View attachment 3242826
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akimwapisha Suleiman Abubakar Mombo kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Ikulu ya Dar es Salaam , 11 Julai 2024.
I. USULI
Naandika dokezo la kisera, lenye kubeba taarifa za intelijensia ya kisiasa na kijasiriadola, kwa ajili ya kutetea rai ifuatayo:
Kwamba, kwa kuwa uhalifu wa kiuchaguzi unaowafanywa na wanasiasa matapeli wakati wa chaguzi zetu umekithiri kwa miaka 15 sasa kutokana na matobo ya kikatiba na kisheria, basi, tunapaswa kurekebisha ratiba ya uchaguzi mkuu wa 2025, kisha tufanye mageuzi ya kikatiba na kisheria, na hatimaye tufanye uchaguzi mkuu baadaye, na sio kinyume chake.
II. UTANGULIZI
Napendekeza kuanza dokezo hili kwa nukuu muhimu kuhusiana na mtazamo wa Chadema kuhusu Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika 2025.
"Mtu yeyote mwenye akili na macho ya kuona anajua kuwa chaguzi za nchi hii zimekuwa za hovyo sana na kwamba ni za hovyo kwa sababu mfumo mzima wa kiutawala wa nchi hii ni mfumo wa hovyo" -- Tundu lissu, Mwenyekiti CHADEMA.
“Hivyo, hatuzungumzii kususuia uchaguzi, hatutasusia bali tutaenda kuwaambia Watanzania, jumuiya ya kimataifa na walimwengu kwamba kama CCM na Serikali hawako tayari kufanya mabadiliko kwenye mfumo wa uchaguzi ili kuwepo chaguzi huru na haki, uchaguzi wa mwaka huu usifanyike kabisa” -- Tundu lissu, Mwenyekiti CHADEMA.
Huu ndio msimamo ulioibuliwa na Chadema kuhusu kile ambacho baadhi ya vyombo vya Habari, kama vile gazeti la Mwananchi la leo, vinakiita “Njiapanda ya Chadema Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2025.”
Lakini, napendekeza kwamba, kutokana na uzito wa hoja yenyewe, hasa tunapaswa kuwa tunaongelea “Njiapanda ya Watanzania Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2025.”
Kwa njia ya swali, “njiapanda” inayoongelewa kwenye vyombo vya habari, ndani na nje ya Chadema pia, inaweza kusomeka hivi:
Je, kwa kuzingatia uhalifu wa kiuchaguzi ambao umekuwa ukifanyika nchini Tanzania tangu 2010 kutokana na uwepo wa milima, mabonde na makorongo yaliyopo kwenye uwanja wa uchaguzi wa vyama vingi nchini Tanzania, tufumbe macho na kuendelea na utekelezaji wa ratiba ya uchaguz mkuu wa Oktoba 2025 au tusogeze ratiba hii mbele kidogo ili uchaguzi huu ufanyike baada ya mageuzi ya kikatiba na kisheria kufanyika ili kusawazisha milima, mabonde na makorongo yaliyopo?
Kutokana na utafiti nilioufanya, dokezo hili linapendekeza kwamba, tunapaswa kusogeza ratiba ya uchaguzi mkuu mbele kidogo ili uchaguzi huu ufanyike baada ya mageuzi ya kikatiba na kisheria kufanyika ili kusawazisha milima, mabonde na makorongo yaliyopo.
III. UTARATIBU WA UTAFITI (METHODOLOJIA)
Katika utafiti wangu nilikusudia kujibu maswali yafuatayo:
- Hoja ya Chadema kuhusu changamoto ya uhalifu wa kiuchaguzi nchini Tanzania inasema kitu gani kuhusu uwanja wa siasa za uchaguzi wa vyama vingi?
- Je, ni kweli kwamba kuna milima, mabonde na makorongo kwenye uwanja wa siasa za uchaguzi wa vyama vingi nchini Tanzania?
