Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Ufafanuzi yakinifu; maana halisi ya biashara haiishii kwenye kununua na kuuza bidhaa. Biashara ni kitendo cha kutoa huduma yenye kuhitajika sana kwa jamii. Maana yake hata kama huna mtaji wa pesa, ukajitolea kuamka asubuhi kisha ukaenda kufanya usafi wa kukata majani na kuondoa takataka kwenye majumba ya watu, ni lazima watakulipa. Ninachomaanisha hapa ni kuangalia tatizo ambalo limekuwa ni kero kwa jamii unayoishi na kutafuta namna ya kuliondoa.
 
Katika ugumu wowote wa uchumi, wakati ambapo wengi wanakiri na kulalamika pesa kukata mifukoni mwao, wewe umiza zaidi akili kutoa huduma ambayo hata kama mtu ana pesa kidogo ni lazima apate huduma yako.
 
Ngoja nifafanue kwa mfano halisi. Pengine mtaani kwako kumejaa maduka yanayouza maji ya kunywa, kuanzia shilingi 600 na kuendelea, lakini ukitazama wakazi wengi wa eneo hilo uwezo wao wa kununua maji kwa bei hiyo zaidi ya mara moja ni mgumu na wewe unajua kabisa kuna maji ya bomba ambayo hayana chumvi mahali fulani, kwa nini usiyachukue maji hayo na kuyaweka kwenye vyombo maalum kama chupa safi na kuyaweka kwenye friji ambapo unakuwa unauza kwa shilingi 200?
 
Huoni kama utakuwa unatengeneza nafasi ya kujipatia pesa? Ninasisitiza uumize akili kupata wazo bora la biashara ambayo iko kwenye kundi la mahitaji ya lazima ya kila siku ya watu.
 
Kabla sijamalizana na kipengele hiki, ninataka nikupe mfano mmoja mfupi wa msichana ambaye alilazimika kuachana na masomo ya shule ya msingi kwa sababu ya wazazi wake kukosa uwezo wa kumsomesha na wakati huo bibi yake alikuwa mgonjwa wa kansa hivyo pesa kidogo iliyopatikana kwa familia iliishia kwenye chakula na matibabu ya mgonjwa.
 
Ni katika kipindi ambacho yuko nyumbani, binti huyo akawa anamhudumia bibi yake kwa mahitaji yote. Kadiri siku zilivyosonga ndivyo alijikuta akipenda sana kuhudumia wagonjwa na hapohapo akapata wazo la kutoa huduma kwa wagonjwa wakiwa nyumbani. Akaandika tangazo na kulibandika mtaani kwao, kwamba kama kuna familia yenye mgonjwa asiyejiweza yeye
yuko tayari kumhudumia.
 
Kuanzia hapo akawa anapata oda zaidi ya ishirini kwa siku na hatimaye kuanzisha kampuni ya kutoa huduma kwa wagojwa majumbani, leo hii ni miongoni mwa wanawake wanaotajwa kuwa na pesa nyingi katika nchi ya Marekani. Wakati vyuma vimekaza, wewe amsha akili yako kutatua mahitaji muhimu, lazima pesa zikufuate hata kama huzitaki! Mtaji wa kupata pesa zaidi uko nyuma ya kichwa chako, hapo kisogoni.
 
Ndiyo, ninamaanisha akili yako ina majibu ya kila kitu unachokihitaji maishani. Ingia kazini na jitolee kikamilifu, pesa inapenda sana jasho halali la mtu. Mtu mmoja aliwahi kubanwa na haja kubwa akiwa stendi ya basi. Alihangaika sana kutatua tatizo hilo, hadi aliposaidiwa na watu waliokuwa wakiishi karibu na eneo la stendi, kuanzia hapo alianzisha wazo la kujenga vyoo stendi ya mabasi, leo hii kuna pesa inapatikana kupitia huduma ya vyoo na kuoga kwenye stendi za mabasi, tumia akili yako kukukwamua na mkazo wa vyuma.
 
ONGEZA UBUNIFU
Hakuna biashara mpya! Nyingi zilishafanywa, lakini hiyo isikupe shida. Muhimu ni wewe kuongeza ubunifu kwenye biashara yako. Ijumaa ya wiki iliyopita, nilikwenda kula gengeni, lakini niliondoka na elimu kubwa sana kuhusu ubunifu.
 
Mwanzoni nilikaa peke yangu, lakini ndani ya muda mfupi sana viti vyote vilijaa wateja, lakini wauzaji wa pembeni hawakuwa na watu kabisa. Nikaanza kufanya utafiti unaomfanya yule mama auze kuliko wenzake ndipo nikabaini jambo moja. Yule mama anaweka maji ya kunywa kwenye kidumu cha lita tano, kwa hiyo mteja akimaliza kula hatoi pesa mfukoni kununua maji ya kunywa, lakini wauzaji wengine hawakuwa na maji,
 
mteja akimaliza kula inamlazimu kwenda kununua maji wakati bei ya chakula ni sawa na ya mama mwenye maji kwenye dumu, nani ataacha kwenda kula kwenye maji ya kunywa ambayo halipii?
 
Kwa hiyo hakikisha unakuwa mbunifu sana kwenye biashara yako. Hata kama umeajiriwa, hiki ni kipindi ambacho waajiri wengi wanajitahidi sana kubaki na wafanyakazi ambao wanazalisha zaidi kuliko wategeaji na wanaofanya kazi kwa mazoea na ndiyo maana makampuni mengi yamepunguza wafanyakazi,
 
si kwa lengo baya, lakini ni kutaka kubaki na wenye tija, ambao hata kama wanalipwa pesa nyingi, lakini wanaizalishia kampuni. Kuwa mtu wa kipekee kwenye eneo lako la kazi na biashara. Kama unauza maembe kwa mfano, hakikisha unakuwa mbunifu kuanzia kwenye kifaa au mahali pa kuuzia.
 
Usafi wa mazingira na wewe unakuwa wa kiwango kikubwa. Weka maji safi ya kunawa kwa ajili ya wateja wanaokula hapohapo, menya kwa ustadi mkubwa na kwa wanaonunua na kuondoka, wafungie kwenye mfuko safi na onesha unyenyekevu na ukarimu wa hali ya juu,
 
Ndugu zangu, maisha ni mchakamchaka. Hakuna kusimama, ni kama mwendesha baiskeli ambaye ataacha kunyonga pedeli na baiskeli itasimama na hatimaye ataanguka. Pambana na maisha kwa kuwa mbunifu kwa kila ulifanyalo ili uendelee kupata pesa kwenye kipindi chochote kigumu, kamwe usifanye mambo kwa mazoea, zama na nyakati hizo zilishapita zamani mno. Narudia tena, umiza akili kwa kiwango kisichotamkwa.
 
Katika kipindi kama hiki, unapataje usingizi? Tunatofautiana sana. Yaani kama kuna mtu anavuta shuka na kukoroma kabisa hadi asubuhi, basi anayafaidi sana maisha! Wengine hatukumbuki mara ya mwisho kulala usingizi wa pono ilikuwa lini! Kuwa wa kipekee kwenye kila eneo. Kama umepewa kazi ya kufagia, fagia hadi malaika wa zamu waseme kwa sauti kwamba hapa alifagia mtu!
 
Back
Top Bottom