HII ARTICLE NIMEIKUTA MAHALI UKIPATA MUDA IPITIE ITAKUSAIDIA
!
!
ATHARI ZA KUCHANGANYA DAWA ZA HOSPITALI NA MITI SHAMBA/TIBA MBADALA.....
Watu wanaougua magonjwa sugu wamekuwa wakijikuta kwenye mkanganyo kiasi cha kuwafanya watumie dawa za hospitalini pamoja na zile za asili bila kujua athari mbaya zaidi zitakazowapata.
Matumizi ya dawa za asili au tiba mbadala kwa sasa yameenea sana. Za asili zinajizolea umaarufu sehemu mbalimbali duniani kutokana na kupigiwa debe muda mwingi.
Sheria za kimataifa zinapiga marufuku dawa za hospitalini kutangazwa kwa sababu mwenye mamlaka ya kuamua matumizi ni daktari na wala si mgonjwa.
Dawa za hospitalini hadi ziidhinishwe kwa matumizi ni lazima zipitie hatua mbalimbali kuthibitisha viwango vya kutibu, faida na hasara.
Dawa za asili zimekuwa zikitumika ama kutokana na mazoea au mgunduzi kuzitangaza wakati athari zake zinazotokana na kiwango cha sumu kilichopo kutokujulikana.
Pamoja na hali hiyo, jambo la hatari zaidi ni watu wengi kuchanganya dawa hizi za asili na zile zinazotengenezwa maalumu kutolewa hospitalini.
Wagonjwa wengi hasa wenye magonjwa sugu yanayoelekea kushindikana hospitalini wanatumia tiba za asili kubahatisha uwezekano wa kupona. Wengine kwa kutokujiamini hujikuta wanaenda hospitali kupata dawa na wakati huo huo huenda kwa waganga wa jadi kupata huduma.
Wengine wanapokwenda kuonana na madaktari, huwa hawako tayari kuweka wazi kwamba wanatumia dawa nyingine za asili.
Kuna baadhi ya waganga wa jadi, kwa tamaa zao huwa wanawaambia wateja wao kuwa dawa zao haziwezi kuingiliana na zile za hospitali kwa kuwa ni kama chakula tu. Ukweli ni kwamba nyingi zina sumu.
Taarifa nyingi za kitabibu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa wapo watu wengi wanaochanganya dawa hizi na kujikuta wanatengeneza tatizo jingine ambalo pengine ni kubwa zaidi ya lile linalowasibu.
Katika utafiti huo, inaonekana kwamba madhara ya mwingiliano ama ukinzani wa dawa za asili na zile za kisasa, linaongezeka.
Hata hivyo, taarifa hizi zinaweza kuwa hazitoi picha kamili kwa vile takribani asilimia 70 ya wagonjwa walioathirika, hawaelezi ukweli wa kuchanganya dawa.
Kwa sababu hiyo hakuna utaratibu maalumu wa kuweka takwimu ili kufuatilia ukubwa wa tatizo hilo.
Dk Shufeng ZHOU aliandika makala kwenye jarida la ‘Herbal Medicine & Drug Interactions’ nchini Singapore, toleo la 6, akielezea juu ya utafiti wa matumizi mchanganyiko wa dawa za asili na zile za hospitalini.
Dk Zhou anasema matumizi ya namna hiyo yanaweza kusababisha mwingiliano au ukinzani wa dawa na kusababisha madhara makubwa kwa mtumiaji.
Matumizi ya namna hii yanaweza kuzuia dawa moja isifanye kazi, au moja iwe na nguvu zaidi kuliko kawaida na kudhuru mwili.
Dawa zote zinaweza kujishikiza katika vipokeleo vya dawa vya aina moja na kushindana au kuzuia uzalishaji wa vimeng’enyo vya mwili visisafirishe dawa mwilini kama inavyotakiwa.
Hali ya namna hii inaweza kusababisha usugu wa viini vya magonjwa hatari dhidi ya dawa mfano Viini vya Kifua Kikuu (TB), Virusi Vya Ukimwi (VVU), au kudhurika kwa ini na figo na kusababisha viungo hivi vya mwili, kushindwa kufanya kazi zake vizuri.
Wakati mwingine mwingiliano kinzani wa kiutendaji wa dawa za asili na zile za hospitalini, unaweza kusababisha dawa kugeuka kuwa sumu na kusababisha mzio hatari wa kuzimia na kushindwa kupumua.
Hatari ya mwingiliano kinzani wa utendaji wa dawa, huwa mkubwa zaidi pale dawa zaidi ya moja zinapotumiwa kwa pamoja.
Mtafiti mmoja wa maswala ya dawa anasema kuwa, mtu anapotumia dawa mbili kwa wakati mmoja, hatari ya mwingiliano kinzani ni asilimia 6. Anapotumia aina tano za dawa mwingiliano ni asilimia 50 na hatari huongezeka zaidi hadi kufikia asilimia 100 pale mtu anapochanganya dawa nane au zaidi.
Hii ni kwa mujibu wa Kuhn Merrily, katika kitabu chake cha “Pharmacotherapeutics: A Nursing Process Approach. Philadelphia, Pa: FA Davis, 1998”.
Dawa zinapoingiliana kiutendaji, hutengeneza mazingira yasiyofaa katika tumbo la chakula na utumbo, kiasi kwamba sehemu hizi za mwili hushindwa kufanya kazi ipasavyo.
Matokeo yake ni kuharisha, kupata kichefuchefu au kupata vidonda vya tumbo au mwili kushindwa hufyonza kiasi cha kutosha cha dawa kwa ajili ya kupambana na ugonjwa. Mfano mzuri ni pale mtu anapotumia aloe vera na dawa za hospitalini kwa wakati mmoja anaweza kuharisha.
Pia mwingiliano kinzani unaweza kusababisha dawa kujishikiza katika vipokeleo visivyo vya kawaida na kushindwa kusambaa kama inavyotarajiwa.
Tatizo jingine hutokea wakati dawa zilizoingiliana kiutendaji zinapofika ndani ya ini. Hapo dawa huathiri vimeng’enywa vya ini vinavyoshughulikia dawa, vijulikanavyo kama
CYP 450 enzymes na P-glycoprotein . Hali hii huweza kupunguza au kuongeza makali ya dawa kwa namna isiyokuwa ya kawaida.
Hatari haiishii hapo, dawa zinapoingiliana kiutendaji pia huathiri utendaji wa figo na kushindwa kuondosha kiasi kikubwa cha sumu hatari mwilini.
Hali hii inaweza kudhuru figo na kusababisha kiungo hicho muhimu kufa au kuwa dhaifu kiutendaji.