- Kama jawabu kwa swali la kwanza ni “ndiyo,” milima, mabonde na makorongo haya yamekuwa na madhara gani katika matokeo ya uchaguzi?
- Kutokana na majibu ya maswali haya mawili hapo juu, nah atua gani zichukuliwe tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.
IV. MATOKEO YA UTAFITI
Hoja ya Chadema
Maneno ya Tundu Lissu kuhusu msimamo wa kisera wa chama chake juu ya umuhimu na ulazima wa kusogeza mbele ratiba ya Uchaguzi Mkuu ujao yamenukuliwa hapo juu.
Kwa maoni yangu, haya ndio maneno yanayotueleza msimamo rasmi wa Chadema. Maneno haya yanaweza kufafanuliwa katika muundo wa hoja rasmi kama ifuatavyo:
1. Kama tungekuwa na mifumo ya kikatiba na kisheria inayowanyima wanasiasa matapeli fursa ya kufanya uhalifu wa kiuchaguzi kwenye michakaato ya chaguzi zetu basi tungekuwa na sababu nzuri ya kushiriki Uchaguzi Mkuu Ujao kabla ya kufanyika kwa mageuzi ya kimfumo.
2. Lakini, uzoefu wetu kutokana na chaguzi zote za 2010, 2015, 2019, 2020 na 2024 unaonyesha kwamba tunayo mifumo ya kikatiba na kisheria inayowapatia wanasiasa matapeli fursa ya kufanya uhalifu wa kiuchaguzi kwenye chaguzi zetu, kiasi kwamba, kwa kipindi cha miaka 15, tumekuwa tukiongozwa na serikali haramu zilizotokana na mbinu haramu.
3. Hivyo, bila kufanya mageuzi ya kuboresha mifumo ya kikatiba na kisheria inayowapatia wanasiasa matapeli fursa ya kufanya uhalifu wa kiuchaguzi kwenye chaguzi zetu hatuwezi kupata serikali halalai iliyotokana na mbinu halali.
4. Kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai, kama ilivyotafsiriwa kwenye Kesi ya Abdallah Zombe na wenzake 12, Kesi ya Mahakama Kuu Na. 26/2006, kuna njia tatu za mtu mmojawapo kushiriki katika kitendo cha uhalifu wa kiuchaguzi, kabla, wakati na baada ya mchakato wa uchaguzi:
- (a) Ama kwa mtu huyo kutekeleza uhalifu wa kiuchaguzi kwa kutumia mikono yake mwenyewe; au
- (b) kwa mtu huyo kumpa ushirikiano wa aina yoyote mtu baki mwenye nia ya kutenda uhalifu wa kiuchaguzi na hivyo kumsaidia mtu baki kufanikisha utekelezaji wa uhalifu; au
- (c) kwa mtu huyo kuficha taarifa muhimu zinazohitajika kwa ajili ya ama kuzuia uhalifu wa kiuchaguzi kutendeka au zinazoweza kusaidia kuwatia hatiani watu waliotenda uhalifu wa kiuchaguzi.
5. Hivyo, kama tunao wajibu wa kupigania ujio wa serikali halali iliyotokana na mbinu halali, basi, tunapaswa kupigania ujio wa serikali halali kwa kufanya yafuatayo:
- (a) Ama kujizuia na kumshawishi kila mtu baki kujizuia kutekeleza uhalifu wa kiuchaguzi kwa kutumia mikono yake mwenyewe; au
- (b) Kujizuia na kuwashawishi watu baki kujizuia kumpa ushirikiano wa aina yoyote mtu mwenye nia ya kutenda uhalifu wa kiuchaguzi na hivyo kumfanya mtu baki asifanikishe utekelezaji wa uhalifu; au
- (c) Kufichua taarifa muhimu zinazohitajika kwa ajili ya ama kuzuia uhalifu wa kiuchaguzi kutendeka au zinazoweza kusaidia kuwatia hatiani watu waliotenda uhalifu wa kiuchaguzi.
