NAMNA YA KUJUA HADITHI ILIYO SAHIHI NA ILIYO DHAIFU.
Ndugu msomaji tumeulizwa swali na ndugu yetu Hamza M Mikana katika comment za madarsa yetu lakini kutokana kuzuka gogoro hasa kwa wale wapenzi wa kutumia hadithi dhaifu mpaka huulizwa maswali yasiyo tarajiwa kuuliza mtu anaejinasibisha kuwa yeye ni msomi.
Kwa faida ya wote tunaleta tena somo hili kwenu ili ifahamike kinacho sababisha hadithi kuwa sahihi au kuwa dhaifu.
Kigezo cha hadithi kuwa sahihi ni kupatikana masharti matano yafuatayo.
Hata hivyo wapo wanaohoji juu ya kanuni hii, je kuna dalili juu ya vigezo hivyo vitano? Jibu vigezo vyote vimeendana na dalili kama ifuatavyo.
الحديث الصحيح.
وهو ما اتصل سنده بنقل العدل، الضابط عن مثله ولم يكن شاذاً ولا مُعللاً،
(a) Sharti la kwanza ni kuungana Sanadi, mpokezi iwe kweli kapokea kwa mtu anae mtaja ili asimulie kilekile alicho kipokea kwake ili kulinda ukweli, Qurani inatutaka tuwe wakweli.
Dalili juu ya hilo.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَكُونُوا مَعَ الصَّادِقِين.
Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kuweni pamoja na wakweli ( Attawbah 119)
(b)Pili mpokezi awe ni mtu muadilifu,Qurani inatutaka tuwe waadilifu.
Dalili juu ya hilo.
اعْدِلُوا هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ ۖ وَاتَّقُوا اللَّهَ ۚ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُون.َ
Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchamungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda (Maidah 8).
(c)Tatu mpokezi anatakiwa kuhifadhi hadithi ima kifuani au kuandika, Qurani inatutaka kuhifadhi mambo na inapobidi kuandika ili kutunza kumbukumbu.
Dalili juu ya hilo.
وَلَا تَسْأَمُوا أَنْ تَكْتُبُوهُ صَغِيرًا أَوْ كَبِيرًا إِلَىٰ أَجَلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ أَقْسَطُ عِنْدَ اللَّهِ وَأَقْوَمُ لِلشَّهَادَةِ .
Wala msipuuze kuliandika deni likiwa dogo au kubwa mpaka muda wake. Hayo ndiyo haki zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu, na ndiyo sawa zaidi kwa ushahidi (Albaqarah 282)
(d)Nne Mpokezi anatakiwa asitofautiane na aliye mtangulia, Qurani inatutaka kutunza amana kama tulivyo ipokea bila ya kubadilisha chochote maana hadithi ni amana zifikishwe kwa walengwa kama zilivyo simuliwana Mtume swalla llaahu alayhi wasallama, hivyo mpokezi yatakiwa aisimulie kama alivyo ipokea.
Dalili juu ya hilo.
إِنَّ اللَّهَ يَأْمُرُكُمْ أَنْ تُؤَدُّوا الْأَمَانَاتِ إِلَىٰ أَهْلِهَا
Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe (Annisaai 48).
(e)Tano isipatikane hila kwa mpokezi kama tabia ya kusahau au uzee sana au utoto sana, au ugonjwa wa akili ikawa ni sababu ya kupoteza kumbukumbu.
Dalili juu ya hilo.
عن عائشة عن النبي صلى الله عليه وسلم قال : رفع القلم عن ثلاث عن النائم حتى يستيقظ وعن الصغير حتى يكبر وعن المجنونحتى يعقل.( النسائي :3432)
Amesimulia mama Aisha, kutoka kwa Mtume swalla llaahu alayhi wasallama, lmeinuliwa kalamu kwa watu watatu, Aliye lala mpaka atakapo amka, Mtoto mdogo mpaka akikua, Na mwendawazimu mpaka akipona (Anasaai 3432).
Hizo ni shuruti za kuwa hadithi ni sahihi na zote zimeendana na Qurani na Sunna.
VIGEZO VYA HADITHI KUWA NI DHAIFU.
الحديثالضعيف.
وهو ما لم يجتمع فيه شروطالصحيح ولا شروط الحسن.
Hadithi dhaifu wakasema ni kuwa kinyume chake vigezo vya hadithi sahihi kama ifuatavyo.
(a)Kutokuwepo muunganiko wa sanadi ikawa mtu anasimulia kutoka kwa fulani hali ya kuwa huyo anaemtaja hakupokea kwake au hawakuwahi kuonana kabisa.
(b) Kukosekana uadilifu kwa mpokezi akawa siyo mtu mwenye kuaminika katika jamii.
(c) Mpokezi kukosa sifa ya kuhifadhi hadithi iwe kifuani au kuandika.
(d)Mpokezi kutofautiana na aliye mtangulia kuipokea hadithi hiyo.
(e) Mpokezi kuwa na hila itakayo mpelekea kuto aminika kuhifadhi kwake, kama kuwa msahaulifu au kuugua kichaa n.k.