa mkubwa wa mambo mengi yanayoendelea duniani asiye na simile kuongea kilichomo akilini mwake.

Lissu alikuwa ameskiliza hotuba ya Baba wa Taifa alipoongea na Baraza Kuu la Umoja wa vijana wa CCM Mwanza wiki chache kabla ya mkutano huo wa akina RPC Mahita. Mwalimu alikuwa amesema -"Wanaodhani mageuzi hayatuhusu bali yanazihusu nchi za Ulaya mashariki pekee ni wajinga kwani Tanzania sio kisiwa".

Muda wa maswali ulipofika huku wengi wakiamini hakuna atakaekuwa na ubavu wa kuuliza swali, Lissu bila kuogopa na kwa ujasili wa hali ya juu ambao haukuwahi kuonekana hapo Itende JKT, akanyoosha mkono. Servicemen wenzake waliokuwa wakijua misimamo yake isiyoyumba walijitahidi kumshusha mkono bila mafanikio. Huku akitumia lugha kali bila kumun'gunya maneno kama kawaida yake, Lissu aliwauliza viongozi hao -"Je, mjinga ni Baba wa Taifa aliyesema mageuzi ya vyama vingi yanatuhusu au ni nyie mnaosema hayatuhusu?"

RPC Mahita, kwa wajihi, ni mweupe sana lakini swali hilo lilimbadilisha na kuwa mwekunduuuu. Ghafla bin vuu maafande wakamkimbilia Lissu kutaka kumkwida kwa "kosa" la kutukana meza kuu. Bahati nzuri, Kanali Shija akawa na busara na akawazuia na kuwaambia "Huyo kijana Lissu yupo sahihi kwani hicho ndicho alichosema Baba wa Taifa." Huo ndio ukawa mwisho wa mkutano.

Baada ya songombingo na tafrani hiyo ya kipekee siku hiyo , maafande wote wa Itende JKT wakaanza kumuogopa sana Lissu wakiamini yeye ni mtu wa Usalama wa Taifa na akawa hapangiwi tena kazi bali akawa anakula shushi hadi kumaliza muda wake!

Kutokana na kufaulu vizuri kidato cha sita, Lissu alijiunga na kitivo cha sheria mwaka 1991 UDSM. Huko aliendelea na harakati zake za kupigania haki za wanafunzi na akajiunga na NCCR MAGEUZI. Miaka hiyo, chama hicho kilichokuwa chini ya mmoja ya viongozi waliowahi pendwa mno nchini, Mh. Augustin Mrema, ndicho kilikuwa chama kikuu cha upinzani nchini.

Baadae mwaka 1995, Lissu akaenda kusomea shahada ya uzamili chuo cha Warwick UK. Alipofika huko akaomba ruhusa aje kugombea ubunge Singida mashariki. Hata hivyo, kutokana na maandalizi duni, kura hazikutosha hivyo akarejea masomoni.

Lissu alipomaliza masomo yake 1997 alirejea na kufanya kazi ya sheria Arusha. Baadae akaoa na kuhamia Dar Es Salaam. Akawa mmoja wa wanasheria wa chama cha wanasheria wa mazingira (LEAT) pamoja na Dr. Rugemeleza Nshalla na Alex Shauri. Lissu akaanza kujipambanua kama mtanzania anaepigania haki za wanyonge na maliasili za nchi yake bila woga wowote.

Ujasiri wake mkubwa wa kwanza kupigania maliasili za taifa lake ulikuwa mwishoni mwa miaka ya 90. Serikali ya awamu ya tatu ilikuwa imempa raia wa Ireland aitwae Reginald Nolan hekta 20, 000 kuchimba mabwawa ya kambakoche kwenye delta ya Rufiji katika maeneo ya watu yenye vijiji nane waliokuwa wakiishi na wakilima humo. Lissu aliwahurumia sana wananchi hao wanyonge. Hivyo, aliratibu kampeni iliyoendeshwa na LEAT kimataifa kuupinga mradi huo kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kimataifa. Hii ilikuwa ni kazi ngumu mno na yenye vitisho vingi. Ilikuwa si ajabu asubuhi kukuta chini ya mlango wa ofisi ya LEAT Mavuno house barua ya vitisho. Lissu hakujali wala kuogopa.

Kutokana na juhudi kubwa ya Lissu, hatimaye "European Investment bank", iliyokuwa tayari kutoa mkopo kwa Nolan ambao ungedhaminiwa na serikali ya awamu ya tatu, ikakubaliana na hoja kuntu za Lissu na kugoma kutoa fedha hizo. Hivyo, mradi huo ukasambaratika. Huu ulikuwa ushindi mkubwa kwa Lissu na alipongezwa mno na wanavijiji hao wanyonge waliomuona kama Mungu.

Lissu akapata umaarufu na kualikwa kwenye kipindi cha "Hamza Kasongo hour" Octoba 1998 na mzalendo mmoja akawa amempa nyaraka za Baraza la Mawaziri ambazo zilisema mradi huo ni wa hovyo na ulipitishwa kinyemela!

Mwezi Septemba 2000 alikwenda USA kama mtafiti kwa miaka mitatu kwenye kampuni ya World Resource Institute huku akirudi mara kwa mara nchini kuendelea na kazi za LEAT.

Mwaka 2001 yeye na wenzake wa LEAT walifanya Press conference maelezo na kudai wana ushahidi wa video kuhusu mauaji ya Bulyankulu. Yeye akarudi US lakini wenzake wakakamatwa. Akaskia imeelezwa ametoroka na atafutwa na Interpol. Akarudi na akakamatwa. Akasachiwa nyumbani kwake na kupelekwa Central. Akafanya ujanja na kuingia na simu na usiku kucha akawa anawasiliana na magazeti ya US na Canada. Hiyo ikamsaidia kuondokana na msala huo.

Je Lissu aliingiaje CHADEMA?

Lissu alijiunga CHADEMA kimazabe mwaka 2004. Mwaka 2003, Lissu alikwenda Tarime kwenye masuala ya madini. Akakutana na Mh. Chacha Wangwe akiwa Diwani wa Tarime akiwa na kesi kumi za jinai. Mh. Wangwe akamwambia Lissu kuwa wanataka kumfunga. Lissu akamwambia aondoe hofu hawataweza.

Mh. Mbowe akampigia simu Mh. Lissu kumuomba amtetee Mh. Wangwe kwenye hizo kesi zilizokuwa zikifunguliwa kila uchao. Lissu akakubali na akafanya kazi yake kwa weledi wa hali ya juu. Mh. Lissu akasaidia pia kushinda kesi za wananchi wanyonge 366 katika kipindi cha miezi minne tu. Hawa ni wananchi waliokuwa wakiishi pembezoni mwa migodi kabla ya kuswekwa ndani kwa kosa la kuvamia migodi hiyo. Lissu aliwatetea bure wananchi hawa mafukara na baada ya ushindi wa kesi hizo akatamka-"Uwekezaji umegeuka kuwa unyama Tanzania". Lissu akaonekana ni mtu asiye na uzalendo na taifa lake kwa kuwasema vibaya wawekezaji ambao serikali ilikuwaikidai walikuwa wakiliingizia taifa mapato makubwa. Hata hivyo, kwa wananchi hao wanyonge, Lissu alionekana ni Mfalme.

