Retrieved from Tanzania Daima 2/2/2013 and 9/2/2013
Oscar Kambona ni miongoni mwa viongozi mahiri na shupavu waliowahi kuwa gumzo ndani na nje ya Tanzania, kutokana na uongozi wake, hekima na busara.
Ndiye Mtanzania wa kwanza kuwa waziri aliyeongoza wizara mbili kwa wakati mmoja. Ndiye Mtanzania pekee anayeaminika kusimama kidete na kufanikiwa kulidhibiti jeshi lililoasi mwaka 1964.Hata hivyo, pamoja na umahiri huo, lakini kubwa zaidi kutokuwa na tamaa ya kutumia nafasi ya uasi wa jeshi kushika madaraka ya nchi.
Pamoja na hayo mchango wake hauthaminiwi kabisa. Tofauti na viongozi wengine wa siasa au hata utamaduni, mpaka sasa hakuna barabara yenye ukumbusho wa jina la mwanasiasa huyu aliyefariki akiwa katika matibabu mjini London, Juni 1997 na mwili wake kurudishwa Tanzania kwa mazishi.
Oscar Kambona alizaliwa mwaka 1925, katika kijiji cha Kwambe kilichoko mwambao mwa Ziwa Nyasa, karibu na Mbamba-Bay, wilaya ya Mbinga, mkoani wa Ruvuma.
Alikuwa ni mtoto wa Kasisi David Kambona ambaye alikuwa miongoni mwa Waafrika wa kwanza kupata upadri katika kanisa la Anglikana la Tanganyika, na kwa mama Miriam Kambona.
Akiwa mdogo, baba yake alikuwa akimweleza kuhusu ndoto zake juu ya uhuru wa nchi yake, hivyo kumfanya Oscar kujawa na hamu ya kuitumikia nchi yake. Msingi wa elimu yake aliupata nyumbani kwao, chini ya mwembe (ambao bado uko mpaka sasa), katika kijiji cha Kwambe, kwa kuwatumia wazazi wake wote wawili na mjomba wake, ambao wote walikuwa walimu.
Alipelekwa shule ya kati ya Mt. Barnabas, Liuli na baadaye Shule ya Sekondari ya Alliance (sasa Shule ya Sekondari Mazengo), ambako alilipiwa ada na askofu Mzungu wa Anglikana kwa vile baba yake hakuweza kumudu kulipa ada ya pauni 30 kwa mwaka. Inasimuliwa kuwa kilichomvutia Mzungu huyo kukubali kumlipia Oscar ada ni baada ya kusali sala ya Baba Yetu Uliye Mbinguni kwa Kizungu. Alichaguliwa kwenda Tabora Boys Senior Government School ambako ndiko alikokutana na Mwalimu Julius Nyerere kwa mara ya kwanza. Wakati huo Nyerere alikuwa anafundisha katika shule ya Kikatoliki ya St Marys.
Kukutana tena na Nyerere
Ilikuwa mwaka 1954, kwenye mkutano wa kitaifa wa walimu, ndipo Oscar Kambona ambaye naye alikuwa amemaliza shule na kufundisha katika shule ya Alliance, alikutana tena na Nyerere na kujadili mambo mbalimbali ikiwemo harakati za chama cha TANU. Oscar alishawishika kuitumikia TANU ambayo ilikuwa imeanzishwa muda si mrefu, bila malipo baada ya Mwalimu Nyerere kumweleza kuwa asingeweza kuajiriwa ndani ya chama kwa vile haikuwa na fedha.
Huo ulikuwa uamuzi mzito na mgumu mno, hasa kwa mtu kukubali kuachia nafasi ya ualimu ambayo alikuwa akilipwa vizuri na kufanya kazi bila malipo tena za chama ambacho ndiyo kwanza kilikuwa kikianza harakati za ukombozi. Kwa miezi takriban sita, Oscar Kambona alifanya kazi ngumu ya kuzunguka sehemu mbalimbali za nchi na kuonana na machifu na wazee wa vijiji ili kusajili wanachama.