6. Kwa hakika, tunao wajibu wa kisheria na kimaadili wa kupigania ujio wa serikali halali, jambo linalomaanisha kwamba tunao wajibu wa kisheria na kimaadili wa kuzuia ujio wa serikali haramu, kwa sababu zifuatazo:
- (a) Kisheria, ibara ya 28(1) ya Katiba ya Tanzania (1977) inampa kila raia “wajibu wa kulinda, kuhifadhi na kudumisha uhuru, mamlaka, ardhi na umoja wa taifa.”
- (b) Kimaadili, sheria ya maadili asilia inatupa jukumu la kutekeleza matendo mema na kuzuia matendo maovu, kwa kuhakikisha kwamba, kisiasa, inasimikwa serikali iliyotokana na wapiga kura halali, inayofanya kazi kwa niaba ya watu wote, na yenye kutekeleza majukumu yake kwa faida ya watu wote.
7. Kwa hiyo, raia wa Tanzania tunao wajibu wa kupigania uchaguzi utakaofanikisha ujio wa serikali halali na kupinga uchaguzi utakaofanikisha ujio wa serikali haramu. Hii ndio mantiki ya kaulimbiu isemayo kwamba “Bila Kufanya Mageuzi Kwanza Hakuna Kufanya Uchaguzi,” yaani “No Reforms, No Elections.”
Kwa ujumla, ni wazi kwamba hitimisho hili lisemalo linawaweka njiapanda baadhi ya wanachama wa Chadema wanaotaka kugombea Udiwani, Ubunge na Urais kwa tiketi ya Chadema.
Pia, ni wazi kwamba vyama vingine vinaweza kuendelea na maandalizi ya uchaguzi, maana hii sio sera yao. Na wanachadema wanaopinga sera hii wanayo hiari ya kutafuta jukwaa jingine la kisiasa lisilotambua sera hii ili wapewe fursa ya udhamini wanaoutaka.
Milima, mabonde na makorongo ya kisiasa
Tuhuma kwamba chaguzi zote za 2010, 2015, 2019, 2020 na 2024 unaonyesha kuwa tunayo mifumo ya kikatiba na kisheria inayowapatia wanasiasa matapeli fursa ya kufanya uhalifu wa kiuchaguzi kwenye chaguzi zetu, kiasi kwamba, kwa kipindi cha miaka 15, tumekuwa tukiongozwa na serikali haramu zilizotokana na mbinu haramu, nazi zinao ushahidi wa kuziunga mkono kama ifuatavyo:
(a) Uchaguzi unaosimamiwa na ma-WEO, ma-DED, ma-DC, ma-DAS, na ma-RAS unakosa uhuru, uwazi na ushindani wa kweli, kwa sababu wao ni watumishi wa serikali ya chama tawala, na hivyo kufanya uhalifu wa kiuchaguzi kwa faida ya chama tawala.
(b) Sheria za uchaguzi zinawaruhusu Watumishi wa umma kuvaa kofia za Watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati w auchaguzi na hivyo kufungua milango ya uhalifu wa kiuchaguzi.
(c) Tume ya Taifa ya Uchaguzi imo kwapani mwa Rais wa nchi, ambaye ndiye huteua wajumbe wake, na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria pekee kwa sababu ya kuyumbishwa na maagizo kutoka Ikulu.
(d) Tume ya Taifa ya Uchaguzi haina uwezo wa kisheria wala kifedha wa kusimika watumishi wake kwenye kila jimbo la uchaguzi kwa mujibu wa sheria.
(e) Katiba inamruhusu Rais wa nchi aliye madarakani na ambaye ni mgombea kuendelea kutekeleza majukumu yake ya Urais wakati wa kampeni za uchaguzi ilihali yeye ni Amiri Jeshi Mkuu, Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, na Msimamizi Mkuu wa Jeshi la Polisi.
Jambo hili linafungua mianya kwa baadhi ya vyombo vya ulinzi na usalama, kama vile Jeshi la Polisi na TISS, kufanya uhalifu wa kiuchaguzi ili kumsaidia “bosi” wao kushinda.
