Vurugu zazidi kurindima Kiteto
2008-02-22 09:57:20
Na Simon Mhina, Kiteto
Maofisa wa Jeshi la polisi na Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) jana walilazimika kumshusha jukwaani Mbunge wa Mbinga na Mkurugenzi wa kundi la sanaa la TOT, kapteni John Komba, baada ya kuibuka vurugu kubwa za kampeni za uchaguzi mdogo katika kata ya Kijungu wilayani hapa.
Vurugu hizo ziliibuka baada ya ratiba ya Tume ya Uchaguzi kuonyesha waliopaswa kufanya mkutano wa kampeni ni CHADEMA badala ya CCM ambapo Kapteni Komba alionekana kulishambulia jukwaa na bendi yake ya TOT.
Jeshi la polisi limelaumiwa kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka kudhibiti hali hiyo licha ya viongozi wa CHADEMA kuwasilisha malalamiko hayo kwa jeshi hilo.
Katika tukio hilo, Mpiga picha wa Tanzania Daima, Bw. Joseph Zablon alinusurika kipigo baada ya kutaka kumpiga picha kiongozi wa TOT, Kapteni Komba akishushwa jukwaani.
Mara baada ya kuwasili kikosi cha FFU katika magari mawili, PT 1461, PT 1433 na gari dogo la polisi aina ya Landrover PT 1529, waliokuwa wanaongozwa na Mkuu wa Kikosi cha upelelezi mkoa wa Manyara akiwa pamoja na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (ASP), Ernest Sakawa, walitumia zaidi ya saa moja kumshawishi Kapteni Komba kusitisha kupiga mziki, lakini aligoma.
Hata hivyo, mara baada ya kuwasili Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Bw. John Henjewele na kufanya mazungumzo na maofisa hao wa polisi, walifanikiwa kumshawishi Komba kushuka jukwaani.
``Tunakuomba uzime mziki Mheshimiwa Komba na kushuka chini,`` alisikika mmoja wa maofisa wa polisi akimweleza Komba ambaye baada ya kuimba nyimbo za CCM kwa muda ndipo alishuka.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari kijiji hapo, Mkuu wa mkoa wa Manyara, Bw. Henry Shekifu alisema amejionea tatizo hilo na kuahidi kuwa serikali itachukuwa hatua kwa kundi ambalo limevamia mkutano.
``Mimi nimeona lakini sio jukumu langu kuzuia mkutano. Kuna vyombo husika vyenye majukumu hayo nadhani wamepewa taarifa watakuja,`` alisema.
Awali, Bw. Shekifu ambaye yupo katika ziara ya kukagua na kuhamasisha miradi ya maendeleo, aligoma kupigwa picha wala kuzungumza na waandishi wa habari kwa maelezo kwamba hajatoa ruhusa na ni makosa kumpiga picha bila idhini yake.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa, alifaya jitihada za kuwazuia vijana waliokuwa tayari wamebeba mawe kushambulia kundi la TOT.
Dk. Slaa aliwaeleza vijana hao ambao walikuwa katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kijungu ambapo CHADEMA ndio walikuwa wahutubie kuwa, vurugu zinazofanywa na CCM zinalenga kutaka kusababishwa kusogezwa mbele kwa uchaguzi.
``Vijana wangu kuweni wapole tu hawa wanataka tuwavamie na kuwaondoa kwa nguvu ili vurugu zitokee wapate sababu za kuahirishwa kwa uchaguzi huu,`` alisema Dk. Slaa.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kushuka jukwaani na kuzima muziki, Komba alisema kilichotokea ni masuala ya siasa na ni kweli kuwa CHADEMA ndio walikuwa na mkutano katika eneo hilo.
Hata hivyo, alisema waliamua kuvamia eneo hilo sio kufanya mkutano bali ni kupiga muziki na kudai kuwa hata wao CHADEMA hupita katika maeneo yao ya mikutano na kupiga muziki.
Mgombea wa Ubunge wa Jimbo hilo kupitia CHADEMA, Bw. Victor Kimesera, aliwaomba wananchi wa Kijungu kumchagua ili aongeze nguvu katika vita dhidi ya mafisadi na kuwaletea maendeleo.
Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kiteto, Bw. Festo Kang`ombe, naye alikiri kwamba jana kuwa CHADEMA ndio walipaswa kufanya mkutano katika eneo hilo kwa mujibu wa ratiba na alilaumu jeshi la polisi kwa kushindwa kudhibiti vurugu zinazotokana na kukiuka ratiba za mikutano ya kampeni.
Tukio hilo limekuja siku chache tu baada ya viongozi sita wa CHADEMA kuvamiwa na kupigwa na vijana wa CCM na polisi katika kijiji hicho.
Hata hivyo, hadi jana hakuna mtuhumiwa ambaye alikuwa amekamatwa na polisi.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe jana alianza kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la kiteto kwa kutumia helikopta.
Mapema kabla ya kutua na helkopta bila kuzuiwa, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bw. Shekifu na Mkuu wa Wilaya Bw. Henjewele walifika katika Uwanja wa shule ya msingi, Kijungu ambapo helkopta hiyo ilipangwa kutua na kuwaeleza viongozi wa CHADEMA kuwa helikopta hiyo haitakiwi kutumika.
Akizungumza na viongozi hao, Bw. Shekifu alisema serikali mkoani Manyara bado haijakubali kutumika kwa helikopta hiyo kwenye kampeni, kutokana na ukosefu wa taarifa ya ujio wake.
``Hapa leo helkopta haitashuka kwani tumeipinga na hatuna taarifa nayo,`` alisema Shekifu kuwaeleza viongozi wa CHADEMA.
