Uwajibikaji unaooneshwa wakati wa Mwenge unapopita uwe Utamaduni wa Viongozi wetu Kila Siku

Uwajibikaji unaooneshwa wakati wa Mwenge unapopita uwe Utamaduni wa Viongozi wetu Kila Siku

DogoWaNjombe

JF-Expert Member
Joined
Feb 7, 2022
Posts
3,284
Reaction score
7,708
Kwa takribani miaka saba sasa nimekuwa nikifuatilia kwa karibu masuala ya Kijamii na Kisiasa nchini, nimejikuta nikijiuliza swali moja ambalo hadi leo halijapatiwa majibu ya kuridhisha.

Nimewahi pia kuwauliza baadhi ya watu walioko karibu nami, lakini hata wao walionekana kuwa na mashaka au kutoelewa vyema chanzo au muktadha wa jambo hili.

Mara kwa mara, ninaposhuhudia Mwenge wa Uhuru ukipita katika maeneo mbalimbali ya nchi, kuna jambo moja hujirudia miundombinu hukarabatiwa kwa kasi ya ajabu, miradi hufanyiwa ukamilishaji kwa dharura, barabara hutengenezwa usiku na mchana.

Mara nyingi, haya yote hufanyika kwa lengo la kuandaa mazingira ya uzinduzi wa miradi inayopaswa kukaguliwa au kuzinduliwa na Mwenge huo.
photo_2025-06-04_10-05-59.jpg

photo_2025-06-04_10-05-58.jpg

photo_2025-06-04_10-05-54.jpg
Kinachonishangaza ni kwamba kiwango hiki cha uwajibikaji na kasi ya utekelezaji huwa hakionekani katika kipindi kingine chochote cha mwaka, isipokuwa tu pale ambapo Mwenge unatarajiwa kupita.

Kwa mfano, katika mtaa ninakoishi, niliposikia kuwa Mwenge utapita kuzindua kisima cha maji na vyumba vya madarasa, ghafla tulishuhudia greda likisafisha barabara mchana na usiku, mafundi wakikesha eneo la mradi, na viongozi wakiwa karibu kusimamia kila hatua.

Hili linanifanya kujiuliza: Je, kuna bajeti maalumu inayotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hii kwa haraka wakati wa Mwenge? Na kama hakuna, kwa nini jitihada kama hizi hazifanyiki wakati wote hata bila Mwenge?

Kwa mtazamo wangu, kiwango cha uwajibikaji kinachoonekana wakati wa maandalizi ya Mwenge kinapaswa kuwa sehemu ya utamaduni wetu wa kila siku, na siyo tukio la msimu. Kama jitihada na ufuatiliaji kama huu zingekuwa endelevu, huenda changamoto nyingi za miradi kusuasua zisingekuwepo.

Ni dhahiri kuwa inawezekana kwani tunakiona kila mwaka lakini kinachokosekana ni nia ya dhati na msukumo wa kudumu wa ufuatiliaji na usimamizi.
photo_2025-06-04_10-05-53.jpg
Kwa hiyo, ni rai yangu kuwa tuchukulie kwa uzito uwajibikaji unaoshuhudiwa kipindi cha Mwenge kama chachu ya kuleta mabadiliko ya kweli ambayo hayategemei tukio au msimu, bali yanakuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku hasa kwa viongozi wetu na mamlaka mbalimbali.
 
Back
Top Bottom