Anaandika Malisa GJ
Tume ya Uchaguzi nchini Zambia (ECZ) imemtangaza Hakainde Hichilema wa chama cha UPND kuwa mshindi wa kiti cha Urais wa nchi hiyo kwa kura 2,965,326 sawa na 60.1%, akifuatiwa na Brian Mundubike wa NRPUP aliyepata kura 1,856,217 sawa na 38.6% ya kura zote zilizopigwa. Wagombea wengine wamepata chini ya asilimia moja.
Hichilema mwenye umri wa miaka 64 amewahi kugombea Urais wa nchi hiyo mara 5 akishindwa, kabla ya mwaka 2021 kufanikiwa kumwangusha Rais Edgar Lungu aliyekuwa akigombea kwa muhula wa pili. Kwa matokeo ya leo, Hichilema ataongoza taifa hilo kwa awamu ya pili hadi mwaka 2031.
Hata hivyo mwitikio wa kupiga kura haukuwa mkubwa kwani ni watu milioni 4.9 tu waliojitokeza kwenye vituo vya kupiga kura kati ya watu milioni 8.4 waliojiandikisha.
Hichilema ametangazwa mshindi wa kiti cha Urais majira ya saa 9 usiku kwa saa za Zambia sawa na saa 10 alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki. Tume ya Uchaguzi nchini humo (ECZ) haijaeleza kwanini imeamua kumtangaza mshindi wa Urais usiku wa manane watu wakiwa usingizini.
Hata hivyo wakati Tume ikitangaza matokeo hayo usiku, mgombea wa upinzani Brian Mundubike amejificha ofisi za umoja wa mataifa (UN) kuomba hifadhi akihofia kukamatwa na Polisi. Jana polisi walimtuhumu kwa uhaini, akidaiwa kusuka mipango ya kuiangusha serikali. Zaidi ya watu 20 walio karibu nae wamekamatwa na kupewa kesi za uhaini.
Pia mapema leo Wizara ya mambo ya ndani nchini humo, imemtangaza Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Mhashamu Trevor Selwyn Mwamba kuwa Mhaini na kwamba atakamatwa na kuunganishwa katika kesi ya kujaribu kuangusha serikali, inayomkabili Brian Mundubike na wenzake.!