4. MWALIMU WA MA-NGULI
Kwa vipindi tofauti Mabala amefundisha kwenye shule na vyuo mbalimbali nchini. Baadhi ya shule na vyuo alivyofundisha ni Mirambo, Mzumbe, Korogwe, vyuo vya ualimu Chang’ombe na Marangu. Pia amewahi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1973 na 1993. Mabala analikumbuka zaidi darasa lake la kwanza la Shule ya sekondari ya Wavulana Mirambo ambalo lilikuwa na wanafunzi ambao sasa ni wanasiasa na wanazuoni nguli.
Baadhi yao ni Marehemu Profesa Jwani Mwaikusa, Mwanazuoni wa Sheria aliyebobea na Wakili katika Mahakama ya Kimataifa Maalum ya Mashtaka ya Jinai juu ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda, ICTR, iliyoko Arusha, Profesa Abdallah Njozi, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro na Mwanafasihi Mbobezi wa Lugha ya Kingereza na Dk Harrison Mwakyembe, Waziri wa Uchukuzi.