» Home » Habari za Kitaifa » Msuya akabidhiwa Kibo Breweries
Msuya akabidhiwa Kibo Breweries
By Habari Tanzania | Published 10/23/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Ramadhani Siwayombe, Moshi
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), imekifunga kiwanda chake cha bia kilichopo mkoani Kilimanjaro, maarufu kwa jina la Kibo Breweries na kumkabidhi majengo pamoja na mitambo ya kiwanda hicho, Mwenyekiti wa Kilimanjaro Development Forum (KDF), Waziri Mkuu mstaafu, David Cleopa Msuya. Makabidhiano hayo yalifanyika juzi mjini Moshi katika kiwanda hicho kati ya Mkurugenzi Mkuu wa TBL, Craig Mac Dougall na Msuya.
Mac Dougall alisema wameamua kutoa majengo ya kiwanda hicho kwa KDF kutokana na azima yao ya kutaka kushirikiana na jamii katika kuhakikisha wananchi wa Kilimanjaro ambao ni wadau wakuu wa biashara yao wanapata fursa ya kujikwamua kiuchumi kupitia taasisi hiyo ambayo itakuwa kiungo muhimu kati ya kampuni hiyo na wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro. Alisema wametoa majengo hayo ili yatumike kuendesha miradi mbalimbali ambayo itatoa ajira kwa wananchi wa Kilimanjaro, na wao kama kampuni kwa kipindi cha miaka mitatu wataisaidia taasisi hiyo kulipia baadhi ya gharama, ikiwamo umeme, maji na walinzi, ili kuiwezesha taasisi iweze kujiendesha kwa faida katika miradi watakayoanzisha katika kiwanda hicho.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa majengo hayo, Msuya alisema wamefarijika kwa msaada huo, kwani mkoa huo kwa hivi sasa umekuwa ukiyumba kiuchumi kutokana na viwanda vingi kusimamisha uzalishaji, hivyo kupunguza mapato ya mkoa na pia ajira kwa wananchi wa mkoa huo.
Alisema baada ya kugundua upungufu huo ambao umetokana na kupungua kwa uzalishaji wa zao kuu la biashara la kahawa hadi kufikia tani nne kwa mwaka kutoka tani 28, waliamua kuanzisha taasisi hiyo ili kujaribu kusaidiana na serikali kuwasaidia wananchi wa mkoa huo kuboresha uchumi wao.
Akitoa tathmini ya mkoa, Mkuu wa mkoa huo, Mohamed Babu, alisema kutokana na viwanda vingi vilivyokuwapo kusimamisha uzalishaji na kufungwa, ajira 6,0852 zilizokuwapo zimepungua hadi kubaki 441 za wafanyakazi wa kudumu.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Cril Chami, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Salome Mbatia, na mke wa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Anna Mkapa