Katiba ya Tanzania ibara ya 66
66. Wabunge Sheria Na. 15 ya 1984 ib. 13; 4 ya 1992 ib. 18; 12 ya 1995 ib. 9; 3 ya 2000 ib. 9
(1) Bila ya kuathiri masharti mengine ya ibara hii, kutakuwa na aina zifuatazo za Wabunge, yaani–
(a) Wabunge waliochaguliwa kuwakilisha majimbo ya uchaguzi;
(b) Wabunge wanawake wa idadi inayoongezeka, kuanzia asilimia ishirini ya Wabunge waliotajwa katika aya ya (a), (c) na (d), itakayotajwa mara kwa mara na Tume ya Uchaguzi kwa taarifa itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali baada ya kupata kibali cha Rais, watakaochaguliwa na vyama vya siasa vinavyowakilishwa Bungeni, kwa mujibu wa ibara ya 78, na kwa kuzingatia masharti ya uwiano wa uwakilishi baina ya vyama hivyo;
(c) Wabunge watano waliochaguliwa na Baraza la Wawakilishi kutoka miongoni mwa wajumbe wake;
(d) Mwanasheria Mkuu;
(e) Wabunge wasiozidi kumi walioteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa kwa mujibu wa ibara ya 67, isipokuwa sifa iliyotajwa katika ibara ya 67(1)(b).
(2) Rais, Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar, kila mmojawao hatakuwa Mbunge.
(3) Endapo Mkuu wa Mkoa atachaguliwa kuwa Mbunge anayewakilisha wilaya ya uchaguzi au endapo Mbunge anayewakilisha wilaya ya uchaguzi atateuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa, Bunge litahesabiwa kuwa lina idadi ya Wabunge inayohitajika na shughuli zake zitakuwa halali ingawaje idadi ya jumla ya kawaida ya Wabunge kwa mujibu wa masharti ya ibara hii, itakuwa imepungua kutokana na uchaguzi huo wa Mkuu wa Mkoa au uteuzi huo wa Mbunge anayewakilisha wilaya ya uchaguzi.