SEHEMU YA NNE (04).
Namna majini walivyoanza kufichua ukweli wao wenyewe na kujidhihirisha kwa familia yangu .
Katika kipengele hiki sitasahau huu wakati sababu hapa palitokea mambo mengi sana hata kuonekana mtu wa ajabu ajabu sana.
Siku moja mzee aliponijia aliniuliza iwapo nataka dada Aisha yaani dada yangu wamfungue macho aweze kuwaona na yeye, kwakuwa dada yangu nampenda sana basi nilikubali haraka haraka na kusema ndio .
Haikupita muda mrefu dada akawa ananambia mbona mwenzio siku hizi naona vitu vya ajabu ajabu au naota? Siku moja nilikuwa nyuma ya nyumba yetu karibu kabisa na ile miembe na ule mkuyu , dada alinifata ili tukanywe chai lakini ghafla alipokuja pale alianza kupiga kelele baada ya kuona kenge mkubwa sana yupo mbele yangu na sina hofu kabisa.
Alikuwa akimuita baba ndani na kaka zetu ili waje kumuua kenge , nilimkataza lakini hakusikia aliendelea kupiga kelele hadi watu wengine walianza kujaa, mmoja ya watu waliokuja nakumbuka ni baba mmoja aliyekuwa akiitwa omary kwasasa ni marehemu ( Mungu amlaze mahali pema amiin).
Watu walipokuja dada kwa kuwa alikuwa anaona macho yamefunguliwa basi akawa anasema kila kitu kuhusu kule kwenye muembe na mkuyu, nilipata hasira sana na wasiwasi mkubwa sana nikihofia kuwa sijui nitaeleza nini .
Basi yule kenge aliondoka pale na kupanda juu kabisa ya ule muembe wengine walikuwa hawaoni chochote ni mimi na dada tuu, na muda huu alikuwa amekaa tuu chini akipiga kelele kwa anayoyaona. Aliwaambia watu waliofika kuwa "huu muembe una mashetani wengi sana wamejazana hadi wengine wameenda kule kwenye mkuyu, wamevaa nguo nyeupe sana , wana ndevu nyingi na wengine ni watoto na vijana..." Dada alizidi kuongea.
Mzee Ruhaby siku ile hakuwepo lakini kulikuwa na mtumishi wake ambae nilimuona kule Iran na nilikuwa nae Yemen kwenye ile hospital yao, huyu mtumishi wa mzee Ruhaby alinambia kwa ishara kuwa niondoke pale .
Niliondoka pale kichwa kikiniuma sana pamoja na pua kwa hasira, nilichukia sana dada kukosa moyo wa kutunza siri, niliingia ndani na haikuchukua muda mrefu sana baba alikuja ndani nae ni kama alihisi kitu na kuniuliza hivi yule mzee wa msikitini ile ijumaa ulinambia ni nani ? hakuwa jini kweli yule ? mtoto wewe tangu kuzaliwa kwako ni vioja vioja tuu, tumboni umekaa miezi kumi na moja na wiki mbili sasa hapa napata hisia kuwa wewe una mawasiliano na uhusiano wa moja kwa moja na majini... baba aliongea kwa kunikazia macho .
Nilikuwa kimya tuu , nilisimama na kuingia chumbani nikafunga mlango kwa ndani nikaangalia ukutani mzee Ruhaby nikamuona (ni mfano wa kuwa natazama television) basi akawa anaongea nasikiliza kisha najibu
" Kijana wangu usiwe na hasira wala kuumiza akili yako muda wa familia yako kujua umefika haiwezekani kuficha kila siku, mimi nitakuja mwenyewe kumjibu baba yako maswali na mwisho nitajitambulisha, rudi alipo baba yako nitajitokeza kama mgeni ninaehitaji msaada muda sio mrefu sana..." mzee Ruhaby alisema.