Siupingi ushauri wako ila nataka nikusahihishe kidogo.
Idadi ya watu waliohesabiwa wakati wa sensa, kiuhalisia hakuna uhusiano na idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa vyuo vikuu. Miaka ya 1990, wakati wa utawala wa Mwinyi, chuo kikuu kilifungwa kwa sababu ya mgomo wa wanachuo. Wanachuo wote waliamriwa kila mmoja kuripoti mkoani kwake, akianzia kwenye Serikali ya kijiji na kisha wilayani.
Mwisho wa zoezi lile zilitolewa takwimu za wanachuo wote kwa kadiri walivyoripoti vijijini, wilayani na mikoani kwao.
Matokeo yake yalikuwa:
1) Mkoa uliokuwa na wanachuo wengi UDSM kuliko mkoa wowote, ni Kagera.
2) Wa pili ulikuwa ni mkoa wa Kilimanjaro
3) Wa tatu ulikuwa Mbeya.
4) Wa nne ulikuwa mkoa wa Iringa
Dar es Salaam yenye idadi kubwa maradufu kuliko mikoa yote, haukuwemo hata katika ile mikoa 5 yenye wanachuo wengi UDSM.
Njombe inaweza kuwa na idadi ndogo ya wakazi waliohesabiwa wakiwa Njombe. Lakini wakawepo wengi waliohesabiwa wakiwa maeneo mbalimbali ya nchi. Huo mkoa, wakazi wake ni watafutaji sana wa fursa. Popote penye fursa watakuwepo. Hiyo ni kuanzia kwenye fursa za Elimu mpaka fursa za kiuchumi.
Ukienda israel ukawahesabie Wayahudi, hawafiki hata 6m. Lakini Waisrael wanaoishi nje ya Israel, ni zaidi ya 19m. Ukiwatazama waisrael waliopo Israel tu, utasema Israel ni nchi yenye watu wachache sana.
Njombe kuna tawi pia la chuo kikuu cha Tumaini. Sijui kama na wao wamefuata ukabila!
Mimi nadhani, vyuo, ni kama mabenki, utashangaa mabenki karibia yote yapo Kahama na siyo Shinyanga au Tabora. Mabenki hufanya utafiti wake wa ndani ili kujua mahali penye pesa. Kuna maeneo watu wana mwamko zaidi wa elimu, kuna maeneo watu wana mwamko zaidi wa biashara, uvuvi, ufugaji kuliko masuala ya Elimu. Ukipeleka huko shule yako utaishia kukaa na majengo yako bila wanafunzi.
Kabla ya shule za kata, mkoa wa Iringa ndio uliokuwa unaongoza kwa idadi ya sekondari za Serikali kuliko mkoa mwingine wowote. Je, ilikuwa ni ukabila? Niliwahi kuambiwa na afisa mmoja wa Serikali kuwa kilichosaidia Iringa kuwa na shule nyingi ilikuwa ni pamoja na hali nzuri ya hewa inayotengeneza mazingira mazuri ya kusoma. Akidai kuwa miongoni mwa maeneo mabaya ya kusomea ni Dar ambayo ina joto kali na humidity kubwa inayosababisha wanafunzi kuwa wachovu wakati wote.
Nadhani ni vema kujenga hoja ya kupinga au kukubali bila ya kujenga fikra za ukabila, ambazo kimsingi haupo. Ukiacha kabila la wasukuma ambalo ni kubwa, Tanzania ina vikabila vidogo vidogo sana kiasi cha kuwa na mchango mdogo katika kufanikisha takwa la mtu anayetaka kutumia ukabila.