Kwa kipindi hicho huku akitumia fedha kidogo alizokuwa amejiwekea akiba yake, alifanikiwa kusajili wanachama 10,000 na haikuwa ajabu kuwa baada ya mwaka mmoja alikuwa amepata wanachama hai 100,000. Ili kutunza fedha za chama, Kambona alifungua akaunti ya kwanza ya TANU na kisha kwenda Butiama kumshawishi Mwalimu Nyerere achukue uongozi wa chama moja kwa moja kama mtendaji mkuu.
Mwaka 1957, Kambona alikwenda kusomea sheria katika Chuo cha Middle Temple, nchini Uingereza kwa ufadhili wa Gavana. Akiwa London Kambona alikuwa kiongozi wa chama cha wanafunzi wa Tanganyika na mwenyekiti wa tawi la TANU la London.
Kukutana na watu mashuhuri
Mwaka 1958, Kambona alipata fursa ya kukutana kwa mara ya kwanza na watu mashuhuri akiwemo George Padmore, mwanaharakati wa umoja wa wa Waafrika duniani, ambaye alimshawishi ahudhurie mkutano wa Waafrika wote (All Africas Peoples Conference), uliofanyika nchini Ghana muda mfupi baada ya kupata Uhuru. Kambona alisafiri mpaka Ghana, wakati huo akiwa bado anaendelea na masomo yake nchini Uingereza na huko alipata nafasi ya kukutana na mwanaharakati mwingine maarufu wa siasa za Afrika, Kwame Nkrumah.
Utangazaji wake BBC
Kambona ndiye Mwafrika wa kwanza kutangaza taarifa ya habari kwa lugha ya Kiswahili, katika Idhaa ya Kiswahili ya BBC, ambayo sasa inajulikana kama (BBC Swahili). Inadaiwa kuwa alikuwa akipenda sana uandishi wa habari kwenye vyombo vya kimataifa. Katika kuhakikisha anapigania uhuru na mafanikio ya TANU, Kambona akiwa anaendelea na masomo yake nchini Uingereza, alikutana na Mwalimu Nyerere kila alipoenda nchini humo na kupanga mikakati ya kudai uhuru. Kambona alifunga ndoa na Flora Moriyo na harusi ilifungwa katika kanisa la Mt. Paul, London, na Nyerere ndiye alikuwa msimamizi.
Kurudi Tanganyika
Mwaka 1959, Kambona alirudi Tanganyika na kuendeleza harakati za kudai uhuru kupitia TANU, huku wakiweka bayana madai ya kupewa serikali ya madaraka. Kambona kwa kushirikiana na wenzake akiwamo Nyerere, waliweka mikakati mbalimbali huku wakiwa tayari kuanzisha mapambano kama ilivyokuwa kwa Mau Mau ya Kenya. Katika uchaguzi wa kwanza TANU ilishinda viti vyote isipokuwa kimoja na kuunda Serikali ya Mambo ya Ndani chini ya Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa Waziri Kiongozi wa kwanza. Kambona aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na baadaye alishika nyadhifa za Waziri wa Mambo ya Ndani, Mambo ya Nchi za Nje na Ulinzi na Tawala za Mikoa. Katika nyadhifa hizo, Kambona pia alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika na Mwenyekiti wa Utayarishaji wa OAU ambayo sasa ni AU.
Kuunganisha bara na visiwani
Mwaka 1964, Kambona alifanya kazi kubwa katika kuunganisha Zanzibar na Tanganyika, akiwa pamoja na Rais Nyerere na Karume. Hii ilikuwa ni baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Januari 20, 1964, wanajeshi wa kikosi cha Calito waliasi. Kambona akiwa waziri wa Ulinzi, alisimama kidete kusuluhisha na msemaji mkuu upande wa serikali huku viongozi wakuu Mwalimu Nyerere na makamu wake, Rashid Kawawa, ikisemekana wakiwa wamekimbilia mafichoni Kigamboni walikokaa kwa siku tatu za majadiliano mazito mpaka machafuko yalipoisha.
