FaizaFoxy
Una pointi ya msingi kwamba sehemu kubwa ya lengo la ugaidi ni kuogopesha jamii na kuifanya ifuate matakwa ya magaidi.
Lengo hili linafanikishwa na kusambazwa kwa habari za ugaidi.
Hivyo, kwa upande mmoja, kukataa kuripoti habari hizi za ugaidi kunaweza kusaidia kudhoofisha kiasi cha lengo hili kufikiwa.
Vyombo vingi vya habari vimeshawahi kufanya namna ya jambo hili. Mfano mmoja ni vyombo kadhaa vya Marekani vilivyokataa kutaja jina au kutoa picha ya Adam Lanza aliyeua watu kwa kuwapiga risasi ovyo katika shule ya Sandy Hook Connecticut.
Lakini, tunapoangalia tija ya kufanya hivi, tupime kwa mizani itakayotuletea tija bila kuleta madhara mengine.
Nchi za kidemokrasia zinaendeshwa kwa misingi ya uwazi na uhuru wa habari. Wananchi wana haki ya kupewa habari. Wanahabari wana wajibu wa kutoa habari.
Zaidi, habari za ugaidi zinaweza kusambazwa katika lengo na minajili ya kumaliza ugaidi.
Mathalani, habari za ugaidi zinaweza kuenea, ikiwamo picha za magaidi, na kusaidia magaidi hao kukamatwa kwa msaada wa wananchi.
Pia, habari za ugaidi zinaweza kusambazwa na kuweza kuisaidia jamii kujihami. Mfano, kama eneo la Rufiji lina ugaidi, habari za kuwaasa wananchi kwamba wachukue tahadhari wanapotembelea eneo hilo, kwa sababu lina ugaidi, zitakuwa habari muhimu katika kuwatayarisha wananchi wajihami vizuri na kuchukua tahadhari zote kabla ya kutembelea eneo hilo.
Kwa kifupi, kwa upande mmoja kuna haja ya kuacha kuhamanika sana na kuandika habari za ugaidi ovyo kiasi cha kutisha wananchi na kuwasaidia magaidi. Kwa upande wa pili, kuacha kabisa kuandika habari za ugaidi kutaweza kusababisha matatizo vilevile.
Kuna kanuni kadhaa nzuri na muhimu katika kuamua kutoa ama kutotoa habari ya kigaidi.Chache kati ya hizo ni:-
1. Habari itasaidia kuelimisha jamii kupambana/ kujihami na ugaidi?
2. Habari itamsaidia zaidi nani? Jamii au gaidi?
3. Kamahabari ikitolewa, itolewe kwa kiwango gani? Kutoa picha za watu waliouawa kinyama kutafaa au kutakosa staha kwa umuhimu wa maisha ya binadamu?
4. Habari zimethibitishwa au hazijathibitishwa na zinaweza kusababisha kashfa isiyo kweli (libel)?
5. Habari zinaandikwa kwa ukweli (facts) tu na si kwa ushabiki.
6. Gaidi hapewi uwanja wa kujitangaza zaidi ya inavyohitajika kuihami na kuifunza jamii.
7. Habari haiingilii wala kuharibu uchunguzi wa polisi na vyombo vya usalama.
8. Habari haihatarishi usalama wa raia wasio na hatia (kama kutaja vyanzo vinavyoweza kuumizwa na magaidi)
9. Habari haihatarishi usalama wa waandishi wa habari. Ikifikia sehemu ambayo waandishi wataanza kuhatarisha usalama wao,usalama wao uwe na kipaumbele kuliko habari.
10. Mizani mizuri itumike kati ya kuchapisha habari mapema na kuihakiki vya kutosha ili isiwe na au ipunguze makosa.