MUENDELEZO WA SEHEMU YA NNE:
Basi nitarudi pale sebleni alipokuwa baba , na haikuchukua muda mlango wetu uligongwa.
Baba akanambia kuna mgeni huko , mimi nilishajua mgeni yule ni nani lakini nilinyamaza kimya kama sijui kitu chochote.
Baba alinyanyuka yeye mwenyewe kwenda kufungua mlango , baada ya salamu alimkaribisha ndani . Mzee Ruhaby na mimi tulitazamana macho kwa macho na haikuchukua muda mrefu akaanza mazungumzo yake na baba .
" Nilikuwa napita naenda pangani stahabu lakini nimevutiwa na ukimya wa hapa , ufanyaji wa ibada wa wakazi wa hapa lakini nilipata kusikia kuna mtoto mmoja hapa alipata kutumbukia kisimani sasa nimeona niingie hapa kuwajulia hali wakazi wa nyumba hii .." mzee Ruhaby alisema.
Lakini muda wote huu tangu aingie pale ndani kulikuwa na utulivu mkubwa sana kuliko kawaida na harufu ya manukato mazuri iliongezeka mbali na ubani ambao huwa tunafusha mara kwa mara harufu ya manukato iliongezeka.
Baba yangu yeye ni mkarimu sana na anapenda sana wageni na ilikuwa ni desturi ya pale nyumbani kuja wageni mbalimbali haswa waliokuwa wanakuja masjid kwaajili ya darsa mbalimbali, nafikiri yeye baba alijua mzee yule alitokea kule masjid na alipewa habari na sheikh Yusuf kumbe haikuwa hivyo.
Baba alivunja ukimya na yeye akasema nikweli mtoto mwenyewe ni huyu hapa ( nakumbuka alinishika kichwa hivi ) , akasema huyu bwana alitoka na wenzie zikaja habari kuwa amezama kisimani na mara akatoka.
" Lakini mambo ya watoto bwana sijui ametoka vipi ila huyu mtoto ana mambo ya ajabu ajabu leo yeye na dada yake wamenishangaza...." Baba alisema.
Mzee Ruhaby muda wote huu yeye hakujitambulisha hata kidogo lakini nilishangaa namna ambavyo baba yangu alimuamini ghafla sana na hata kuongea mambo mengi.
Lakini mada ikabadilka baada ya mzee Ruhaby kutoa kitabu kidogo na kumpa baba , kilikuwa kidogo dogo tuu na jalada lake ni kama ngozi hivii.
" Haya hii ni zawadi yangu kwako bwana utasomasoma ni kitabu changu hiki ila nakupa . Baba akavaa miwani yake na kusoma maandishi ya nje ya kitabu kisha akakiweka kando.
Baba ni kama alikuwa akiendeshwa fikra zake bila kujijua akawa anaongelea mada za majini tuu tena ghafla sana.
Saa saba kasoro kama dakika 23 hivi mzee Ruhaby akamwambia baba sasa mimi niruhusu nitoke niendelee na safari baada ya swala ya adhuhur nitafika pangani kule stahabu lakini huyu mtoto wako nimempenda sana ni mpole na mkimya muda wote huu hajasumbua hata kusema lolote msiwe mnamsema kwa hasira.
" Haya Ruhaby nilikuwepo sasa natoka" alisema.
Baba baada ya kusikia hili jina ni kama alishtuka hivi lakini alificha na badala yake alitoka nae nje na kumsindikiza.
Alirudi ndani na kunambia tujiandae twende zetu masjid lakini tulivyofika masjid mzee Ruhaby hakuwepo na baba ni kama alikuwa akiangalia huku na kule kama labda atamuona lakini hakumuona sababu hakuwepo.
Tuliswali na kumaliza na baada ya swalat adhuhur alimuita rafiki yake sheikh Yusuf na kumuuliza iwapo kuna ugeni wowote aliupokea pale masjid na kuwaelekeza nyumbani.
Lakini sheikh Yusuf alisema yeye hakupokea ugeni wowote, baba alishtuka tena kidogo ni kama machale yalianza kumcheza hivi sababu hakuwa mgeni sana na habari za ulimwengu wa majini .
" Sasa Yusuf swahiba wangu hivi Ruhaby ina maana gani? maana alikuja mzee pale nyumbani nikamkaribisha lakini sikupata kumuuliza jina maana sio vyema sana ila mwisho kabisa aliniaga na kusema kuwa yeye ni Ruhaby sasa alisema atapitia hapa masjid kisha anaenda stahabu pangani lakini sikumuona hapa " baba alisema.
Sheikh Yusuf aliposikia jina la eneo hili la stahabu pangani basi alimwambia baba moja kwa moja kuwa mzee yule hakuwa binaadamu ni jini sababu hapa stahabu pangani ni sehemu yenye makazi ya majini .
Baba alishtuka lakini hatukuwa na muda mrefu tukaondoka pale masjid, njia nzima baba alikuwa anarudia kusema tuu Ruhaby Ruhaby Ruhaby hili jina lina maana gani ? Mimi sikusema kitu chochote.