Baadae Mh. Mbowe akampigia Lissu na kumuomba asaidie kutafuta wanasheria wengine waingie CHADEMA kama yeye. Lissu akamshangaza Mh. Mbowe kwani bila kupepesa macho wala kutikisa maskio, Lissu akasema yeye ni mwanachama wa NCCR MAGEUZI! Mh. Mbowe alistaajabu sana kwani aliamini Lissu ni mwanachama wa CHADEMA. Hivyo, Lissu akamwambia Mh. Mbowe "kama unataka nijiunge nanyi basi najiunga" ndivyo Lissu alivyojiunga CHADEMA.

Lissu aliendelea na jitihada zake kuwasaidia wananchi waliokuwa wakinyanyasika migodini huku akiacha wateja wenye fedha nyingi Dar Es Salaam. Kwa Lissu, hakuna kitu kinamuuma moyoni mwake kama akiona mnyonge ana haki lakini anaonewa. Lissu kamwe hawezi kukaa kimya kuona hali hiyo ikiendelea.

Jitihada hizi zikamfanya Lissu azidi kukorofishana na serikali mara kwa mara. Serikali ikamwita ni mchochezi anaechochea wananchi kuwachukia wawekezaji wa Barrick ambao serikali ilikuwa ikidai ni wawekezaji wazuri waliokuwa wakiliingizia taifa pato kubwa.

Lissu amekuwa mstari wa mbele kwenye harakati za kutetea sekta ya madini nchini. Kwa miongo zaidi ya miwili amekuwa akipambana na wawekezaji wazungu waliokuwa wakikingiwa kifua na serikali ya awamu ya tatu na ya nne na kuonekana yeye si mzalendo. Alikuwa ni mmoja wa waliopinga hadharani na kwenye maandiko yake, sheria ya madini ya mwaka 1998 na ya 2010 kwa hoja kwamba zinawatajirisha wawekezaji wazungu na kutuachia watanzania mashimo tu na umaskini mkubwa wakati Mungu aliibariki nchi hii kwa kuipa madini mengi. Hoja hizi zilikuwa zikikejeriwa na wabunge wa CCM ambao walikuwa wakiipitisha miswada hii kutokana na wingi wao bungeni. Aidha, Lissu alipinga vikali kupitishwa na bunge sheria zote za madini kwa hati ya dharura mwaka 2015 na 2017.

Licha ya jitihada hizi kubwa za kuwapigania wananchi wanyonge na maskini huku wengi akiwatetea mahakamani bure na kupambana vikali na wawekezaji wa makampuni ya madini ambayo yeye miaka yote amekuwa akiyaita ni ya wezi wanaotuibia madini yetu na kunyanyasa wananchi migodini, Lissu anaonekana kwenye macho ya baadhi ya watu kwamba si mzalendo bali ni "kibaraka anaetumiwa na wazungu asieitakia mema nchi yetu".

Je Mh. TUNDU ANTIPASS MUGWAI LISSU ni mzalendo au Mchochezi? The ball is in your court!

Naomba nimalizie makala yangu kwa nukuu hizi kuntu toka kwa viongozi wetu watatu wapendwa:

1."Mtu mwenye weledi huwezi tu ukakubali kila unachoambiwa. Unatakiwa kuwa kama Mbayuwayu. Akili zako unachanganya na za kuambiwa kisha unapata jibu".
MH. JAKAYA KIKWETE

2."Watanzania tumeibiwa sana haya madini yetu. Tumechezewa kiasi cha kutosha lazma tufike mahali tuseme imetosha. Sijui watanzania tumerogwa na nani? Basi tuwaombe mapadri, wachungaji na mashehe watuombee ili mapepo yatutoke. Kwa maamuzi haya mabovu ipo siku vizazi vyetu vitakuja kuyatafuta makaburi yetu na kuyapiga mawe".
MH. DR. J. MAGUFULI
12.6.2017

"Mzalendo wa kweli wa Taifa hili ni yule aliyeivishwa vizuri na TANU au ASP aliyetayari kujitoa muhanga kulipigania taifa lake kwa akili na nguvu zake zote bila woga kupambana na mabeberu na manyan'gau yasiolitakia mema taifa letu iwe kwenye mapambano ya kiuchumi au ya kulinda kulinda mipaka ya nchi yetu".
JK NYERERE, BABA WA TAIFA, 1.3. 1971
Yupi mzalendo ?

Lakini pia
HISTORIA FUPI YA MZALENDO WA KWELI TUNDU LISSU KAMA ILIVYOANDIKWA NA GAZETI LA RAIA MWEMA MWAKA 2012

Lissu: Niliishi maisha ya furaha sana ya utoto. Tangu nikiwa shule ya msingi ni kama vile nilikuwa mwanaharakati. Unajua shuleni kuna shughuli nyingi sana kama kuchota maji kwa ajili ya walimu, kulima mashamba ya walimu na kupanda. Nilikuwa nikiona haya mambo hayako sawa, lakini pia kuna suala la kuwahi shuleni.

Sikumbuki kwa miaka saba ya shule ya msingi, kama kuna siku nimewahi zile namba. Siku zote nilikuwa mchelewaji na nimechapwa kweli.

Raia Mwema: Ni ukaidi wa makusudi?

Lissu: Siwezi kusema ni makusudi, lakini tatizo ni kuamka alfajiri saa 11 ili saa 12 niwe shuleni. Kwa hilo nilikuwa rebel (muasi). Pia sikumbuki mahali ambako sikuwahi kubishana na walimu iwe primary school, secondary school, iwe chuo kikuu, siku zote imekuwa hivyo.

Lakini vile vile nilizaliwa katika familia ambayo mijadala ya kisiasa ilikuwa sehemu yetu. Baba yangu alisoma hadi darasa la sita, mama yangu hakusoma kabisa.

Kila jioni tunasikiliza kwanza taarifa ya habari na idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani; baada ya hapo ni mjadala mpaka saa tano au sita, mjadala wa kisiasa kuhusu mwenendo wa mambo duniani. Nilikuwa mtoto mdogo sana, lakini nilikuwa na ufahamu.

Nafikiri nilikuwa miaka sita au saba hivi.

Wakati nikiwa darasa la kwanza (1976), nilikuwa nafahamu karibu viongozi wote duniani na miji mikuu mashuhuri.

Raia Mwema: Kutokana na ufahamu huo, ni viongozi gani hapa nchini walikuvutia wakati huo?

Lissu: Ni swali gumu kidogo. Si rahisi sana kusema nilivutiwa na Mwalimu Nyerere. Ukweli ni kwamba hapana, alikuwa sehemu ya mazungumzo ya kisiasa nchini. Siwezi nikasema nilivutiwa sana na Mwalimu.

Raia Mwema: Unaposikia jina la Julius Nyerere kwa sasa, unakumbuka nini?

