RA aliingia kimya kimya Busanda na kumwanga fedha kufanikisha ushindi wa Bibie ambaye wengi wanasema ilipata ushindi wa kura za maoni kwa kupitia mngongo wa Katibu mkuu na kuwashinda Bwana Donald Max na yule kibaraka wa Dialo huku wengi wakitegemea Max ashinde akambulia nafasi ya pili.
RA ikabidi atumwe kwenda kumkatia Max ambaye tayari alishaweka makundi hivyo kuhatarisha ushindi wa CCM kama kipande hiki kinavyothibitisha
"Kutokana na makubaliano hayo CCM kiliagizwa kusaka fedha za kumrudishia Max ambazo zililetwa na mbunge mmoja wa Kanda ya Magharibi, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, ambaye imeelezwa aliingia Geita kimya kimya na kufanya mazungumzo naye."
Hata hivyo RA alikuwa analalamika kuwa kuna baadhi ya viongozi wamemtenga sijajua kwanini (papa)?
news baadhi ndio hizo
Hivi RA ndio Mbunge pekee wa kanda ya magharibi na Mjumbe wa halmashauri kuu au ndio unataka kumuingiza mkenge??? Hebu tuweke wazi mkuu.
Hicho kipande ni ulichokikata ktk mwananchi; full news yake ni hii hapa chini : -
JK Aipa Pumzi CCM Busanda Amrejesha Aliyesababisha Mpasuko
*
Helkopta ya Chadema kutua wiki hii
Frederick Katulanda, Busanda
ZIKIWA zimebakia siku saba kufanyika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Busanda Chama cha Mapinduzi (CCM) kimelamba dume baada ya kufanikiwa kumshawishi kada wake aliyeshindwa kura za maoni, Donard Max ambaye atapanda jukwaani kuanzia leo, ili kusaidia kuokoa jahazi.
Kukubali kupanda jukwaani kwa Max ambaye anaanzia kampeni zake katika Kata ya Nyarugusu, kunaelezwa kunatokana na agizo la Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete ambaye baada ya kuambiwa kuwa Max amegoma kusaidia kampeni, alimpigia simu na kumuomba kubadili msimamo wake kwa faida ya chama.
Ni kweli Max leo ataanza rasmi kumnadi mgombea, lakini jambo hili ni siri kubwa, amepangiwa kata zenye hali mbaya ambako akiwa na timu yake atalazimika kupenya huko na kufanya vikao vya faragha na kambi zake, kilieleza chanzo chetu na kudokeza kuwa amekubali baada ya juhudi za mwenyekiti wa chama.
Hatua hiyo inaelezwa na wachambuzi wa hali ya kisiasa jimboni humo kuwa ni muhimu kwa chama hicho ili kiweze kujinasua, kwa vile mgawanyiko unaokikabili kwa kiwango kikubwa ulisababishwa na kumeguka kwa kambi ya Max aliyeibuka mshindi wa pili katika kura hizo, nyuma ya mgombea Lolensia Bukwimba.
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Mkuu wa kitengo cha Propaganda, Tambwe Hiza zimeeleza kuwa baada ya kubaini kuwa chama kipo katika hali mbaya, CCM ililazimika kumuita Max ili aweze kurejesha uhai wa chama hicho, kilichokuwa kinakabiliwa na misukosuko ya viongozi wake kuzomewa na watu wachache kujitokeza kwenye kampeni zake.
Awali, ilielezwa kuwa Max amegoma kurudi Busanda na kutoa sharti la kuondolewa kwa hasimu wake, Anthony Diallo ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, jambo ambalo lilifanyika. Pia Max alifanya mazungumzo na makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Samwel Malecela na makada wengine bila mafanikio.
Diallo anadaiwa kumsaidia Sostenes Kulwa aliyeshika nafasi ya tatu kwa nia ya kumuengua Max, jambo ambalo liligawa kura zake na kuambulia nafasi ya pili.
Taarifa nyingine za ndani zilisema kukubali kwa Max kupanda jukwaani, kunatokana na makubaliano ya faragha baina yake na Malecela kwa niaba ya Kikwete ambaye aliagiza arejeshewe gharama zake za kampeni katika mchakato wa kura za maoni.
Kutokana na makubaliano hayo CCM kiliagizwa kusaka fedha za kumrudishia Max ambazo zililetwa na mbunge mmoja wa Kanda ya Magharibi, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, ambaye imeelezwa aliingia Geita kimya kimya na kufanya mazungumzo naye.
Hata hivyo, Max alipozungumza na Mwananchi Jumapili jana, alisema ameamua kusaidia kampeni kama mwanachama na siyo kwa kuombwa na vigogo wa chama hicho.
Kauli inayofafana na hiyo pia ilitolewa na Hiza ambaye alisema kwamba, Max ni sawa na wanachama wengine wa CCM wa wilaya ya Geita ambao wamekuwa na jukumu moja la kumnadi mgombea wa chama hicho.
Huyu ni mwanachama sawa na wengine, hatusemi anapanda jukwaani kwa sababu zenu ninyi waandishi, anapanda sawa na viongozi wengine wote wa chama wilayani, hakufanya hivyo tangu awali kwa sababu hakuwapo Geita, sasa amekuja, atapanda jukwaani, alisema Hiza.
