Pole sana
Aaliyyah
Kukataliwa kwa mara ya kwanza ndiyo chanzo cha haya yote. Na kukataliwa huko kuliambatana na jambo ambalo halikuwa na msingi wowote. Unaamini mlipaswa kuunganishwa na upendo baina yenu kuliko imani zenu. Kuachana kwenu kulichagizwa na mvutano wa nje, wala si maamuzi yenu binafsi.
Ukweli ni kuwa (hata kama utakataa hapa jukwaani), ulikuwa tayari kuufata upande wake ili kulinawirisha penzi lenu. Ukweli ni kuwa, hujapata mbadala wa kumpenda kama ambavyo ulimpenda mpenzi wako wa kwanza.
Hali hii inakuathiri na unapaswa kufanya yafuatayo;
1. Acha kufikiria kukataliwa kwa mchumba wako wa mara ya kwanza. Kubali kuwa, mmeachana na kamwe hamtokuwa pamoja.
2. Jiaminishe kuwa ndugu zako wana mapenzi mema zaidi kwako na wala hawakukataa kwa hila. Jikoleze kwa kufikiri kuwa familia inayojengwa kwa misingi ya imani mbili tofauti ina migogoro mingi. Aminisha nafsi yako kuwa imani yako ndiyo sahihi na nguzo katika ukuaji wa familia imara hapo mbeleni.
3. Usimlinganishe mpenzi wako wa sasa na aliyepita, vivyo hivyo kwa mapokeo ya nduguzo. Amini ya kuwa sasa huyu atapokelewa na hatua zaidi zitafuata.
4. Thubutu kumtambulisha mchumba wako wa sasa. Anza kwa rafiki zako kisha ndugu wa karibu kama kaka na dada. Sikilizia muitikio wao. Utakupa nguvu ya kumruhusu kwenda nyumbani. Zaidi, kubali wewe ukatambulishwe kwanza na hiyo itakupa msukumo wa wewe kumpeleka nyumbani.
5. Waza kuwa na familia. Jiaminishe ni wakati sahihi wa kuwa na mwenza na hata kupata watoto. Hii itakusukuma kuanza taratibu, kutambulisha ikitangulia.
6. Muombe Mungu kwa imani yako akupe wepesi na nguvu ya kuliendea jambo hili bila hofu yeyote.
7. Nikutakie kila la kheri na amini umeshafanikisha. Mungu akutangulie.