Lissu: Ni hotuba za Mwalimu Nyerere kuhusu vita dhidi ya Uganda. Wakati huo nikiwa darasa la tatu mwaka 1978, nchi iko vitani tulichangishwa (familia) ng’ombe.

Baba yangu alitoa ng’ombe watatu kama sikosei ili kusaidia vita mpakani. Shuleni tuliimbishwa sana nyimbo kwamba Iddi Amini ni nyoka; ingawa baadaye nimekuja kugundua kwamba inawezekana kuna vitu vingine vingi hatukuambiwa kuhusu mgogoro wetu na Uganda.

Nakumbuka pia wakati huo tukiwa wadogo tulichimbishwa mahandaki. Nilikuwa na miaka 10, nilishangaa tunachimba (mahandaki) nje ya nyumba yetu halafu siyo marefu sana.

Lakini kuna kitu kingine kilichotafsiri mtazamo wangu kuhusu serikali ambao sio chanya sana. Nilipokuwa miaka kama sita hivi, nyumba yetu na wanavijiji wengine zilibomolewa halafu tukaachwa tu. Kina mama wanalia, kila mtu analia; halafu hawa watu wakavunja nyumba wakaondoka.

Raia Mwema: Hao wavunjaji walitumwa na nani?

Lissu: Unajua ukiwa na miaka 10 huulizi sana. Ni tukio ambalo haliwezi kuondoka katika kumbukumbu zangu kwamba; serikali inaweza kufanya vitu visivyo na akili (mantiki).

Sisi na wanakijiji wengine tumejenga nyumba, ingawa pengine hazikuwa nzuri sana wao (serikali) wametubomolea kwa jina la Operesheni Vijiji.

Baba yangu alikuwa Mwenyekiti wa Kijiji wakati huo, baadaye (watendaji wa serikali) wakaja na kamba za katani na wataalamu ili kupima namna ya kujenga nyumba za kisasa, wanaita maendeleo.

Kwa hiyo, wazee wanatembea na kamba ya katani wanapima namna ya kujenga nyumba za kisasa, zijengwe kwa mstari ulionyooka. Lakini hatimaye hawakutujengea wala kutusaidia chochote.

Hali hiyo ilinifanya niamini kwamba pengine serikali haina watu wenye akili sana kama nilivyokuwa nikifirikia mwanzoni.

Raia Mwema: Ukiwa katika umri wa utoto, unakumbuka nini enzi za nchi kufunga mikanda na baa la njaa lililowahi kutokea?

Lissu: Kuna njaa ya mwaka 1974 serikali ilileta chakula kudhibiti njaa hiyo, nakumbuka kuna kitu (chakula) kinaitwa burga ilikuwa sijaanza shule baadaye tukaletewa ugali wa muhogo. Sisi kwetu tunakula muhogo wa kuchemsha. Ilikuwa hali tofauti.

Raia Mwema: Tueleze safari yako kielimu, ilikuwaje…ngumu au nyepesi tu.

Lissu: Wakati wa Operesheni Vijiji ilitokea mvutano wa kuhama. Baba yangu pamoja na wazee wengine walisafiri kutoka kijijini Singida wakaja Dar es Salaam kulalamika.

Walilalamika kwamba tunatakiwa tuhame kwenye kijiji chenye mashamba makubwa. Wakaja kupiga kelele na serikali wakati huo iliwasilikiza.

Lakini ikaibuliwa hoja kwamba; tuhame (kijiji) kwa sababu hakuna shule. Wakati ule, hoja ya vijiji vya ujamaa ililazimisha kuwapo huduma za kijamii.

Sasa ili kukabili hoja hiyo na tusiweze kuhamishwa, kuna mzee mmoja alijenga nyumba yake mpya, akasema sitahamia ili iwe shule ya watoto. Kwa hiyo, tukaanza shule lakini shida walimu.

Mmoja wa wadogo zake baba yangu wakati huo alikuwa amemaliza darasa la saba, hana pa kwenda, wakasema atakuwa mwalimu. Kuna mama mwingine mjanja mjanja kijijini, naye wakamwambia atakuwa mwalimu.

Kwa hiyo, tukaanza darasa la kwanza Aprili 5, 1976. Shule za miaka ile zilikuwa zinaanza Januari, lakini ya kwetu tulianza Aprili, kwenye nyumba ya tembe sio ya bati, na walimu wasio na mafunzo yoyote.

Hatukuwa na vitabu, swali likawa tutaandikia nini? Wazee wakachanga hela wakamtuma mtu Dar es Salaam aende kumtafuta mtu anaitwa Abdallah Nungu, amueleze tatizo la vitabu shuleni.

Kwa hiyo, tukamsuburi kwa wiki mbili huyu bwana alete vitabu. Akarudi na boski kubwa la vitabu na vile vibao vya kuandikia, ingawa awali tulikuwa tukiandika chini (ardhini). Hivyo ndivyo tulivyoanza shule wengine.

Lakini hilo lilikuwa darasa la kwanza kwenye hiyo nyumba ya mzee. Tatizo likajitokeza ni darasa la pili litakaa wapi, kwa sababu ilibidi darasa la kwanza wengine waanze.

Nyumbani kwetu baba alijenga nyumba jirani na mdogo wake, lakini huyo mdogo wake hakuwa akiishi hapo kijijini alikuwa Moshi, nyumba yake haikuwa ikikaliwa.

Mzee akasema darasa la pili hilo hapo (nyumba ya mdogo wake). Kwa hiyo, darasa la pili tukahamia kwetu (nyumbani). Natoka mlango huu, naingia mlango wa pili niko darasani. Baada ya hapo, tukaanza ujenzi wa shule ambayo ikaitwa Shule ya Msingi Mahambe.

Raia Mwema: Serikali haikutoa mchango wowote katika hatua za awali za ujenzi?

Lissu: Hatukusaidiwa na serikali katika ujenzi. Ilikuwa asubuhi tunakwenda shule, saa nane tunaporudi (shule) tunabeba vibuyu na ndoo za maji pamoja na mama zetu kupeleka eneo la kufyatulia matofali; shughuli iliyokuwa ikifanywa na baba zetu.

Mwaka mzima tumefyatua matofali na baadaye kuanza ujenzi. Kule kwetu kuna Wakatoliki wengi, pale eneo la ujenzi (wa shule) kulikuwa na padre anapita kwenda kusalisha kijiji cha jirani kila Jumatano. Kila akipita anakuta ujenzi unaendelea na watoto wanasaidia.

Huyo padre anaitwa Charles ni mu-Irish, kila siku anapita pale anakuta watoto na wazazi wanafanya kazi, nadhani alikuwa akijiuliza kuna nini?

Siku hiyo akasimama. Alikuwa anatumia pikipiki kubwa….sijui ni kubwa (pikipiki) kweli au mimi ndiye nilikuwa mtoto na kuiona kubwa.

Akauliza, akaambiwa tunajenga shule. Akauliza serikali iko wapi? Akaahidi tukishamaliza ujenzi, ataleta mafundi kukamilisha kwa kuweka bati, ikaitwa Shule ya Wazazi.

