Pasco umechanganya mambo kuhusu mfumo au utaratibu wa majina. Kwa sehemu kubwa duniani kuna mifumo miwili ya majina, kuna huu wa nchi za magharibi ambao kutokana na ukoloni ndiyo na sisi tumeurithi na upo wa nchi za mashariki. Huu wa magharibi huwa unaanza na "first name" au kama ukipenda "forename" halafu ukimalizia na "surname" yaani jina la ukoo. Unaweza pia kuwa na jina au majina ya kati "middle name/s". Mfano ni Juma Maharage au Juma Pasco Maharage.
Ule wa mashariki huanza na jina la ukoo halafu likaja la kwako au pengine ukawa na jina la kati. Mfano Wachina; ukisikia anaitwa Xi Jinping basi ujue "Xi" siyo first name bali ndiyo jina la ukoo halafu "Jinping" ndiyo la kwake. Kwa maana nyingine kama Juma Maharage angekuwa Mchina basi angeitwa "Maharage Juma".
Sasa basi utaratibu sahihi hata kwa hapa kwetu kwa mfano ni mtu kuitwa jina lolote la kwanza (first name) au hata la kati (middle name) kama wazazi wake watakavyopenda ila jina la ukoo (surname) linabaki lile lile ambalo linatumika kifamilia. Hili linatakiwa liwe la "kilugha" sababu hakuna ukoo wa Kitanzania au Kiafrika wenye jina la kizungu, yote yanapaswa kuwa ya kikwetu.
Kuna utaratibu mbovu hapa kwetu ambapo mtu anayeitwa kwa mfano "Steven Paul Mkama" anazaa mtoto halafu badala ya kumuita mfano "Judith Mkama" au "Judith Roselyn Mkama" utasikia anamuita "Judith Steven" au "Judith Steven Mkama".
Haya ni makosa maarufu sana. Kwa mfano huu, huyu mtoto ni Judith Roselyn, hayo ndiyo majina yake sahihi. Jina pekee analoazima ni "Mkama" ambalo ni la ukoo. "Steven" na "Paul" hapaswi kabisa kuyatumia kwa sababu haya ni "personal names" za baba yake kama vile yeye alivyo na personal names zake mbili yaani Judith Roselyn. Atakapokuwa anatumia personal name yoyote ya baba yake tayari anapoteza huo ukoo. Hili tatizo linajitokeza mara nyingi mno hapa Tanzania.
Kuhusu "nicknames", haya ni majina ya utani ambayo hayachukuliwi kuwa rasmi, mfano yule beki wa Yanga anayeitwa "Canavarro", hakuna mtu yeyote anayeamini kwamba hilo ndiyo jina lake na wala hawezi kulitumia "officially" popote. Yapo pia majina yanayoitwa "stage names" ambayo hutumiwa sana na wanamuziki au wacheza sinema na wengine huamua kuyatumia rasmi kisheria kama majina yao. Mfano mwanamuziki maarufu wa Uingereza anayefahamika kama "Elton John" jina hili ni stage name ambayo amelirasimisha. Majina yake ya kuzaliwa ni Reginald Kenneth Dwight.
Kwa leo niishie hapa.