Naye Mkuu wa wilaya hiyo, alifanya kikao na viongozi wa CHADEMA na maofisa wa polisi waliofika katika eneo hilo la Kijungu kutuliza ghasia na kusisitiza kuwa helkopta hiyo haitakubaliwa kutua katika wilaya yake.
``Jambo hili tumelijadili na msimamizi wa uchaguzi na tumekubaliana kuzuwia helikopta hii kutumika katika kampeni,`` alisema Henjewele.
Wakati huo huo, Mwandishi Wetu jijini Dar es Salaam anaripoti kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeruhusu chama chochote cha siasa kuweka wakala wa mgombea wake kutoka sehemu yoyote hata kama ni nje ya Kata au Jimbo la uchaguzi.
Kwa mujibu wa taarifa ya NEC, sheria ya uchaguzi namba 1 ya mwaka 1985 haijaeleza bayana Mawakala watoke ndani au nje ya Kata au jimbo la uchaguzi.
Taarifa hiyo ya NEC iliyotolewa na Mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC Bw. Rajabu Kiravu, ililenga kujibu madai ya msimamizi wa uchaguzi katika jimbo la Kiteto Bw. Festo Kang\'ombe, kupiga marufuku wakala wa kusimamia kura kutoka nje ya Kata au jimbo hilo.
Bw. Kiravu alisema, chama chochote kina uhuru wa kuweka mawakala wanaowataka kwa ajili ya kulinda kura za mgombea wao bila kujali kama ni mkazi wa eneo hilo au anatoka nje.
Hata hivyo, NEC imesema msimamizi wa uchaguzi katika kituo ndiyo mwenye mamlaka ya mwisho katika kutoa maamuzi na yeyote atakayeona ameonewa anatakiwa kufuata sheria na kujaza fomu husika.
Kuhusu suala la kuwaapisha mawakala, Bw. Kiravu alisema, kila wakala anatakiwa kuapa kutunza siri mbele ya msimamizi wa uchaguzi.
Alisema agizo hilo ni kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi namba 1 kifungu cha 93 (1) ya mwaka 1985.Bw. Kiravu alisema, kesho ndiyo siku ya mwisho ya kuwaapisha Mawakala.
Naye Raymond Kaminyoge anaripoti kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Bw. John Tendwa, amelitaka Jeshi la Polisi kuwakamata waliofanya vurugu katika uchaguzi wa jimbo la Kiteto, mkoani Manyara, badala ya \'kukimbizana\' na wauza gongo.
Bw. Tendwa alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu vurugu zilizotokea hivi karibuni.
Alisema wanapoachia vurugu kama hizo kutokea bila kuwachukulia hatua wahusika, wanaweza kuifikisha nchi hii katika machafuko kama yaliyotokea nchini Kenya.
Alisema inashangaza kuona kuwa pamoja na vurugu zilizotokea waliofanya vurugu hawakukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola badala yake imetuma maofisa kwenda kufanya uchunguzi.
``Katika kampeni za uchaguzi kunakuwa na polisi wanaolinda usalama, wilaya ya Kiteto ni ndogo inasikitisha kuona kuwa vurugu zimetokea bila watuhumiwa kukamatwa, badala yake polisi wanakimbizana na wauza gongo,`` alisema.
Aliongeza: ``Polisi wasikwepe lawama kwa tukio hilo, hatutaki waje kutufikisha katika matukio mabaya ya kuuana kama yanayotokea nchini Kenya.``
Aliviasa vyama vyote vinavyoshiriki katika uchaguzi huu kuheshimu kanuni za maadili ya vyama vya siasa ili kuepuka ubabe, vurugu na uvunjifu wa amani.
``Katiba ya nchi ibara ya 20 (2) (C) inasisitiza kuwa chama cha siasa hakiwezi kusajiliwa ikiwa katiba yake au sera zake zinakubali au kuchochea vurugu au matumizi ya nguvu kwa maana hiyo chama chochote chenye usajili wa kudumu kinaweza kupoteza sifa ya kuitwa chama cha siasa,`` alisema.
Jumapili iliyopita viongozi sita wa chama cha CHADEMA walijeruhiwa kwa kupigwa, kuchomwa visu na kupuliziwa machoni kemikali ambayo haijatambuliwa.
Kampeni za uchaguzi mdogo katika jimbo hilo unafanyika ili kuziba pengo la aliyekuwa Mbunge wa Kiteto, Bw. Benedict Losurutia aliyefariki mwishoni mwa mwaka jana.
Wakati huo huo, Chama cha CUF kimedai kuwa mashambulizi dhidi ya viongozi wa CHADEMA waliojeruhiwa jimboni Kiteto mkoani Manyara kwenye kampeni za uchaguzi mdogo unaofanyika keshokutwa, yalifanywa na CCM na polisi.
Kaimu Mkurugenzi Haki za Binadamu na Mahusiano na Umma wa CUF, Bw. Mbaralah Maharagande, alitoa madai hayo jana katika taarifa yake iliyosambazwa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi huyo alisema inasikitisha kuona kuwa CCM inakana kuhusika na vitendo hivyo na kuongeza kuwa mashambulizi yanayofanywa na chama hicho wakati wa uchaguzi yanajulikana na mifano ipo wazi na Watanzania wanaijua .
``CUF inasikitishwa na kauli ya Katibu Mwenezi wa CCM Bw. John Chiligati ya kukana vitendo vya vurugu zilizofanywa na makada wa CCM kwa kushirikiana na polisi dhidi ya viongozi wa CHADEMA katika kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Kiteto.``