Darasa la tatu tukaingia sasa kwenye darasa zuri na bora. Kuanzia hapo, kila mwaka nilipokaa pale shule ya msingi tulikuwa tunajenga darasa moja moja, hadi tulipomaliza mwaka 1979 tunaingia darasa la tano ndiyo kwa mara ya kwanza ikaitwa Shule ya Msingi Mahambe, na tutakaletewa mwalimu wa serikali.

Kwa hiyo, kati ya vyuo vikuu vyangu, chuo kikuu cha kwanza ni hicho….miaka minne ya kufundishwa na walimu wasio na mafunzo yoyote.

Siku hizi nikipita nikiwaambia watu shule niliyosomea na walimu walionifundisha, hawaamini. Tulifundishwa na wanakijiji kabisa wasio na mafunzo! Serikali ilipoanzisha mpango wa UPE wale walimu walijiendeleza, wakaenda vyuoni na wapo ambao wamekuwa waalimu wanataaluma.

Raia Mwema: Hayo ni ya shule ya msingi, tueleze ya sekondari, unakumbuka nini hasa?

Lissu: Cha kwanza nimetoka nje ya kwetu (Singida), nimeenda kusomea Ilboru Sekondari, Arusha. Pale (Ilboru) maisha yalikuwa mazuri na nilikuwa mdogo kuliko wengine wote (wanafunzi).

Sikuwahi kuwa kiongozi shuleni, na sikutaka uongozi. Viongozi wakati ule tuliwaita manyoka kwa sababu wanapeleka habari kwa walimu.

Lakini baadaye nilipoingia kidato cha tano na sita, Galanos Sekondari (Tanga), nilipewa uenyekiti wa Kamati ya Taaluma, lakini baada ya miezi sita hivi nikagombana vibaya sana na mwalimu wa taaluma, ikabidi nivuliwe madaraka.

Raia Mwema: Mlitofautiana katika jambo gani na mwalimu wa taaluma?

Lissu: Ni msimamo tu. Ilitokea kwamba mwaka 1988 niko kidato cha sita, sasa kidato cha nne na cha sita kila mwaka hufanya graduation (mahafali). Wakati huo, hasa Galanos na shule nyingi za sekondari, disko hazikuwa nyingi (mara kwa mara) kama sasa.

Kipindi cha kwenda kucheza disko ilikuwa wakati wa graduation. Sasa walimu wakaamua watoto wa kidato cha nne hawatakwenda kucheza disko. Mimi niko kidato cha sita, sasa tulipanga kwenda disko Korogwe Girls. Wakaamua (walimu) kidato cha nne hawatakwenda Korogwe Girls, badala yake waletewe taarabu.

Sikukubaliana, nikaandika makala inahoji uamuzi huo. Title yake naikumbuka hadi leo, inasema; “taarab for who’s benefit?” – taarabu kwa faida ya nani?

Halafu tukafanya mpango (wanafunzi) ikabandikwa kwenye mbao za matangazo shuleni, sikuandika jina langu halisi. Walimu wakauliza, wakapeleleza nani anaweza kuandika vitu kama hivi?….wakanikamata.

Nikatuhumiwa kuleta uchochezi, nikasimamishwa shule, baadaye walinirudisha. Lakini kwa ujumla miaka ya sekondari ilikuwa mizuri, hapakuwa na njaa kama wakati huu.

Raia Mwema: Baada ya kuhitimu kidato cha sita, nini kilichofuatia?

Lissu: Nikaenda JKT Mbeya, kwanza nilipelekwa Mafinga, lakini sikukaa tukapelekwa Mbeya operesheni yangu inaitwa; Operesheni ya Programu ya Chama, mwaka 1989.

Raia Mwema: Unakumbuka nini kuhusu enzi za JKT?

Lissu: Ninachokumbuka mjadala wa vyama vingi ulikuwa umeiva na CCM hawataki vyama vingi. Ilikuwa mwaka 1989/1990, kwa Katiba ya CCM wakati huo, kulikuwa kuna mkoa unaitwa Mkoa wa Majeshi, ulikuwa mkoa sawa na mingine katika chama.

Kwa hiyo, wakatuma wajumbe wao wa Mkoa wa Majeshi kutembelea kambi zote za jeshi na JKT Tanzania nzima, kueleza msimamo wa CCM.

Waliokuja Itende JKT kwetu nawakumbuka ni Omari Mahita wakati huo ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Kanali Andrew Shija na mtu mwingine simkumbuki.

Nawakumbuka Kanali Shija na Omari Mahita kwa sababu walijenga hoja kwamba haya mageuzi (vyama vingi) hayatuhusu kwa hiyo tusishabikie yasiyotuhusu; eti yanayowahusu Wazungu, Ulaya Mashariki na kwingine.

Nakumbuka nilipambana vibaya sana na Omari Mahita kwenye huo mkutano. Nilisimama kuuliza maswali nikitambua kuwa kabla hawajaja, Mwalimu Nyerere alihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Vijana wa CCM, Mwanza na akasema wanaodhani mageuzi ya Ulaya Mashariki hayatuhusu, ni wajinga.

Kwa hiyo, nikamuuliza RPC Omari Mahita nikamwambia kwamba Mwalimu Nyerere alisema wanaofikiri mageuzi ya Ulaya Mashariki hayatuhusu ni wajinga, na wewe umekuja na timu yako unatuambia haya mambo ni ya Wazungu hayatuhusu.

Sasa mjinga ni Mwalimu Nyerere aliyesema yanatuhusu au nyie ambao mnatuambia kwamba hayatuhusu?

Raia Mwema: Bila shaka ulitumbukia katika uhasama wa ghafla na meza kuu. Hali ilikuwaje?

Lissu: Omari Mahita ni mweupe sana, basi, ghafla akabadilika rangi akawa mwekundu. Ikawa makamanda kadhaa wakasimama tayari kumshughulikia huyu serviceman…maana nilishapita ukuruta. Wakasimama kutaka kumshughulikia anayetukana maofisa wa jeshi.

Lakini kanali Shija (marehemu sasa) akasimama akanitetea. Akasema; hoja ya serviceman ni sahihi kabisa, Mwalimu ndivyo alivyosema. Kwa hiyo, hatuwezi….kusema hayatuhusu. Maana yake tayari nilianza kusakamwa pale… akasema ni kweli hatuwezi kukwepa haya mawimbi na upepo. Shija akapiga siasa, na hatimaye akaniepushia kibano.

Raia Mwema: Kwa hiyo makamanda wenyewe kwa wenyewe walitofautiana mbele yenu?

Lissu: Walitofautiana na baada ya hapo, hakuna ofisa wa JKT aliyenigusa tena. Wengi baada ya hapo wakaamini mimi ni usalama wa taifa.

Maisha yakawa mazuri. Hakuna aliyenigusa kwa sababu kama nimezungumza vile na kanali wa jeshi, kwa sababu mkuu wa kambi mwenyewe hakuwa kanali, alikuwa luteni kanali, sasa mimi nimetetewa na Kanali Shija. Kwa hiyo nilikuwa nakula shushi (mambo mteremko).