(f) Katiba inaruhusu Rais wa nchi kushika nafasi ya mwenyekiti wa chama cha siasa, kabla na wakati wa uchaguzi, na hivyo, kufungua mlango wa Rais huyu kuvitumia vyombo vya ulinzi na usalama kwa faida ya chama tawala.
(g) Katiba na sheria zetu vinazuia matokeo ya uchaguzi wa Rais yanayobishaniwa kupingwa mahakamani kisheria. Hivyo, uhalifu wa kiuchaguzi kuhusiana na kura za urais hauwezi kukosolewa kimahakama.
(h) Sheria na Katiba havijapiga marufuku tabia ya uhalifu wa kiuchaguzi wa kugeuza mchakato wa uchaguzi kuwa mashindano ya kujaza fomu za wagombea, jambo ambalo linazalisha wagombea wa kupigiwa “kura za ndio au Hapana,” na hivyo kukiuka kanuni ya uchaguzi wenye ushindani.
Madhara ya milima, mabonde na makorongo haya
Makorongo haya kwenye uwanja wa siasa za vyama vingi yamekuwa na madhara ya kisiasa tangu zamani, hata kabla ya hayati Magufuli hajakanyaga Ikulu. Mfano:
(a) Mwaka 2010 na 2015 enzi za Kikwete
Katika zama hizi kulikwa na “vikosi kazi” vya kukomboa majimbo yaliyo hatarini.
Kwa kila jimbo ambalo tayari lilithibitika kuanguka mikononi mwa wapinzani, vikosi hivi vilikuwa vinashirikiana na baadhi ya ma-WEO, ma-DC, ma-DAS, ma-DED, ma-DSO, ma-OCD, ma-RSO, ma-RAS na ma-RC kufanya “ukombozi.”
Mfano mmoja ni ule wa Jimbo la Karagwe mwaka 2010. Mgombea wa CCM, Gosbert Blandes Begumisa, alipoteza jimbo hilo kwa tofauti ya kura zipatazo 500. Mgombea wa Chadema alishinda.
Kikosi kazi kikafika Karagwe haraka. Kiongozi wa kikosi kazi kile alikuwa ni Afisa Usalama aliyeitwa “Haule.” Wakachakachua takwimu Blandes akatangazwa mshindi.
Niliambiwa kuwa, Kila kikosi kilikuwa kinapewa magari, fedha taslimu na wakati mwingine helikopta. Na kwa kila jimbo lililokuwa linakombolewa “malipo ya kazi maalumn” yalikuwa fedha ipatayo TZS 100,000,000 (soma milioni mia moja).
Hivyo, wajumbe wa “vikosi kazi” hivi enzi za Kikwete walifanikiwa kujenga majumba, kununua magari, na kuanzisha biashara kubwa. Kwao, wakati wa msimu wa uchaguzi wajibu wao ulikuwa ni kuiba majimbo na ulikuwa ni msimu wa “mavuno” makubwa.
(b) Mwaka 2019 na 2020 enzi za Magufuli
Wakati wa JPM idadi ya “vikosi kazi” iliongezeka, kiasi kwamba uhalifu wa kiuchaguzi ikawa sera rasmi ya kila jimbo la uchaguzi. Ma-WEO, ma-DC, ma-DAS, ma-DED, ma-DSO, ma-OCD, ma-RSO, ma-RAS na ma-RC wote walipewa maagizo rasmi ya kusimamia ushindi wa wagombea wa CCM.
Uliotegemewa kuwa uchaguzi haali uligubikwa na uhalifu wa kiuchaguzi wenye sura zifuatazo:
- Kutoandikisha wapiga kura kwenye ngome za wapinzani,
- Kuwaengua wagombea wao wengi,
- Kutowaruhusu mawakala wa vyama vya upinzani na
- Kutowatangaza wapinzani hata pale walipoonekana kushinda.
