Uchaguzi huu umetufundisha mengi sana:
i) Wananchi wakiamua hakuna linaloshindikana. Huko Tarime wananchi walilishwa kila aina ya sumu, ikiwemo ghiliba na pesa nyingi lakini wameikataa CCM. Tumeshuhudia akina Makamba wakiwapa wananchi malaki na mamilioni ya shilingi. Lakini walichofanya watani zangu wa Tarime ni kukusanya hela zote walizopewa na akina Makamba na kwenda kununua pombe zote wakanywa usiku kucha. Akina Makamba kuona hivyo walikasirika mno na ndio ukawa mwanzo wa kuagiza mapolisi lundo kama tulivyoona. Walichotufundisha wana Tarime hapa ni kwamba hela ambazo CCM wanazimwaga wakati wa uchaguzi ni za kwetu ambazo wametuibia na kutunyang'anya, kwa hivyo tunaweza kuzipokea na bado hiyo isibadilishe nia yetu. Na pengine mtindo waliotumia wananchi wa Tarime ndio njia sahihi ya kukabiliana na uharamia wa CCM wa kutumia pesa katika uchaguzi.
ii) Tumefika turning point, kwa maana kwamba katika kila sehemu kuna watu wenye kutaka kuona haki inawepo. Tarime kulikuwa na majaribio mengi ya kutaka kubadilisha matokeo, lakini kuna baadhi ya watendaji ndani ya Halmashauri ya Tarime ambao walikuwa wanafanya kazi kwa niaba ya Tume walikataa kata, wakisema kuwa haki lazima itendeke. Hii ina maana kuwa kuna watendaji katika serikali hii ya ovyo ya CCM ambao kwa kweli wapo tayari kusimamia haki hata kama kufanya hivyo italeta matatizo kwenye vibarua vyao. Ni hatua ya namna hii iliyowezesha vyama vya upinzania huko Zambia, Malawi, na hata Kenya. Bila kuwa na watu wenye uchu wa haki ndani ya vyombo vya dola, itakuwa ngumu kuishinda CCM. Kwa sababu hiyo nachukua nafasi hii kuwashukuru sana watendaji mbalimbali wa Tume ya Uchaguzi huko Tarime waliohakikisha kuwa wanashinda majaribu na mashinikizo ya akina Makamba na kuhakikisha wana mtangaza mshindi kama walivyoamua wananchi.
iii) Tunawashukuru wana JF kwa changamoto na nasaha zenu, ambazo kwa kweli zimekuwa zinatusaidia sana kujifunza. Matokeo ya Tarime yametuchochea kufanya kazi ya siasa, na katika siku chache zijazo mtashuhudia viongozi wa chadema wakisambaa mikoani kwa ajili ya kazi ya kukisimika chama katika nyoyo za watanzania.
iv) Sasa hakuna shaka yeyote kuwa wenzetu NCCR wanafanya kazi ya kuisaidia CCM katika juhudi zao za kufifisha nguvu za upinzani. Mwanzo mimi binafsi nilikuwa mgumu kuamini kwamba NCCR wanafanya makusudi. Lakini sasa kwa matendo yao ya Tarime, na baada ya mimi mwenyewe kuongea na baadhi ya viongozi waandamizi wa chama hiki, nimekubali kabisa kwamba chama hiki hakipo kwa ajili ya kupambana na CCM. Hawa ni wachafuzi wanaofanya kazi maalumu ya kuua vuguvugu la mabadiliko katika nchi yetu. Kwa sababu hii nitakuwa mtu wa pili ndani (yupo aliyekwishanitangulia) ya chadema kupinga kwa nguvu zangu zote ushirikiano na NCCR. Kama kuna haja ya ushirikiano, basi ushirikiano huo uwe baina ya CHADEMA na CUF. Kwa maoni yangu hivi ndivyo vyama halisi vya upinzani Tanzania, ambayo vina strengths na weaknesses zake, kiasi kwamba kuungana kwao kutasaidia kupunguza weaknesses na kujiimarisha zaidi.
v) Uchaguzi huu umetukumbusha maadili halisi ya kitanzania, kwamba si utanzania kujaribu kujipatia umaarufu kupitia kwenye msiba. Sisi watanzania hutumia msiba kumaliza mitafaruku, sio kuikuuza. Wenzetu CCM, nafikiri kwa kufilisika kimawazo na kimikakati, waliamua kutumia msiba wa Wangwe kama njia ya kuimaliza CHADEMA Tarime. Wananchi, kwa kutumia common sense, sio madigrii, wamekataa ghiliba hizi. Imekuwa ni aibu kubwa. Wakajaribu kujenga propaganda kwamba Mbowe akienda Tarime atapigwa-lakini wamepigwa wao na Mbowe kapokelewa huko Tarime kuliko Malkia wa Uingereza alivyopokelewa wakati anapewa taji. Ni aibu kubwa.
Vi) Mwisho, niseme kwamba uchaguzi huu unaashiria mwisho wa siasa za ujanjaujanja. Siasa za akina Tambwe, Makamba na Akwilombe hazitawasaidia huko tuendako. Huko tuendako kinachotakiwa ni umakini, ukweli na uwezo. Blabla, longolongo na uongo unaoenezwa na akina Tambwe hauna tija. Anayeendelea kuwadanganya CCM kwamba umahiri wa kusema uongo ndio ushujaa katika siasa anawadanganya, na wajiandae kuumbuka zaidi huko tuendako. Kwa kuwasaidia, katika kujipanga upya, wawafukuze au wawape kazi nyingine akina Tambwe, Akwilombe na Makamba.