Baada ya hapo nikaenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Miaka ile ulikuwa huendi chuo kikuu kama si mwanachama wa CCM na sehemu ya mafunzo unayopata JKT ni pamoja na itikadi ya CCM na mnapomaliza mafunzo mnakabidhiwa pia kadi za chama. Kwa hiyo, nilikuwa mwanachama wa CCM na hiyo ni muhimu watu wakafahamu.

Lakini nilikuwa mwanachama kwa sababu tu nilitaka kusoma. Ndivyo maisha yalivyokuwa na baada ya hapo. Nilipoingia chuoni kadi haikuwa na kazi sana kwangu. Siku ya kwanza chuo kikuu hadi naondoka, mijadala yote nilikuwa mstari wa mbele kabisa pamoja na kwamba sikuwahi kuwa kiongozi.

Raia Mwema: Katika mijadala yenu chuoni hasa ile mikubwa, hoja gani unakumbuka zilitikisa uongozi au hata nchi?

Lissu: Wakati huo, dunia na nchi ilikuwa ikibadilika, hatukuwa tayari tena kutawaliwa na mfumo wa chama kimoja, eti usipokuwa na kadi ya chama huendi chuo. Nikiwa mwanafunzi, uchangiaji wa gharama za shule ulianza wakati huo.

Nilikaa mwaka mzima nyumbani kabla ya kuingia chuo kikuu kwa sababu mwaka 1989 wanafunzi wa UDSM waligoma, chuo kikafungwa.

Pamoja na kwamba sikuwa sehemu ya huo mgomo wakati huo nilikuwa JKT, lakini madhara ya mgomo yalinigusa kwa kukaa nyumbani mwaka mzima. Nilipojiunga chuo mwaka 1991, tayari vuguvugu lilikuwa kubwa sana. Na upinzani dhidi ya uchangiaji gharama za elimu ulikuwa mkubwa sana.

Raia Mwema: Mliguswa vipi na tukio la kumdhalilisha Rais Mwinyi wakati ule chuoni UDSM?

Lissu: Chuo kilifungwa kutokana na tatizo hilo mwaka 1989. Ni tukio lililotugharimu ambao ndiyo tulitaraji kwenda kuanza masomo. Tulikaa nyumbani mwaka mzima.

Raia Mwema: Katika changamoto za mageuzi chuoni, baadaye ulijiunga na chama gani baada ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa?

Lissu: Kama nilivyosema, nimezaliwa rebel , na hivyo haikuwa ajabu hata kidogo mimi kujiunga na chama cha upinzani ambacho kilivutia wasomi – NCCR-Mageuzi. Ilikuwa ni hatua inayotegemewa.

Nisingeweza kuwa CCM au CHADEMA kwa sababu kilikuwa chama kisichokuwa na msimamo mkali….hawa watu ni waoga, wanaogopa kuweka msimamo mkali. Ni kama chama cha kibepari hivi na mimi kimsimamo nimekuwa Mjamaa wa mrengo wa kushoto kabisa.

Raia Mwema: Uchaguzi wa kwanza baada kuruhusiwa vyama vingi mwaka 1992 ulifanyika 1995. Ulishiriki vipi uchaguzi huo?

Lissu: Ingawa jimboni kwetu (Singida Kusini wakati huo) mwanzo hapakuwa na uchaguzi wa vyama vingi, lakini ilikuwa sehemu ya changamoto kisiasa, hata wabunge waliokuwa wakichaguliwa walidumu kwa muhula mmoja tu.

Sasa ghafla tukawa na demokrasia pana zaidi – vyama vingi, lakini kwenye uchaguzi huo (1995) ikaelekea CCM itapita bila kupingwa. Kwa hiyo nikajitokeza kugombea ubunge jimbo la Singida Kusini.

Lakini wakati naanza mchakato wa kuwa mgombea, nikapata scholarship ya Serikali ya Uingereza kwenda kusoma Master’s (Uzamili). Nikaenda shule kuripoti, nikawaambia narudi nyumbani kujaribu ubunge, nikishindwa nitarudi.

Nikatoka Uingereza kuja kugombea ubunge mwaka 1995, nikiwa na miaka 27. Nikarudi shule baada ya kushindwa. Safari yangu ya kisiasa ilianza kujitokeza kipindi hicho.

Nikamaliza shule yangu mwaka 1997, nikaoa na nikahamia Dar es Salaam (kutoka Arusha alikokuwa akifanya kazi kama mwanasheria ofisi binafsi).

Raia Mwema: Katika harakati zako, tukio gani kubwa unakumbuka lilikutia msukosuko au kuibua katika jamii?

Lissu: Tukio la kwanza kubwa ilikuwa ni mradi wa ufugaji kamba delta ya Rufiji. Mradi wa Mzungu mmoja wa Ireland anaitwa Reginald Nolan. Alipewa na Serikali ya Mkapa hekta 20,000 ili atengeneze mabwawa ya kufuga kamba kwenye delta ya Rufiji katika maeneo ambayo yana vijiji karibu vinane, watu walima na kuishi, kuna msitu ya mikoko pale. Yote ile Reginald Nolan akapewa ili atengeneze mabwawa. Sisi kama watetezi wa mazingira kupitia Chama Cha Wanasheria wa Mazingira – LEAT, tulishikia sana bango mradi wa Rufiji.

Tulifanya kazi kubwa. Niliratibu kampeni ya kimataifa kwa kila njia, ikiwamo mitandao ya kimataifa ya wanaharakati kuupinga mradi huo.

Hatimaye, Benki ya Vitega Uchumi ya Ulaya (European Investment Bank) iliyokuwa itoe mkopo kwa Nolan ambao ungedhaminiwa na Serikali ya Tanzania, wakasema hawatatoa mkopo na kwa hiyo, mradi mzima ukasambaratika.

Niliwahi kushiriki mdahalo kwenye kituo cha televisheni nchini kuhusu mradi huo wa kamba, nikiwa mimi, mmiliki wa mradi na mwandishi wa habari wa siku nyingi, James Mpinga. Kwa mara ya kwanza ndipo nilipoanza kuonekana kwenye televisheni katika kipindi cha Hamza Kasongo Hour, Oktoba 1998.

Tuliwasambaratisha kila mahali. Tukapata nyaraka za Baraza la Mawaziri zilizosema mradi ni wa hovyo, lakini umepitishwa kinyemela.

Raia Mwema: Katika mchakato mzima wa harakati hizo, uliwahi kukumbwa na vitisho vya aina fulani?

Lissu: Vitisho vingi. Unaweza kufika ofisini ukakuta bahasha yenye ujumbe wa vitisho imepenyezwa chini ya mlango.

Baada ya hapo Machi, mwaka 1999, kuna kampuni moja wenye ginnery (kinu cha kuchambua pamba). Ni kampuni ya ki-Swisi. Wakaja ofisini kwetu (LEAT) wakaomba tuwafanyie utafiti juu ya madhara wanayoweza kupata kutokana na mgodi uliokuwa ukijengwa Geita. Walitaka kubaini kama shughuli za mgodi zitaathiri shughuli zao za kusafisha pamba.