Hatimaye wapinzani hawakuambulia kitu.
(c) Mwaka 2024 enzi za Samia Suluhu Hasan
Wakati wa SSH utaratbu wa hayati Magufuli ulifufuliwa na kutekelezwa kikamilifu. Ma-WEO, ma-DC, ma-DAS, ma-DED, ma-DSO, ma-OCD, ma-RSO, ma-RAS na ma-RC wote walipewa maagizo rasmi ya kusimamia ushind wa wagombea wa CCM. Wapinzani hawakuambulia kitu pia.
Kwa mara nyingine tena, uliotegemewa kuwa uchaguzi haali uligubikwa na uhalifu wa kiuchaguzi wenye sura zifuatazo:
- Kutoandikisha wapiga kura kwenye ngome za wapinzani,
- Kuwaengua wagombea wao wengi,
- Kutowaruhusu mawakala wa vyama vya upinzani na
- Kutowatangaza wapinzani hata pale walipoonekana kushinda.
Tena wapinzani hawakuambulia kitu.
View attachment 3242833
Jakaya Mrisho Kikwete
V. MAPENDEKEZO YA HATUA ZINAZOPASWA KUCHUKULIWA
Kutokana na yaliyojadiliwa hapo juu, napenda kutoa wito na mapendekezo yafuatayo kwa Serikali, Bunge, Makanisa, Misikiti, Azaki, Wanazuoni wa Vyuo Vikuu na watu wote wenye mapenzi mema kwa Tanzania:
1. Kwa kuwa Tanzania sio dola ya Kiimla, wala Himaya ya Kifamle wala Taifa la Kijeshi, bali ni Dola ambayo ni Jamhuri ya Kikatiba na Kidemokrasia, inayofuata demokrasia ya vyama vingi vya siasa tangu mwaka 1992;
2. Kwa kuwa, sifa kuu ya dola ambayo ni Jamhuri ya Kikatiba na Kidemokrasia ni uchaguzi unaofanyika kwa uhuru, uchaguzi unaofanyika kwa uwazi, uchaguzi unaofanyika kwa haki na uchaguzi unaofanyika kwa ushindani wa hoja za kisera;
3. Kwa kuwa chaguzi za 2019, 2020 na 2024 zilifanyika kwa njia ya udanganyifu ulioratibiwa na matapeli wa kisiasa waliokuwa wanafuata nyayo za Hayati JMP;
4. Kwa kuwa udanganyifu wa kisiasa katika chaguzi za 2019, 2020 na 2024 ulitekelezwa na ma-WEO, ma-DED, ma-DC, ma-DAS, ma-DAS na Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya sasa;
5. Kwa kuwa udanganyifu wa kisiasa ulifanikiwa kwa sababu ya uwepo wa mifumo mibovu ya kikatiba na kisheria;
6. Kwa kuwa sheria na Katiba ya sasa vinasabaisha kuwepo kwa uwanja wa uchaguzi usio tambarare bali uwanja wenye milima, mabonde na makorongo yanayowakandamiza wagombea wa vyama vya upinzani;
7. Na kwa kuwa serikali inayoingia madarakani kwa njia za udanganyifu inakuwa haina uhalali ikiwa ni sawa na serikali zilizokuwepo enzi wa ukoloni chini ya wazungu na serikali zilizokuwepo enzi za utumwa chini ya waarabu;
8. Hivyo basi, natoa wito kwamba, Serikali na Bunge vinapaswa kuandaa vikao maalum vya Bunge kwa ajili ya kupitisha Mabadiliko ya 15 ya Katiba ya Tanzania (1977) pamoja na marekebisho stahiki ya sheria za uchaguzi ili mambo yafuatayo yawezekane kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025:
(a) Sheria na Katiba vikataze ma-WEO, ma-DED, ma-DC, ma-DAS, ma-RAS kusimamia chaguzi.
(b) Sheria na Katiba vitamke kuwa chaguzi zote nchini zitasimamiwa na Watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyo huru.
