WEWE NI WA PEKEE. Hivi unajua kwamba, tangu kuumbwa kwa dunia, kati ya mabilioni ya watu waliopita na wajao, hajawahi kutokea na hatotokea mtu kama ulivyo WEWE? Kati ya wote waliopata kuishi juu ya mgongo wa ardhi au watakaokuja kuishi, hayuko mwenye mjumuiko wa vipaji, mwonekano, uwezo, huzuni, marafiki, furaha, maadui na fursa kama ulivyo WEWE. Kama ukuaji wa nywele zako tu, haufanani na wa yeyote; kama alama za vidole (fingerprints) vyako tu hazishabihiani na za yeyote, unashangaa nini kwamba hakuna kama WEWE? Hakuna mwenye siri n dhahiri sawasawa na zako, wala hayuko anayepitia mapito ya kifamilia na kijamii kama WEWE. Baadhi ya wapuuzi wachache wanaokucheka kwa kufanya mambo tofauti na wanavyotaka, wameshindwa kujua kwamba WEWE siyo wao. Acha wakucheke, acha wakununie; duniani hayuko anayependwa na watu walewale wanaokupenda WEWE, na akachukiwa na walewale wasiokupenda WEWE; hayupo, hajapata kuwapo na hatotokea. Sasa, thamini na furahia huo upekee; ni tunu Maanani aliyokutunukia, zawadi kwa ajili yako wewe tu. Haupaswi kuigiza maisha kwa kuongea, kutembea, kuimba, kucheza au kufanya lolote ili tu uonekane kama fulani. Haukuletwa duniani kuja kuwa kama fulani; ndo maana ukaumbwa tofauti na huyo unayetaabika kujifananisha naye. Hakuna popote katika kumbukumbu ya dunia, vitu vilevile unavyowaza na kuvifanya wewe, vikazunguka katika mtindo huohuo, kichwani kwa mwingine. Hakuna anayeweza kufungamana na jamii kwa namna hiyo hiyo unayofungamana nayo WEWE. Hayuko awezaye kuyazungumza maneno yako. Hakuna awezaye kustarehe kwa kiwango kilekile unachostaladhi wewe uwapo stareheni. Hakuna awezaye kuuchukua ufahamu wako na kuupandikiza kwa mwingine. Hakuna anayeweza kuwa na wivu na hasira kama vilivyo kwako. Wewe ni wewe tu. Kama utautumia vema upekee ulionao, katika kuyaenenda mambo yako, hakika utapaa katika kilele cha ubora. Kama unaimba, usijifananishe na Diamond; kama unacheza ndondi, usijifananishe na Mike Tyson; kama unaandika, usijifananishe na Shaaban Robert; kama wewe ni mtangazaji, halafu unajiigiza kwa Masoud Kipanya, si ni bora nizime idhaa unayotangaza - nikamsikilize huyo Kipanya mwenyewe? Itoshe tu kujifunza toka kwao ili kuuboresha upekee ulionao.