Mkataba Kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya DPW ya Emirates Dubai umeacha maswali mengi na kuamsha hisia za kudai Katiba mpya kwa nguvu zote.
Ni mkataba ambao ulisainiwa kwa mwendokasi bila kuchukua tahadhari juu ya madhara yake yaliyo dhahiri. Mkataba huu haukubaliki kwa sababu nyingi Sana.
Moja , ni mkataba wa milele kwa sababu hauna ukomo. Najua wapo waliosema ni wa miaka 100 na wapo waliosema ni wa miezi 12.
Hawa wote sijui wametoa wapi huo muda wa mkataba. Ibara ya 23 ya mkataba na randama zake (appendixes) zake hakuna popote zinaonyesha mkataba huu ni wa muda gani. Hii inaweza kutafsiriwa kuwa ni mkataba wa kudumu.
Ni kweli unaweza kuwa miaka mia lakini pia hakuna Cha kuzuia uwe wa miaka 1000.
Pili, mkataba huu unanguvu kuliko Sheria za Tanzania pamoja na Sheria za kimataifa ( Takes precedent over national and international law)
Mathalani Ibara 23( 4) hairuhusu kuvunja mkataba huu hata pakiwa na ukiukwaji mkubwa ( material breach) au kukitokea hali inayopelekea mkataba usitekelezeke ( fundamental change of circumstances) ambalo ni Takwa la mkataba wa kimataifa uitwao Vienna Convention on the Law of Treaties,1969 ambao Tanzania imejifunga nao.
Sasa hii tafsiri yake ni kwamba baada ya kusaini mkataba huu hata Dubai wakikiuka kabisa hatuwezi kujitoa. Hicho ni kitu Cha ajabu mno dunia itatushangaa.
Mbaya zaidi mkataba hausemi je una nafuu ili mbadala ukiachilia mbali kuvunja mkataba.
Kifungu Cha 23( 4) kinaenda mbali zaidi na kusema ikitokea sababu yeyote inayotambulika kwenye Sheria za kimataifa ya kupelekea kuvunja mkataba bado mkataba huu hautavunjwa.Tafsiri yake ni kwamba tumeingia kwenye shimo ambalo halina pa kutokea( coup de sac) .
Tatu , mawanda ( scope ) ya mkataba pia ni mapana, ni Kama hayana ukomo. Ibara ya 2(1) itaruhusu muwekezaji kujenga na kuendesha miradi ya bandari za Bahari na maziwa yote.
Mkataba unakwenda mbali zaidi hata kwenye kile kinachoitwa logistic parks na trade corridors ambazo bahati mbaya hazijatafisiriwa kwenye mkataba.
Kwa namna mkataba huu ulivyo sisi tutakuwa tumepoteza udhibiti wa bandari zote za bahari na maziwa yote.
Mkataba ungeweka wazi ni bandari zipi hasa kwa sababu kwa namna ya Sasa hata usalama wa nchi unaweza kuwekwa rehani.
Nne , mkataba hausemi sisi tutapata nini( consideration) kwa maana ya faida za mradi. Je sisi tutakusanya Kodi tu? Au tutakuwa wabia?
Tano , mkataba hauonyeshi nafasi ya mamlaka ya bandari( TPA) ni ipi katika uendeshaji wa mkataba. Kumbuka kwa mujibu wa sheria TPA ndo chombo chenye mamlaka ya kuendesha bandari zote. Sasa je mkataba huu umefuta sheria hiyo? Kwa mamlaka gani?
Mkataba hauelezei kuhusu usalama wa mapato yetu bandarini na nafasi ya vyombo vya ulinzi na usalama kwaajiri ya usalama wa nchi yetu hasa kwenye marine.
Nafasi pekee ya TPA kwa mujibu ya randama ya kwanza imeachiwa kuendesha na kusimamia " DHOW AND WHARF TERMINAL" ya bandari ya Dar es Salaam.