(c) Tume ya Taifa ya Uchaguzi iondolewe kwapani mwa Rais wa nchi kusudi iweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria pekee bila kuyumbishwa na maagizo kutoka Ikulu.
(d) Tume ya Taifa ya Uchaguzi iweke watumishi wake kwenye kila jimbo la uchaguzi kwa mujibu wa sheria.
(e) Katiba ikataze Rais wa nchi aliye madarakani na ambaye ni mgombea kuendelea kutekeleza majukumu yake ya Urais wakati wa maandalizi na uendeshaji wa kampeni za uchaguzi.
(f) Katiba ikataze Rais wa nchi kushika nafasi ya mwenyekiti wa chama cha siasa.
(g) Katiba na sheria zetu viruhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais yanayobishaniwa kupingwa mahakamani kisheria.
(h) Sheria na Katiba vipige marufuku tabia ya udanganyifu wa kugeuza mchakato wa uchaguzi kugeuzwa mashindano ya kujaza fomu za wagombea.
(i) Rais Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, anayejua vizuri sana haya "mambo mambo" alisaidie Taifa kuondokana na hii Kero Sugu ya Uhalifu wa Kiuchaguzi, hata kama chama chake cha CCM kitangoka madarakani kwa sababu hiyo. Tanzania ni kubwa kuliko vyama vya siasa.
(j) Wanasheria wa Tanganyika Law Society watusaidie kuandaa miswada ya sheria zinazopaswa kuwasilishwa Bungeni muda wowote kwa ajili ya kutekeleza mapendekezo hapo juu. Tumechelewa sana, hivyo inabidi tukimbie.
VI. MAPINGAMIZI NA MAJIBU YAKE
Mapendekezo yangu hapo juu yanaweza kupingwa na watu kadhaa kwa njia mbalimbali. Baada ya mapingamizi ninayoyatarajia na ambayo nataka kuyajibu kabla hayajaibuka ni kama ifuatavyo:
Pingamizi: “Hoja ni nzuri, utafiti mzuri, ila sio realistic, kwa maana kuwa hayana uhalisia kama tukiangalia muda uliobaki. Tuachane na utopian politics”
Majibu: Naamini kuwa hoja yangu inatekelezeka kwa kuwa kazi ya kuandaa miswada kwa hati ya dharula inawezekana. Bajeti ya kuitisha Bunge maalum kwa ajili ya kupitisha miswada hiyo iko ndani ya uwezo wa serikali. Wabunge bado wapo maana Bunge halijavunjwa.
Pingamizi: “Uchaguzi is a process inayosimamiwa na serikali. Hakuuna siku serikali iliwahi kuahirisha uchaguzi mkuu kwa kuusogeza mbele kwa sababu ya kurekebisha jambo lolote.”
Majibu: Ukweli kwamba huko nyuma hatujawahi kufanya jambo Fulani hakumaanishi kuwa leo au kesho hatuwezi kufanya jambo hilo. Tukumbuke kuwa uchaguzi upo kwa ajili ya watu na sio watu kuwepo kwa ajili ya uchaguzi. Pia, ratiba ya uchaguzi sio msahafu.
Pingamizi: Tundu Lissu na Chadema yake hawana uwezo wala mamlaka ya kusema “no reforms no election” na kauli yake ikatekelezwa na serikali. Kwa hiyo, hakuna mageuzi yoyote na uchaguzi utafanyika.
Majibu: Mawazo hayo yana-personalise hoja yangu. Lissu ameanzisha hoja. Mie nimejielekeza kwenye hoja na kumweka pembeni. Tujiepushe na tatizo hilo la ARGUMENTUM AD HOMINEM. Yaani tutofautishe hoja na mleta hoja. Tufikirie juu ya uwezekano kwamba hoja ni nzuri, serikali itaweza kuipenda, Bunge litaweza kuichagamkia. Let us think positively. Namna hiyo, tutakuwa na mchango ambao sio biased sana.
Nawasilisha.