Kutokana na makubaliano hayo baina ya CCM na Max chanzo chetu kimedokeza kuwa tofauti kati ya kambi yake na Diallo imemalizika na hivyo mjumbe huyo wa NEC, kurejea Geita ambako tangu juzi ameonekana mitaani akiendelea kusaidia kampeni.
Kwa upande mwingine, CCM imepunguza idadi kubwa ya mikutano yake ya kampeni ya kumnadi mgombea wake katika miji na badala yake imeimarisha mikutano ya vijijini ambapo kwa siku imekuwa ikifanya mikutano mitatu hadi minne kila kata.
Hatua hii imekuja baada ya kukumbana na hali ngumu katika mikutano ya majukwaani ambayo imekuwa ikiishia kuzomewa kwa viongozi wake, hatua ambayo imeelezwa kuwa imekiathiri chama hicho kutokana na watu wengi kubadilika na kuisapoti kambi ya wapinzani wao na hasa Chadema.
Katika mikutano hiyo ya nje ya mji, viongozi na wabunge wa CCM wamekuwa wakizunguka kila kijiji kuzungumza na wananchi mbalimbali kwa makundi maalumu ambayo ni makundi ya wazee, vijana na viongozi wa dini.
Hali yetu ni ngumu lakini siyo kama mnavyodhani, mkakati wetu wa vijijini ni mzito sana kutokana na kuonyesha mafanikio, alieleza mmoja wa viongozi wa wilaya wa CCM ambaye amepangiwa kata ya Nyarugusu.
Alisema viongozi hao wamekuwa wakizungumza na wazee kwa kuwaomba radhi kutokana na kushindwa kutimiza ahadi walizoahidiwa wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2005 na kuwasii watoe nafasi kwa CCM kwa vile Rais Kikwete ameahidi kuyapa msukumo matatizo ya Busanda mara baada ya uchaguzi.
Wakati hayo yakitendeka, Chadema wameanzisha mkakati maalumu kwa ajili ya kusimamia na kulinda kura katika vituo ili kudhibiti upotevu wa kura zao.
Habari za ndani ya Chadema ambazo zimethibitishwa na Afisa Mwandamizi na Kurugenzi ya Sera na Utafiti, Mwita Mwikwabe Waitara, zimesema kuwa kamati maalumu imeundwa kwa ajili ya kuratibu mbinu za usimamizi wa kura katika vituo jimboni Busanda ili kuhakikisha mgombea wao, Finias Magesa anaibuka mshindi.
Katika kufanikisha mkakati huo, kamati hiyo imetoa namba za viongozi ili wananchi waweze kutoa taarifa wakati wowote pale wanapoona masanduku yakiwa nje ya vituo au katika hali isiyo kawaida.
Akizungumza juzi katika mkutano wa hadhara wa chama hicho, Waitara alisema wanatambua mikakati ya CCM, kwani baada ya kuzidiwa katika jukwaa wametulia wakielekeza mbinu zao katika wizi wa kura, jambo ambalo alisema watalisimamia kikamilifu kuhakikisha hawapati mwanya wa kufanikisha azma yao hiyo.
Sambamba na mkakati huo Chadema wamepanga kufanya kampeni za mwisho kwa kishindo huku wakitumia helkopta atakayozunguka nayo mwenyekiti wa chama, Freeman Mbowe ili kufikia vituo vingi kwa kipindi kifupi.
Vyama vingine vinavyoshiriki uchaguzi huo vimeendelea na mikakati yake ya kutumia majukwaa. CUF wameongeza nguvu kwa kumuita Mwenyekiti wake, Profose Ibrahimu Lipumba ambaye ataingia leo kumnadi mgombea wao, Oscar Ndalawah.
Kampeni za UDP zimeendelea kudorora kutokana na kutumia mbinu ya kutoa matangazo kwa njia ya vipaza sauti vilivyowekwa katika gari ambalo limekuwa likipita mara kadhaa katika mitaa kuwahimiza wananchi kumchagua mgombea wake, Beatrice Lubambe.
Katika hatua nyingine, Salma Said anaripoti kutoka Zanzibar kuwa, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa (UVCCM), Hamad Yussuf Masauni amewakemea wapinzani wanaowatisha na kuwazomea viongozi wa chama hicho katika kampeni zinazoendelea katika uchaguzi mdogo wa Busanda.
Akihutubia wanachama wa CCM katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Magogoni Visiwani Zanzibar, Masauni alisema Chadema kinaendesha kampeni chafu huko Busanda jambo ambalo ni kinyume na demokrasia ya mfumo wa vyama vingi.
Tumevumilia vya kutosha, sasa imetosha na sasa tunataka kuona mambo haya yanakomeshwa haraka
, alisisitiza Mwenyekiti huyo.
Masauni aliyasema hayo wakati Chadema wakimlalamikia mkuu wa polisi wilaya ya Geita kwa kupokea amri kutoka kwa CCM kuwakamata wanachama wake bila sababu na wengine kufikishwa mahakamani, huku akiwaachia huru makada wa CCM waliokamatwa wakinunua shahada za kupigia kura.