Taifa letu tuna bahati mbaya sana, tulipata uhuru wa kisiasa tukiwa hatuna wasomi wa kutosha, ikitegemewa kwamba, baada ya kupata uhuru, ndio tungeenda kuwekeza ili kuwaondoa wale maadui watatu ikiwemo ujinga.
Bahati mbaya sana, licha ya kuongeza idadi ya wasomi, lakini bado tumejikuta tuna tatizo kubwa zaidi, kubwa zaidi ya kutafuta ule uhuru wa kisiasa, wasomi waliotegemewa waje kuikomboa nchi kifikra, wamegeuka wajinga wanaopenda kuishi kwa kujipendekeza kwa watawala, huku wakichekelea bila aibu kwa vyeo wanavyopewa.
Matokeo yake sasa, wasomi hao toka idara mbalimbali za serikali ambao wangetegemewa walisimamie taifa kwenye kulinda rasilimali zake, ikiwemo TISS, wamegeuka chawa wa mtawala wanaofanya kila wanaloamriwa bila kuzingatia kama lina maslahi kwa taifa ama hapana.
Sasa tumegeuka taifa la wajinga tusio na mwelekeo, kila mmoja anajitazama binafsi hajali jirani yake ana shida gani, wabunge wamegeuka walafi licha ya mishahara mikubwa na posho, lakini bado wanadanganyika kwa rushwa, tena mbaya zaidi, rushwa inayozitoa sadaka rasilimali za nchi yetu, hii kwangu ni laana.
Hapa tumekaa tunasubiri maamuzi ya mahakama kwenye kesi zilizofunguliwa kupinga ule uwekezaji wa kihuni, tuone kama wasomi kwenye mahakama zetu wataona umuhimu wa kulinda rasilimali zetu, au nao watageuka kama wasomi wa bungeni na serikalini waliotusaliti, ili mwisho wa siku, umma wa Tanganyika ujiamulie kulinda rasilimali zao, tena kwa nguvu zao wenyewe, wasomi tuliowategemea, wamegeuka hasara kwa taifa, wasomi wasiojua hata kuhoji!.