Kwa hiyo, nikapewa hiyo kazi. Nikasafiri kwenda Geita, asubuhi yake (baada ya safari) wenyeji wangu wakanipeleka wanakojenga mgodi. Nikakuta vijiji vinabomolewa kwa magreda na mbele yake wametangulia askari wenye bunduki. Kijiji kile kilipitiwa na barabara, sasa upande wa pili wa barabara yuko Mkuu wa Wilaya, Halima Mamuya, OCD na maofisa wengi.

Mkuu wa Wilaya ya Geita ameshika kipaza sauti, anawaambia wanakijiji kwamba niliwaambia mlipwe fedha (fidia) mmekataa, sasa mtajua mtakwenda wapi.

Pale kwenye shimo kubwa lenye kina cha Kilomita kama tano wanakochimba dhahabu ndipo kilipokuwapo kijiji cha Mtakuja.

Nilishuhudia mgodi wa kwanza ukianzishwa kwa kuharibu kijiji ambako kulikuwa na makazi pamoja na mazao…mahindi yanayoelekea kukomaa, na wakati huo nchi ilikuwa imekumbwa njaa kwa sababu mwaka uliopita kulikuwa na mvua za el-nino.

Hali ile ilinikumbusha wakati wa operesheni vijiji ambako nyumba yetu na za wanavijiji pamoja na mashamba viliharibiwa. Nilishangaa serikali kuharibu mashamba ya chakula. Nikaandika ripoti yangu, nikawapelekea wenye kinu cha pamba na kupendekeza kwamba tunahitaji ginnery kukaa na wananchi kijiji ili kupambana na uhalifu huo.

Nikawaambia nyie mna hela, wanakijiji watawapa ile human element, idadi ya watu ambao wanaathiriwa. Ukizungumza athari, ukaonyesha watu wanabomolewa ina value kubwa sana katika mapambano. Kwa hiyo, wanakijiji mkiwaacha wakasambaratishwa, hata nyinyi hamtabaki.

Wakaniambia sisi ni wawekezaji, nikawaambia wenzangu katika LEAT kwamba ugomvi mkubwa katika miaka inayokuja ni ugomvi wa madini.

Kwa hiyo, kutoka Geita kwenda Bulyanhulu ni mwendo wa dakika 45. Katika kuchunguza makampuni ya madini yanafanya nini kwa wananchi, kitu cha kwanza utakachokutana nacho ni Bulyanhulu. Ndio eneo ambalo kulitokea maafa makubwa zaidi.

Mwaka 1999 nikapata nafasi kwenda Marekani kuwa mtafiti katika taasisi ya World Resource Institute kwa miaka mitatu. Nikawaambia World Resorce Institute nitafanya kwa sharti moja; kwamba kazi niliyoanza kuifanya katika LEAT ya madini niendelee nayo.

Nikaondoka kwenda Marekani Septemba 1999 na kwa miaka mitatu yote mnayojajua juu ya Bulyanhulu yalipatikana katika kipindi hicho. Karibu kila mwezi nilirudi Tanzania kuendelea kutafiti suala hilo la Bulyanhulu.

Tulipata ushahidi wa picha za video na nyingine unaothibitisha kwamba watu wengi waliuawa. Hizo picha ni za jeshi la polisi na kampuni yenyewe.

Tulikuwa kila tunapopata video hizo tunazitangaza hadharani. Mwaka 2001 tulifanya press conference kubwa Maelezo kuthibitisha kwamba tunao ushahidi wa picha za video zinazothibitisha mauaji hayo kutokea.

Nilikuwa mimi na Rugemeleza Nshala. Baada ya mkutano huo, mimi nikaondoka kurudi Marekani. Lakini huko nyuma, baada ya tarehe 23, Polisi wakavamia ofisi zetu za LEAT na nyumbani kwangu wakitafuta huo ushahidi. Na wakati huo Jeshi la Polisi likasema huyu mtu ametoroka, anatafutwa na Interpol, kwa hiyo akamatwe. Wenzangu baadaye walikamatwa.

Niliporudi Marekani walinikamata na kuniweka kituo kikuu cha polisi Dar es Salaam. Nilipokuwa kituoni humo nilifanya ujanja nikaingia na simu na nikafanya mahojiano na magazeti ya Canada na Marekani usiku kucha. Kesho yake ilikuwa sikukuu ya Krismasi. Nikafuatwa na polisi, nikaambiwa napelekwa mahakamani.

Raia Mwema: Tueleze kujiunga kwako na CHADEMA, kulikuwaje?

Lissu: Kujiunga na CHADEMA mwaka 2004 sababu ilikuwa Tarime na suala la kampuni za madini. Harakati za madini Tarime nilizianza mwaka 2003.

Wakati ule mtu aliyenipokea Tarime ni marehemu Chacha Wangwe. Nilimkuta ana kesi 10 za jinai wakati huo akiwa diwani wa CHADEMA. Akaniambia; wanataka kunifunga hawa…nikamwambia hawawezi, wanakutisha tu.

Alisumbuliwa sana, na Tarime ilikuwa inatisha kama ilivyo leo. Mbowe akanipigia simu akaniomba nisaidie kisheria kumtetea Wangwe, chama kitagharimia usafiri. Kwa hiyo, nikaanza kazi ya kuwapa huduma ya kisheria na katika kipindi cha miezi minne nimetoa gerezani watu 366 waliokuwa wanatumikia vifungo.

Siku moja Mbowe akaniambia nitafute watu wengine wanataaluma ili wajiunge na CHADEMA. Nikamuuliza kwa nini unafikiria mimi ni mwanachama wa CHADEMA? Alikuwa miaka yote anafikiria mimi ni mwenzao, kumbe mimi ni NCCR-Mageuzi.

Akauliza kwa nini si mwanachama wa CHADEMA? Nikamwambia hujawahi kunipa sababu za kwa nini niwe mwanachama wa CHADEMA. Kama unataka niwe, niambie tu.

Kwa hiyo, hivyo ndivyo nilivyoingia CHADEMA. Kwa maisha yangu kwa historia yangu na msimamo wangu, mimi ni mwanahakarati, na pengine Rais Kikwete hakosei sana anaposema vyama vingine ni vya wanaharakati.

Raia Mwema: Unazungumziaje nafasi yenu Bungeni, hasa ikizingatiwa suala la idadi na ubora wenu?

Lissu: Bunge kama unaelewa sawawa linakupa nafasi ya kuibua mijadala. Siku zote sasa nimeelewa kwamba Bunge si mahali pazuri pa kutatulia migogoro, lakini ni mahali pazuri pa kuzungumzia na ku-mobilise nguvu ya umma. Hayo matatizo ya kisiasa au kikatiba, hayatatuliwi bungeni isipokuwa yanazungumzwa.

Suala la wingi, kwa maana ya idadi au ubora wa wabunge, bila kujali idadi lina umuhimu wake.

