Sidhani kama Prof. Assad alimaanisha hivyo,kuwa tuwe na Rais anayemsikiliza kila mtu. Kumekuwepo na madhara makubwa sana ya kuwa na viongozi wasioshaurika viongozi wanaodhani na kuamini wao wana akili kuliko watu wote. Hata mipango/miradi yao mingi ni ya kukurupuka pamoja na kuwa na nia njema. Nia njema haihalalishi njia mbovu. Lakini naamini wapo watu walioshauri kwa utalaam walikuwa nao na hawakupewa nafasi.
Nilichoelewa anachomaanisha ni kuwa na mfumo imara wa kumdhibiti Rais dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka.
Marekani ingekosa mfumo imara,watu Kama Rais Trump kwa yale aliyokuwa akijiapiza kuyafanya akichaguliwa kuwa Rais, sijui kama hata nyie mnaoishi huko mngesalimika na bila shaka na ule ukuta wa kuitenga Mexico ungekuwa umeisha.
Mfumo imara utamlazimisha Rais kuheshimu sheria na katiba ya nchi.
Mfumo imara hautaruhusu kuunda sheria kandamizi, kama za vyombo vya habari, au kuunda sheria za kulinda watu wasishtakiwe wakiwa madarakani ndo tunajikuta na watu Kama kina Ndugai anafanya anachotaka kwenye mhimili mzito Kama bunge kisa anayo kinga.
Mfumo imara utazaa bunge huru,leo bunge letu linategemea na nani ni spika kwa wakati huo, angalia kwa kesi zile zile alivyoamua Ndugai na kesi zile zile anavyoamua Tulia.
Mfumo imara utatupa mahakama huru, angalau kidogo kama mahakama zilee chini ya Mzee Nyalali au Barnabas Samata,ulikuwa huwezi kuwaona kwenye shughuli zozote za propaganda,siyo hawa wa sasa, mara kwenye makinikia na wao wapo,halafu sijui kama wenye hayo makinikia,hawaridhiki unawategemea waziamini mahakama zetu,wakati umemuona CJ yuko kiti cha mbele anasikiliza anatikisa na kichwa kwa huzuni. Mfumo imara utatupa tume ya uchaguzi huru siyo hii ambayo nayo inaushangaa uchaguzi wa 2020 ulivyoendeshwa.
Mfumo imara utaweka mipaka ya kiutendaji kwa vyombo vyetu vya dola.
Polisi au JWTZ watajihusisha na majukumu yao ya kikatiba tu na kamwe haitawezekana kuwatumia kisiasa.
Mfumo imara utawapa wananchi heshima kuwa wao ndio wamiliki wa nchi hii na raslimali zake, na siyo kuambiwa eti Rais ametoa fedha za mradi huu kana kwamba ni za kwake na ni hisani yake,utaondoa kauli za kuzimu kama zile,eti mkichagua upinzani hatuwaletei maendeleo,kauli za kibaguzi na wizi mkubwa,unawanyima maendeleo wakati na wao ni wachangiaji wazuri wa pato la nchi kupitia Kodi zao.
Mfumo imara utajenga watanzania wenye kujiamini,wenye kujua haki zao na kuzisimamia na siyo,tabia ya sasa ya kuwa na watu wanafiki wasioaminika,kwao ni kujipendekeza kwenda mbele kisa Rais aliyeko ni kabila lake, au wa dini yake au chama chake.
Tunatamani kuwa na wasomi angalau kidogo wa enzi zile za kina Prof. Chachage, Haroub Othman, Mwesiga Baregu, Mwaikusa na wengine ambao wakikutana Nkurumah hall mpaka nchi jirani zinafuatilia.
Tuwe na wataalam wenye exposure ya kutosha kusimamia raslimali zetu, na siyo tunayoyashuhudia sasa. Tunao wahandisi wazuri midomoni wape kazi sasa ushangae. Bidhaa nyingi tunazoona toka china ukisikia wanaozitengeneza hata diploma kama wanazo ni wa kuhesabu. Hivyo lazima tuwajengee uwezo wataalam wetu kwa kukusudia.
Ni ngumu sana kuamini Maendeleo yetu yatategemea wawekezaji kutoka ulaya na Asia bila kuhakikisha tunawawezesha watu wetu kupata utalaam na wao kuwa na uwezo wa kuanzisha viwanda wenyewe. Wakati Saab scania wanafungua tawi lao hapa Tanzania 1972, pia na Brazil walianzisha, leo ya kwetu imekufa wakati ya Brazil wanatengeneza scania 95% ni 5% tu wanaagiza Sweden.
Hatuwezi kujilaumu na kujuta bado tunayo nafasi ya kufanya vizuri zaidi.
Tupiganie tupate mfumo imara.