Kati ya vitu vinavyofanya sisi waafrika tuendelee kuwa maskini ni kutotumia akili zetu vizuri na pia kupenda sana madaraka/ vyeo.
Nimefuatilia kwa muda sasa kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na nilichogundua ni kuwa wale wengi wanaotaka Zanzibar iwe na Serikali au Tanganyika iwe na Serikali yake wengi ni wanasiasa na wanafanya yote hayo kwa maslahi ya kisiasa ili wapate vyeo vya kisiasa na kujinufaisha binafsi.
Pili, nimegundua uwepo wa Serikali 2 au 3 unawanufaisha zaidi hao wanasiasa kwa sababu uwepo wa Serikali hizo unawahikishia kupata nafasi za kisiasa ili waendelee kunufaika na kodi za wananchi kama vile Uwaziri, Ukuu wa Mikoa , Wilaya katika Serikali hizo mbili/tatu.
Mwisho katika ufuatiliaji wangu nimegundua kero hizi zinazoitwa za Muungano kama wabara kutoweza kumiliki Ardhi Zanzibar kama Wa Zanzibar wanavyomiliki Ardhi huku bara dawa yake ni moja tu yaaani Kuwa na Nchi 1 na Serikali 1 tu na Raisi 1 tu.
Ni vizuri tukiwa tunaenda kujenga daraja la kuunganisha Zanzibar na Tanzania tukafikiria pia kuwa sasa tuwe na nchi 1 na serikali 1 tu ili kuepusha sehemu kubwa ya kodi za wananchi kwenda kuhudumia Serikali 2/3 tena ambazo kiuhalisia hazina manufaa yeyote kwa mwananchi wa kawaida
Heri ya Siku ya Wafanyakazi
SULUHISHO LA KUDUMU LA MUUNGANO HUU WENYE KERO ZISIZOISHA:
1. Watu wa Tanganyika wenye makazi ya kudumu Zanzibar na Wazanzibar wenye makazi ya kudumu Tanganyika, wapewe uhiari, haki na uraia wa kuendelea kuishi Zanzibar au Tanganyika mtawalia.
2. Endapo Tanganyika na Zanzibar zitaendelea kuwa na uraia wa nchi moja, basi nchi hizi mbili ziwe na makubaliano maalum ya uraia maalum wa nchi mbili (Duo Exclusive Treaty on Special Dual Citizenship) kwa Watanganyika na Wazanzibar ambao watahiari kuwa na uraia wa nchi mbili baina ya Tanganyika na Zanzibar pekee.
3. Tanganyika na Zanzibar ziwe madola huru yenye mamlaka kamili kama ilivyokuwa kabla ya muungano na zijiunge katika jumuiya au taasisi mbalimbali za kikanda au kimataifa ikiwa pamoja na Umoja wa Mataifa (UN), FIFA, nk.
4. Pasiwepo viza ya kusafiria kati ya Tanganyika na Zanzibar isipokuwa vitambulisho vya uraia au hati za kusafiria (passports) zitumike kumtambua Mtanganyika au Mzanzibar.
5. Iundwe Tume ya Mahusiano na Ujirani Mwema baina ya Tanganyika na Zanzibar (Commission for Relations and Good Neighbourhood). Tume hii pamoja na mambo yatakayojitokeza, ifanye yafuatayo:
(a) Kuweka utaratibu wa kuimarisha uhusiano na ulinzi wa pamoja wa Majeshi ya Ulinzi ya Watu wa Zanzibar (Zanzibar People’s Defence Forces - ZPDF) na Majeshi ya Ulinzi ya Watu wa Tanganyika (Tanganyika People’s Defence Forces -TPDF). Wanajeshi wa Tanganyika na Zanzibar wataendelea kutumika kwa pamoja kulinda watu na mipaka ya Tanganyika na Zanzibar.
(b) Kugawanya madeni ya nje kulingana na uwiano halisi wa jinsi yalivyotumika kusaidia nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar.
(c) Kuratibu balozi za nje ili ziendelee kutumiwa pamoja kiofisi (shared consulates) kwa Tanganyika na Zanzibar hadi wakati ambapo uwezo wa kila nchi utaruhusu kuwa na ubalozi wake.
(d) Kuratibu fedha na/au sarafu za aina moja ili ziendelee kutumika kihalali kati ya Tanganyika na Zanzibar ili kudumisha uhusiano na utambulisho wa kihistoria.
Hitimisho
Nikiwa mwanafunzi wa Mwalimu Nyerere nihitimishe kwa kusema alichokataza ni kufukuzana baina ya Watanganyika na Wazanzibar. Akaita dhambi kubwa sawa na kula nyama ya mtu. Hakukataza maelewano na makubaliano ya kuagana kwa amani. Na sitegemei watu wanaokubaliana kwa amani watafukuzana au kupigana. Wala si sahihi kulinganisha hilo na Sudan ambao walipigana miongo kadhaa wagawane nchi.
Wakati vita vya Uganda na Tanzania vikielekea ukingoni kabisa, Mwalimu Nyerere alilaumiwa kuwa anataka kuimeza Uganda, wengine wakadiriki kusema kama alivyoimeza Zanzibar. Yeye alijibu kuwa lililo la msingi ni kudumisha amani na nchi jirani na kuwa na uhusiano mwema - si kuunganisha nchi. Tubakie majirani wema kama ilivyo kwa Zambia, Msumbiji, Malawi, Rwanda, Kenya na kwingineko. Kuwa na mahusiano mema na jirani ni jambo la msingi na si lazima muunganishe nchi.
Kuna nchi nyingi tunahusiana nazo vizuri sana na kwa ukaribu japo haziko jirani, sembuse Zanzibar na Tanganyika! Undugu ni mahusiano mema si kuunganisha nchi. Na ujirani na udugu wa kihistoria upo kwa nchi zote tunazopakana nazo, si Tanganyika na Zanzibar pekee.
Muungano usilindwe kwa vitisho, kulazimishana, kubanana, kufinyana, kupunjana na kulaumiana, bali kwa kujenga na kuimarisha mahusiano na ushirikiano mwema wa viongozi na wananchi wa hizi nchi mbili.
Kuna faida nyingi za kitaifa na kimataifa kwetu sisi Watanganyika kuwa nchi kamili, na vivyo hivyo kwa Zanzibar. Tusizibiane fursa na kuendelea kukerana au kulalamikiana!