Kwa mfano; inapofika wakati wa kupitisha sheria au bajeti, hatuwezi ingawa tunao wabunge bora zaidi na wajenga hoja wazuri. Kwa hiyo, hapo ‘ujinga wa wengi’ ndipo unaposhinda. Kama unaitumia nafasi hiyo bungeni vizuri, kama ambavyo tumekuwa tunafanya, hiyo itakuwa inatusaidia kujenga nguvu kubwa nje ya bunge. Inategemea unatumiaje hiyo fursa ya Bunge.

Raia Mwema: Ulikuwa Tarime hivi karibuni. Wako wanaohoji ulikwenda kutafuta nini wakati ni eneo lenye mbunge wake.

Lissu: Labda niwajibu hao wajinga wasiojua nilikuwa nafanya nini Tarime. Kwa historia yangu na Tarime, ilikuwa ni wazi ningeenda Tarime baada ya kutokea masuala haya (mauaji) na ndugu zao kukataa kuwazika hadi uchunguzi. Ningekuwa sio mbunge pia ningekwenda Tarime. Nina historia ndefu ya mapambano ya kudai haki Tarime.

Yaliyotokea yanafamika – tulikamatwa na kuwekwa kwenye selo Tarime, tumeshtakiwa. Ni hali halisi ya Tarime. Ni eneo la vita, ni janga la kitaifa kama nilivyoeleza baada ya kuachiwa kutoka gerezani.

Tarime ya leo ni mbaya kuliko Tarime ya 2003 nilipokwenda kwa mara ya kwanza ambapo mamia ya watu wa Nyamongo walikuwa gerezani. Tarime ya leo ni ya mauaji yanayofanywa na jeshi la polisi. tangu tuwashinde (CCM) uchaguzi. Mauaji ya kwanza Tarime yalifanyika Julai 20, 2005. Hadi kuua hawa wa juzi watano, sasa wamefikia watu 28 waliouawa kwa kupigwa risasi mchana kweupe.

Raia Mwema: Lakini kiini cha tatizo nini? Je, ni mwekezaji au jeshi la polisi?

Lissu: Tatizo ni mwekezaji, polisi na Serikali ya Tanzania. Kusingekuwapo mwekezaji, watu wasingeuawa.

Raia Mwema: Lakini kama tatizo ni pamoja na polisi au serikali kuna migodi mingine mauaji hayaendelei kama Tarime?

Lissu: Katika sekta ya madini unakuja na umwagaji damu. Bulyanhulu, Tarime, Geita, Nzega hakuna mahali ambapo wawekezaji wameweka mgodi wa dhahabu wa kisasa bila kuangamiza uchumi wa wenyeji, bila kuwaondoa kwa mabavu ya kijeshi.

Raia Mwema: Kifanyike nini?

Lissu: Ni mambo mawili ya kuchagua. Kwanza, je, tunataka huyo anayeitwa mwekezaji achume mali na inunuliwe kwa damu za Watanzania? Inunuliwe kwa Watanzania kukosa haki na kwa uchumi wa Watanzania kusambaratishwa? Au tuamue kwamba maisha ya Watanzania ni bora zaidi kuliko dhahabu.

Kwa maoni yangu, haiwezi bei ya dhahabu ikawa sawa na maisha ya mtu mmoja. Watanzania wameshauwa kwa risasi na kwa kunywa maji ya sumu yanayotokana na mwekezaji. Tarime imejaa vijana wanaoshitakiwa kwa kesi za ugomvi na mgodi, lakini sasa hivi wanashtakiwa kwa kesi za mauaji au uhalifu wa kutumia silaha!

Wakati nakwenda Tarime kwa mara ya kwanza, kesi zilizokuwa zikifunga watu zilikuwa uchochezi na kuvamia eneo la mgodi, lakini leo kesi za Tarime ni mauaji. Hata ukikamatwa kwa kurushwa jiwe ambalo halijampiga mtu yeyote, utashtakiwa kwa mauaji au uhalifu wa kutumia silaha!

Na unashtakiwa kwa hayo makosa mawili kwa sababu huwezi kupewa dhamana. Kwa hiyo, polisi wasipofanya upelelezi utafia gerezani.

Nilikamatwa Tarime nikakaa gerezani. Naweza kuthibitisha kuwa Tarime kuna watu zaidi ya 400 wanaokabiliwa na kesi za mauaji.

Sasa njoo huku ambako hakuna mgodi, leo biashara ya teksi Tarime mjini ni biashara ya mapolisi kwa sababu wafanyabiashara wa kawaida pale mjiini aidha wako gerezani wakikabiliwa kwa mauji au wengine wameuawa.

Selo niliyofungwa mimi Tarime inatumika kwa kitu kimoja tu, nimeambiwa kuna watu wengi sana wameuawa, wameumizwa sana. Kuna mtu mmoja amepigwa risasi tano miguuni kwenye kituo cha polisi na mkononi amepigwa risasi mbili, na mkono umekatwa.

Kuna watoto. Kuna mtoto wa miaka 12 selo niliyolala mimi. Bunge hili limepitisha sheria mwaka juzi, sheria ya mtoto inayosema mtoto wa miaka 18 hawezi kupata adhabu ya kifungo.

Huyu mtoto ana miaka 12 anakaa kwenye gereza na wafungwa watu wazima waliopatikana na hatia. Napeleka hoja binafsi bungeni kuomba iundwe kamati teule ya Bunge kuchunguza suala hili.
______________
Tujikumbushe tu! .
Tuzidi kumuombea Lisu..

1. Je Wajua Tundu Lissu Aliwatoa Gerezani BURE Wananchi 466 Wa Tarime Waliofungwa Kwa Kupinga Mwekezaji Asiwanyanganye Ardhi Yao?

2. Je Wajua Tundu Lissu Alishawai Kupigwa Marufuku Asikanyange Nyamongo Kwasababu Ya Harakati Zake Za Kuwatetea Wananchi Dhidi Ya Wawekezaji?

3. Je Wajua Tundu Lissu Alipambana Na Kaka Yake Alute Lissu Mahakamani Kwenye Kesi Ya Kupinga Ubunge Wa Lema, Alute Akiitetea CCM Na TL CHADEMA?

4. Je Wajua Tundu Lissu Akiwa JKT Itende Alidhaniwa Kuwa "Usalama Wa Taifa" Kutokana Na Tabia Yake Ya KUHOJI Bila Woga?

5. Je Wajua Tundu Lissu Alipambana Na Serikali Ya Mkapa ISIUZE Rufiji Delta Kwa Mwekezaji Nolan, Hadi Bank Ya EIB Ikagoma Kutoa Mkopo Kwa Nolan?

6. Je Wajua Mwaka 2004 Freeman Mbowe Alimuomba Tundu Lissu Ajiunge CHADEMA Baada Ya Kumtetea Chacha Wangwe Kwenye Kesi 10 Za Jinai?

7. Je Wajua Tundu Lissu Alianza Kushtakiwa Kwa "Uchochezi" Mwaka 2001 Na Mpaka Leo Hajawai Kukutwa Na Hatia?

8. Je Wajua Kwenye Kampeni 2010 Kikwete Aliwai Kusema Ni Heri Dr.Slaa Awe Rais Kuliko Tundu Lissu Awe Mbunge?

9. Je Wajua 70% Ya Kesi Anazozisimamia Tundu Lissu Halipwi Chochote Na Watu Anaowatetea, Yeye Hufurahi Akiona Mtu Haonewi Wala Kunyanyaswa?