Sita , pamoja na kuweka kipengele Cha local content ili kunufaisha wazawa kwenye ajira na manunuzi kwenye ibara 13( 2) ibara hiyo haina maana yoyote Kwanza kwa sababu haiweki wazi kwamba threshold ya wazawa kwenye ajira itakuwaje.
Pili hata procurement( manunuzi) ya vitu au items au huduma zinazopatikana ndani hailindwi na mkataba kwa sababu kwa mujibu wa ibara ya 6(2) ya mkataba huu serikali yetu hauruhusiwi kufanya usumbufu wowote (interference) yoyote hata kwenye manunuzi yanayokiuka Sheria isipokuwa tu Kama yanahatarisha usalama( safety and security).
Sasa je wakiamua kuagiza mbao Dubai wakati hapa nchini zipo utawazuia kwa kigezo Cha usalama?
Saba , mkataba hausemi nani atawajibika kulipa fidia yoyote inayotokana na utekelezaji wa mradi pamoja na watumishi ambao ajira zao zinaweza athiriwa na mradi.
Nane , pamoja na kwamba ibara ya 26 ya mkataba inaelekea kuruhusu reservation utagundua kwa namna ibara ya 24 ilivyo imepoka kwa mkono mwingine haki ya reservation iliyopo kwenye ibara ya 26 hivyo sioni uwezekano wa nchi yetu kufanya reservation kwenye makubaliano bila kukwaza mkataba.
Kwa namna ya mkataba huu tukifanya reservation Sasa ivi inaweza kupelekea nchi iingie kwenye mgogoro wa kukiuka mkataba.
Tisa , hata kuridhiwa kwa mkataba huu na Bunge tayari umefanyika nje ya muda.
Ibara ya 25(2) ilitaka mkataba uridhiwe ndani ya siku 30 tu na leo ni zaidi ya miezi Saba.
Kumi , kwa mujibu wa ibara ya 8(3) (c ) mkataba huu ni kama unatoa umiliki wa ardhi kwa mwekezaji kinyume na Sheria ya ardhi.
Kwa mujibu wa sheria ya Ardhu Sura ya 113 Kampuni ya kigeni hairuhusiwi kumiliki ardhi Tanzania.
Tulitegemea mkataba useme ardhi zitakuwa chini ya TPA au mamlaka nyingine za serikali na wao watapata derivative rights badala ya kuwapa ardhi kwa mgongo wa lease hold.
IBRAHIM JEREMIAH
S.L.P 602
SONGEA
06/06/2023
KATIBU WA BUNGE, OFISI YA BUNGE
10 BARABARA YA MOROGORO
S.L.P 941,
40490 TAMBUKARELI
DODOMA
YAH. KUPINGA AZIMIO LA UBINAFSISHWAJI WA BANDARI KWA KAMPUNI YA DP WORLD
Ndugu
Husika na Kichwa cha barua hapo Juu,
Mimi ni Mtanzania ambaye nimeguswa na suala hili na kimsingi nina wajibu wa kutoa maoni yangu ili Taifa letu lisiingie matatizoni,
Jambo hili limezua taharuki kwa Watanzania wengi waliosoma na kusikia taarifa hii kwasababu Bandari ni jambo linalohusu Umma,
Lakini pia mchakato huu umekuwa wa haraka na ushirikishwaji wa wananchi umekuwa mdogo sana, hivyo umesababisha kuongeza mashaka zaidi kwa Watanzania,
Hivyo nashauri mkataba huu ubatilishwe kwasababu hizi zifuatazo,
Bandari ni moyo wa Uchumi wa nchi na Kitovu kikubwa cha mapato yetu hivyo kwa umuhimu na Unyeti wake ni muhimu maeneo haya yasibinafsishwe na yakaendelea kuendeshwa na Watanzania wenyewe,
Kupitia uwekezaji huu umetolewa ufafanuzi kuwa Ubinafsishaji wao utaleta mapato kwa asilimia 233,
Imani yangu ni kuwa kupatikana kwa mapato haya hakutumii miujiza,
Ikiwa tutawekeza na kuongeza umakini katika usimamiaji tunaweza kupata mapato zaidi ya asilimia ambazo zimesemwa na wawekezaji,