Kufika nyumbani nilivua kanzu yangu nikaenda jikoni dada na mama walipokuwa wakipika kwaajili ya kuchukua chakula . Na baada ya chakula baba yeye alihitaji kupumzika, na huko kwenye kupumzika ndiko alikojua ukweli baada ya kuota ndoto aliyoeleza baada ya kuamka.
Mimi nilikuwa ni mtu wa kukaa sana peke yangu haswa chumbani tuu na kila nikikaa peke yangu ndio huwa wanakuja sana viumbe na nawaona vizuri kabisa. Basi niliingia chumbani na kufunga mlango na kama kawaida nilipoangalia pale ukutani nilimuona mzee Ruhaby katika muonekano wa kuwa amekaa katika kiti na pembeni kuna fimbo na yupo na kitabu chake mkononi.
Lakini muda huu alikuwa akiongea kwa sauti ya chini chini tuu ila ya upole , ila nilimsikia vyema akisema sasa nimemchukua baba yako na kumtembeza kidogo kumzindua aelewe akiamka atakwambia kuna ndoto na atakuuliza mjibu usimfiche.
Haikuchukua muda aliondoka na ghafla niliskia mlango wangu wa chumbani ukigongwa mfululizo nilifungua mlango na baba aliingia pale chumbani.
Kiukweli ninao kaka zangu watatu lakini baba yangu yupo karibu sana na mimi na muda mwingi anapenda kuwa karibu na mimi na sio baba tuu hata mama pia.
Na umri wangu niliokuwa nao lakini baba alikuwa akiota kitu lazima aniulize nimpe tafsiri sijui kwanini lakini ndio ilivyo, mbali na baba hata watu wengine nilipokuwa Tanga huja na ndoto zao niwape maana .
Jambo hili lilimsukuma sana baba kunambia ndoto yake kama alivyonambia mzee Ruhaby kuwa baba ataota ndoto na kunambia
" Wee mswahili ( aliniita baba kwa utani ) bwana nimeota kitu sielewi kabisa, hivi yule mgeni aliyekuja inawezekana vipi nimuote kwa muda mfupi huu, au ndoto za mchana hizi ? Alisema.
Alinambia ndoto yake kuwa palikuja watu watatu vijana mmoja kati yao ni msichana, walimsalimia na kumwambia tumetumwa na baba tukuchukue tukupeleke nyumbani, walitoka nae na kupanda farasi mweupe mzuri sana na kuna sehemu walivuka bahari eneo kubwa sana lilikuwa na maji na majengo ya rangi nyeupe. walifika katika mji na kuuacha na kufata eneo la jangwa, hadi kwenye mti mkubwa wa mtende hapo wakamfunga farasi na kutembea hadi kwenye lango kubwa mfano wa geti na hapo walikuja watu wawili kuwapokea.
Mandhari yalikuwa mazuri sana ni mfano wa kasri la kifalme. Kuta za nyumba zilikuwa na rangi yenye kuwaka sana.
Pia aliona njiwa wengi weupe na hapo waliingia kwenye ukumbi mkubwa sana na kumuona mzee aliyekuwa amekaa katika kiti huku yupo na fimbo ndogo pembeni.
Hapa nikakumbuka safari yangu ya Iran nilikofanyiwa maulid nikagundua alikwenda pale nilipoenda mimi, yule mzee akamuuliza unanikumbuka? Mimi ni Ruhaby sultan na hapa ni Iran rejea maongezi yangu na wewe pale nilipokujia nyumbani kwako na kukupa kitabu .
Vitabu hivi vipo viwili tuu kimoja nimekupatia wewe na kingine kipo hapa , nimetuma watu wangu kukuleta hapa kukufungua uweze kujua ukweli.
Kwa muda mrefu nimekuwa swahiba na mtoto wako lakini muda haukuwa muafaka wewe kufahamu.
Hapa ni himaya yangu mimi ni sultan wa makazi ya hapa zaidi ya miaka mia tano nipo Iran na baba yangu alikuwa swahiba mkubwa wa babu wa mtoto wako . Baba yangu ni wa hapa Iran na mama yangu ni kutoka Oman.
Baba yako wewe alikuwa na uswahiba mkubwa na baba yangu na mimi nimefanya uswahiba na mtoto wako.
Hapo kwa mujibu wa baba alivyonieleza kuliletwa kitabu kikubwa cha ngozi kikafunuliwa na kumuona babu akiwa na mzee na aliona mandhari ya kigombe na boza pangani. Mbele yake ilisogezwa kitu kama pazia akawa anamuona baba yake yaani babu akiwa katika mazungumzo ya mara kwa mara na watu waliokuwa na mavazi ya kanzu na ndevu nyingi na vilemba kichwani.
Kwa mujibu wa maelezo yake baba aliona mti wa mbuyu na kisima kidogo pembeni na yalikuwa ni mandhari ya kigombe ni kando kabisa ya bahari ( na hili eneo hadi leo lipo na kisima kipo ) hapo aliona mara kwa mara pakifungwa farasi mweupe na akaambiwa farasi aliyempanda ndio yule anaemuona katika pazia lile anazaidi ya miaka 120.
ITAENDELEA
Naendea majukumu mengine ya hapa na pale thread hii ifatilie mtajifunza kitu : utulivu wenu na maswali yenye nia ya kujifunza utafanya niwaeleze mengi bila kuweka password