Moja ya nukuu za Kambona katika mahojiano na gazeti la Daily Telegraph la London, alisema, Baada ya kuwatuliza wanajeshi nilikwenda kuwatafuta viongozi wengine na kuwarudisha mjini kwa kutumia Land Rover yangu. Kambona alisifiwa sana na Mwalimu Nyerere kwa hekima na busara yake hadi kufanikiwa kumaliza uasi huo kwa kutumia nafasi yake ya uwaziri wa ulinzi. Wapo walioanza kuvumisha kuwa huenda kwa uaminifu wake, angeshika nafasi ya urais baada ya Nyerere kumaliza muda wake.
Ilikuwaje akawa adui wa serikali?
Ugomvi wa Nyerere, Kambona
Vyanzo mbalimbali vya habari hadi sasa vinashindwa kueleza ukweli juu ya hasa kile kilichosababisha kuzuka kwa tofauti kati ya Mwalimu Nyerere na Kambona. Kila mtu amekuwa akijaribu kueleza ugomvi wa wawili hawa kadiri ajuavyo. Kuna madai kwamba viongozi hawa wawili ambao kwa sasa wote ni marehemu, walianza kutofautiana baada ya maasi ya wanajeshi.
Inadaiwa kuwa Nyerere alitaka kuanzisha mfumo wa chama kimoja nchini ili kuimarisha usalama na Kambona alipinga hoja hiyo kwa maelezo kwamba mfumo huo ungezorotesha uhuru na maendeleo ya demokrasia. Hoja hiyo ikafikishwa bungeni kwa maamuzi na kwa bahati mbaya kwa Kambona akashindwa lakini akagoma kusaini muswada huo.
Katika safari ya China ya Mwalimu ya mwaka 1965, alipendezwa na mfumo wa kikomonisti wa Mao, na akataka kuanzisha mfumo kama huo kwa jina la Ujamaa hapa nchini.
Dhana ya msingi ya mfumo wa Ujamaa ilikuwa ni kuwahamishia watu katika vijiji vya ujamaa na kutaifisha viwanda na vitegauchumi vilivyokuwa vikimilikiwa na watu binafsi ili kuwa chini ya wananchi, hatua iliyopingwa vikali na Kambona kwa maelezo kwamba ungeongeza umaskini na udhibiti wa serikali kwa watu.
Inadaiwa kuwa kulikuwa na msuguano mkali, kiasi kwamba ilimlazimu Kambona alijiuzulu nyadhifa zake ndani ya serikali na chama na hatimaye yeye na familia yake wakakimbilia Nairobi, Kenya na kisha Uingereza ambako walipatiwa hifadhi ya kisiasa.
Mara baada ya kukimbia nchi, mali za Kambona zilichukuliwa na serikali, huku ndugu zake wawili, wakiwekwa kizuizini bila ya kufikishwa mahakamani na kufungwa kwa zaidi ya miaka kumi. Inaaminika kuwa wazo la Kambona lilikubaliwa na baadhi ya viongozi wa chama na serikali.
Hii inatokana na kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake, Bibi Titi Mohammed, Michael Kamaliza ambaye alikuwa mwanaharakati wa chama cha wafanyakazi, mwanachama wa TANU na waziri, pamoja na Gray Mattaka, Eliya Chipaka na Prisca Chiombola kwa tuhuma za uhaini. Viongozi hao walihukumiwa pamoja na Kambona licha ya kuwa alikimbilia London lakini walikata rufaa katika Mahakama Kuu ya Afrika Mashariki na wakaachiwa huru. Hata pamoja na kuachiwa huru,walikamatwa na serikali na kufungwa tena.