Athari za Kiulinzi na Kiusalama
Ikiwa Bandari itaendeshwa na Kampuni binafsi kwa asilimia 100 kutakuwa na athari kubwa za kiulinzi na Kiusalama,
Hivi karibuni zimesambaa taarifa za Wanyama wa Afrika kupelekwa Dubai, lakini yapo madini, madawa ya kulevya, Pembe za ndovu na vitu vinginevyo vinavyosafirishwa kwa magendo,
Kama tutaruhusu Ubinafsishaji maana yake hata kama tutatoa ulinzi kutokana na Rushwa bado walinzi wetu wataitumikia Kampuni ya kiarabu,
Uwekezaji ni Biashara
Na hakuna Kampuni inayowekeza ili kupata hasara hivyo faida itakayopata Kampuni hii itawanufaisha waarabu wa Dubai,
Kwa lugha rahisi waarabu watachukua Pesa yetu na kwenda kujengea kwao, Jambo ambalo halitainufaisha nchi yetu,
Lipo suala la Ajira,
Ubinafsishaji huu utaleta tatizo la ajira kwa Watanzania kwasababu Waarabu hupenda kuajiri watu wao,
Waajiriwa wa nafasi kubwa katika Kampuni nyingi za Kiarabu hapa nchini huwa ni waarabu, Watanzania wa asili wengi huajiriwa kwenye nafasi za Utwana, nafasi za chini hivyo itapelekea Watanzania kutonufaika na uwekezaji huu na hivyo uwekezaji utawanufaisha waarabu zaidi katika soko la ajira,
Pia Dubai ni nchi ya Kidini hivyo utaratibu wa uajiri katika kampuni hii utakuwa wa Kidini Jambo ambalo si utamaduni wetu na litapelekea kukosekana kwa umoja wa Kitaifa na kuleta athari za kidini,
Mkataba huu ni wa muda mrefu,
Mikataba ya muda mrefu inaleta athari baadae ikiwa awamu zijazo zitakuwa na mpango tofauti katika shughuli za uendeshwaji wa Bandari,
Nyote ni mashahidi kuwa tumekuwa tukipitia wakati mgumu katika kubadilisha na kuvunja mikataba mingi ya muda mrefu iliyosainiwa kipindi cha nyuma ambayo haililetei tija Taifa mfano mikataba ya Madini na Makinikia ambapo madini yetu yamekuwa yakichukuliwa nje pasipo kutuletea tija yoyote hivyo ni muhimu mikataba hii ya muda mrefu tuisitishe na tuwe na utaratibu wa kufanya mikataba ambayo inakuwa ndani ya muda wa viongozi wa wakati huo ili isilete athari kwa Serikali zijazo na vizazi vijavyo,
Kuipa Kampuni ya Taifa jingine kuendesha Bandari kutalishushia heshima Taifa letu, Mkataba huu unakwenda kututukana na kutudhalilisha kimataifa kwasababu tutaonekana tumeshindwa kujiongoza wenyewe hususani kwenye rasilimali hii muhimu ambayo haitakiwi kufanyiwa mnada na mzaha wa namna hii,
Utofauti wa tamaduni za utendaji kazi na tamaduni zetu,
Dubai wanafanya kazi Jumatatu mpaka siku ya Alhamisi, siku ya Ijumaa inakuwa kama mapumziko lakini pia katika mwezi wa Ramadhani shughuli huwa zinasimama na kazi zinafanywa kwa nusu siku tofauti na hapa kwetu ambapo shughuli zinafanywa wakati wote,
Kwa kiasi fulani Dubai wanafanana sana kitamaduni na Zanzibar kuliko huku Bara hivyo kutakuwa na mtafaruku wa Kitamaduni hususani katika sehemu inayohusu Umma kama hii,
Kwa haya machache niliyoyoaanisha nashauri mapendekezo haya yasipitishwe na mkataba huu uvunje kabla ya kuja kutuletea athari Watanzania!
Wako katika kupigania maslahi ya Taifa
IBRAHIM JEREMIAH