10. Je Wajua Tundu Lissu Hutumia Mshahara Wake Wa Mbunge Kusafiri Maeneo Mbalimbali Nchini Kuwatetea Walalahoi BURE Mahakamani

Mungu amzidishie Rehema na uponyaji kwa muujiza Mkuu!


Hatimae tar 7 mwezi wa 9 ,
2017
Anamiminiwa risasi akiwa kwake Dodoma.
Yupo Nairobi kwa matibabu

Mungu amponye
Amen.
 
inatia hasira sana aisee huko nyamongo speaker ndugai aliongoza kamati iliyodai kwamba hakuna sumu iliyotirirshwa mtoni huku lissu akitetea wananchi bure leo huyo speaker anajifanya mzalendo na malipo ya lissu ni kupigwa risasi.
 
Aliandika TUNDU LISSU KATIKA MTANDAO WA TANZANIA 2015 AND BEYOND FORUM
26/05/2017

Na mimi ni Mtanzania pia.
Tofauti kati yangu mimi na wewe na Magufuli ni hii: Mimi nimepigania nchi yangu katika masuala haya tangu mwaka '99.

Wakati huo tulikuwa na mgodi mmoja tu wa dhahabu, Resolute Golden Pride Nzega. Bulyanhulu ilikuwa haijajengwa. Geita ndio kwanza walikuwa wanafukuza wanakijiji wa Mtakuja.

Nadhani nilikuwa wa kwanza katika nchi hii kupiga yowe kwamba tutaibiwa sana kwenye sekta ya madini.

Wewe sijui ulikuwa wapi wakati huo. Najua Magufuli alikuwa wapi: upande wa MaCCM na wawekezaji hawa.
Nimepigana na wawekezaji hawa mahakamani, kwenye medani ya kisiasa ndani na nje ya nchi hii kwa zaidi ya miaka 15. Nimetetea wananchi completely free of charge Bulyanhulu, Tarime, Nzega, Geita, n.k.

Sijui wewe ulikuwa wapi lakini najua Magufuli alikuwa upande wa nani: wa MaCCM na wanyonyaji hawa.

Soma Rai ya tarehe 17 Julai, 2001, uone tulimwambia nini Mkapa siku anaenda kuzindua Mgodi wa Bulyanhulu.

Sijui ulikuwa wapi lakini najua Magufuli alikuwa wapi: alikuwa anatetea tumbo lake na matumbo ya wanyonyaji hawa.

Nilikamatwa na kushtakiwa kwa uchochezi kwa sababu ya Bulyanhulu. Hiyo ilikuwa December 2002. Nilikaa na kesi hiyo mahakamani Kisutu kwa miaka sita.

Sijui ulikuwa wapi ila najua Magufuli alikuwa wapi: upande wa watesi wa wananchi na wanyonyaji wa rasilmali zetu.

Leo Magufuli anajifanya mzalendo na anahoji uzalendo wa yeyote anayepingana nae.

Ni muongo. Anatafuta umaarufu wa kisiasa kwa wasiojua na wasiokumbuka. Ataupata. Kwa siku chache tu. Mark my words: ataumbuka na mtaumbuka.

Mimi ninampinga hadharani. Sio mnafiki, na sijahongwa. Ninampinga kwa sababu atatusababishia matatizo makubwa zaidi kuliko tuliyonayo sasa.

Huo mchanga atauachia upelekwe ambako umepelekwa kwa miaka 16 iliyopita. Kama sheria ndiyo hiyo na mikataba ndiyo hiyo hana pakwenda.

Tatizo ninaloliona ni kwamba by the time anawarudishia mchanga wao, Tanzania itakuwa imekuwa a basket case kama Zimbabwe.

Na tutakuwa tumelipishwa mapesa mengi kama fidia na arbitral tribunals za kimataifa kwa kuvunja mikataba na wawekezaji hawa.

Kama kuna anayefikiri uzalendo ni kufumbia macho masuala haya basi huyo na amuunge mkono Magufuli kwenye upofu wake wa kujitakia.

Ripoti ya Prof. Mruma haitamaliza hata nusu saa under serious scrutiny. Zaidi ya majina ya maprofesa walioiandaa, ripoti hii haina credibility yoyote. Ni kazi ya kisiasa iliyopakwa rangi ya usomi.

Kama umefuatilia taarifa za kitaalamu za Bulyanhulu hata kabla ya Barrick Gold kuingia mwaka '99 utajua ninasema nini.

Sutton Resources, Outukumpu Oy na hata STAMICO walishafanya utafiti mkubwa juu ya utajiri wa Bulyanhulu. Taarifa zipo na zimekuwepo kwa hata mbumbumbu wa jiolojia ya madini kama mimi.

Hiki alichoambiwa Magufuli ni rubbish, hata kama ni ya kiprofesa. Rubbish. Hatuibiwi kwenye mchanga, that's the rubbish fed on the unlettered.

Tunaibiwa kwenye sheria. Kama hamuoni hilo, then God have mercy on us!

[HASHTAG]#PrayForTunduLissu[/HASHTAG]
[HASHTAG]#PrayForTanzania[/HASHTAG]
 
Bahati mbaya watanzania wengi hawayajui haya na hawana namna ya kufikiwa na taarifa hizi kuhusu kazi ya kutukuka ikiyifanywa na shujaa wetu ndg Lisu, yatasikika ya magufuki anayepata airtime ya kutosha katika vyombo vyote vya habari. Mwenyenzi Mungu mponye shujaa Lisu mapema na waadhibu hapa hapa duniani na mwendelezi wake kesho ahera wote walidhamiria kuitoa roho ya Lisu.
 
Justin Mwanshinga; ubarikiwe sana kwa bandiko hili. Umniariki sana.

TAML ndiye anayehitaji maombi ili Mungu amponye, arudi aendeleze harakati za utetezi wa ukombozi dhidi ya wawekezaji majizi na wote wanaowafadhili!
 
Ngoja vijana waje wamwage povu APA Kutoka Chuo kikuu cha utotoni mpaka kumwaga damu September 7
 
Sikumbuki kwa miaka saba ya shule ya msingi, kama kuna siku nimewahi zile namba. Siku zote nilikuwa mchelewaji na nimechapwa kweli.

Dilunga: Ni ukaidi wa makusudi?

Lissu: Siwezi kusema ni makusudi, lakini tatizo ni kuamka alfajiri saa 11 ili saa 12 niwe shuleni. Kwa hilo nilikuwa rebel (muasi). Pia sikumbuki mahali ambako sikuwahi kubishana na walimu iwe primary school, secondary school, iwe chuo kikuu, siku zote imekuwa hivyo.
.

Ni vigumu sana kumbadilisha mtu ambaye harakati zake ameanzia tangu utotoni, unachopaswa kubadilika wewe.

Long live Tundu Lissu.
 
Back
Top Bottom