Siku moja baada ya mtoto Thomas Rwehumbiza (9) aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha kupatikana akiwa amejificha katika moja ya nyumba eneo la Kilungule jijini hapa, mapya yameibuka kuhusu maisha yake.
Thomas alipatikana juzi saa moja usiku akiwa katika nyumba hiyo ambayo haijamalizika kujengwa mali ya Kanisa Katoliki Kigango cha Mtakatifu Salome Parokia ya Mtakatifu Monica Kilungule, alikolala kwa saa 51 akihofia kurejea nyumbani kwao.
Mtoto huyo anayesoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Kilungule, alipotea Jumatano iliyopita eneo la Kimara Bonyokwa, taarifa za walimu na baba yake mzazi Renatus Rwehumbiza, zikieleza kuwa hakurejea nyumbani baada ya kutoka shule.