Tuhuma kubwa ya Kambona ni kwamba aliiba pesa nyingi za umma, na kukamatwa nazo alipopekuliwa katika uwanja wa Embakasi, mjini Nairobi jambo ambalo alilipinga kwa miaka mingi na kuliweka wazi katika taarifa yake kwa waandishi wa habari Septemba 6, 1967 huko London. Kambona alikwenda mbali zaidi akaitaka serikali ya Tanzania kuiomba Kenya kutoa ukweli juu ya jambo hilo, jambo ambalo halikufanyika hadi kifo chake.
Inaaminika kuwa maisha ya Kambona jijini London yalikuwa ya shida na dhiki. Mwaka 1982, baadhi ya ndugu wa Kambona waliachiwa toka kizuizini baada ya juhudi za Waziri Mkuu wa New Zealand, Robert Muldoon. Mwaka 1990, Kambona akiwa na matumaini makubwa ya mabadiliko ya kisiasa katika Tanzania, aliunda chama kiitwacho Tanzania Democratic Alliance, akiwa bado uhamishoni.
Kurudi Tanzania
Mwaka 1992, wakati mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa Tanzania, Kambona aliomba kurudi nchini. Hata hivyo, serikali ya Tanzania ilimkatalia katakata. Kuona hivyo, Kambona aliiomba serikali ya Uingereza kumpa pasi ya kusafiria kurudi Tanzania, lakini pia akakumbana na tishio la kukamatwa na kuwekwa ndani pindi angelitua.
Septemba 5, 1992, bila woga wa kukamatwa, Kambona alitua katika ardhi ya Tanzania na hakushikwa, badala yake alipewa miezi mitatu awe amekamilisha utata wa uraia wake. Nia yake ya kushiriki kwa nguvu katika harakati za siasa ilitiwa doa na kudorora kwa afya yake akisumbuliwa na shinikizo la damu.
Afya yake ilizidi kuwa mbaya, na hivyo akalazimika kurudishwa tena London Uingereza kwa matibabu. Hata hivyo, Juni,1997, Kambona alifariki akipishana kwa siku chache tu na mdogo wake Otini Kambona ambaye pia alikuwa nchini humo kwa matibabu ya moyo.
Katika namna ambayo yaweza kuelezwa kuwa ni tendo pekee la kumuenzi mwanasiasa huyo mashuhuri, serikali ilikubali kusafirisha mwili wake na wa Otini na pia shughuli zote za mazishi. Kambona ameacha mke na watoto wawili, akiwemo Neema Kambona ambaye hivi karibuni alijiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) tawi la London. Mtoto wa kwanza, Mosi Kambona aliuawa miaka si mingi sana iliyopita mjini London katika mazingira ya kutatanisha.
Kambona ameondoka, lakini pamoja na kuwepo kwa dosari hiyo ya kusigana katika siasa, alifanya makubwa mengi. Ni kiongozi pekee ambaye askari wa jeshi walipoasi na kuwalazimu Mwalimu Nyerere na Rashid Kawawa kukimbia, angeweza kutwaa madaraka ya nchi baada ya kufanya mazungumzo yaliyowalainisha wanajeshi hao.
Bila tamaa Kambona, alikwenda Kigamboni kuwachukua Mwalimu Nyerere na Kawawa waliokuwa mafichoni, na kubaki mwaminifu kwa nafasi yake ya uwaziri aliyokuwa nayo. Kambona kasahaulika pamoja na uaminifu huo na mema yote kiasi kwamba hakuna hata sehemu ya kumbukumbu inayomwelezea kwa mazuri yake. Ameingizwa katika kapu la waliosahaulika!
My Take
Pamoja na sifa nyingi tunazompa Nyerere, ukisoma stori hii unatambua kwamba Nyerere hakuwa mtu mzuri kama tunavyomuelezea. Alikuwa na ubabe wa kijinga. Naweza sema Nyerere amekuwa chanzo cha umasikini mkubwa tunaokabiliana nao nchini.