Unamsikia mtu anasema uzalendo utazidi ikiwa tutasimama na wahisani kuwashawishi kuzuia fedha yao hadi masharti ya utu yatimie?
Hivi Mugabe anaongoza kwa wingi wa wazalendo au wizi wa kura? Akiwa na uchaguzi halali unafikiri uzalendo wa Wazimba utamsaidia kubaki kwake kwa sababu ya kuzuiwa kwa fedha ya mkoloni?
Uganda jee?
Ikiwa uchaguzi wa haki utafanyika huyu mzalendo wao atashinda? Kule Zambia jee? Tunahalalisha hadithi za kupanga panga. Hivi kati ya uonevu uliovuka mpaka na kilio cha kuzuiwa misaada kipi hasa kitachozuia uzalendo.
Yaani tunapanga panga hadithi kama tuko katika vita ya baridi katika karne hii. Ukoloni ulishamaliza hizi sentiments za kuwatusi wazungu tukiwa ndani lakini wapenzi wakubwa tukiwa nje ndio ninaouona upuuzi mkubwa zaidi.
Madikteta dunia hawana wingi wa wazalendo kwa sababu ya kuzuiwa misaada. Uzalendo wanaojaribu kutuonyesha ni uzalendo feki unaosukumwa tu na khofu ya bunduki, mizinga na roketi hakukosa kibatari na kauli zake. Firauni hakuangamizwa kwa sababu ya maendeleo bali kukosa utu, kuonea wanyonge na kujifanya Mungu mtu.
Hakuna aliepewa laana za Mungu kwa kupinga maendeleo yasio na utu bali walioangamia wengi ni wanafiki, wadhulumaji na waliosimama katika mabaya kwa wanyonge. Yesu hakusimama kuzuia maendeleo yasio na utu? Kwa nini tulidai uhuru wakati mzungu alijenga na kuhakikisha maendeleo yanakuwa japo kibaguzi na bila ya utu?
Unajuwa hata Iddi Amini nae akituaminisha anawazalendo kwa sababu za kupanga kama hizi?
Botha wa Afrika Kusini nae halkadhalika akiamini uzalendo kuzidi kila akibanwa.
Uzalendo unao "encouraged" kupindwa kwa utu, kudidimizwa kwa haki na kuzimwa kwa demokrasia ni sawa na uchifu wa kuwauza wananchi katika utumwa kwa sababu za kuwa ni shida katika tawala zao.
Na iweje tuwapigie makofi wazungu wanaouona ubaya unaotendeka lakini wakaendelea kuzisaidia kwa hali na mali tawala katili duniani?
Si ndipo tunaposimama na kuwalaumu kuwa ndio sababu ya kudumu kwa ukatili na uongozi wa ghilba barani Afrika na ukoloni mambo leo.
Hivi tunadhani misaada hii inapotolewa katika mazingira yasiojali utu, demokrasia na haki kweli ni misaada ya maslahi nasi au watoaji? Makatili wakubwa duniani walidumu kwa sababu gani kama si misaada iliokuza ubeberu, ubabe na tawala za khofu?
Wazalendo walijengwa Ujarumani katika misingi hii ya taifa langu kwanza halikosei na matokeo yake ubaguzi ukawa ni maisha ya kawaida na mauaji ya kibaguzi yakipewa daraja ya utukufu.
Uzalendo usiohoji utu, haki, usawa na heshima ya kuishi mwananchi kwa sheria na uhuru wake ni uhuni tu usio na chembe ya insaf.
Maendeleo gani yenye manufaa na wananchi ikiwa haki, uhuru na heshima ya kuishi kwa kulindwa na sheria na utu ukiwa haupo?
Yaani ukiwachie kizazi chako urithi wa kukubali aonewe, anyimwe haki na kuishi kwa muono wa mzizi mkuu ilimradi tu kuna maendeleo?