Nini mchango wako kuhusu hili bro kuna ukweli wowote kwenye huu ujumbe mchungu na mzito
Huu ni mtizamo wa Ngugi wa Thiong'o na unaungwa mkono na watu wengi (mimi nikiwemo). Ni ukweli usiopingika kuwa wamishenari wa kwanza walitumiwa vyema sana kama waandalizi wema kumuandaa Mwafrika kisaikolojia ili atawalike kirahisi...(Mamlaka yote yanatoka kwa Mungu, Ukipigwa shavu la kushoto geuza na lingine...). Wakafanikiwa sana kumwaminisha Mwafrika kuwa alikuwa ni kiumbe duni asiye na ustaarabu, kiumbe wa bara la giza asiye na mchango wo wote katika ustaarabu na maendeleo ya dunia. Ngozi nyeusi ikageuzwa nembo ya shetani na madhila yote yanayoambatana nayo. Lugha za Mwafrika zikaitwa duni zisizo na mawanda mapana ya kimawasiliano. Dini zake zikatwishwa ushetani. Utamaduni wote ukavurugwa. Dunia ikaaminishwa kuwa Mwafrika hajatoa mchango wo wote wa maana katika maendeleo ya dunia hii.
Hoja kuu ya Ngugi ni kwamba lugha na utamaduni wa mtu ndiyo humtambulisha hapa duniani yeye pamoja na nafasi yake. Yeye ni nani? Alitoka wapi? Nafasi yake ni ipi katika mifumo mbalimbali inayotawala na kuendesha dunia hii? Falsafa yake ni ipi kuhusu maisha na jukumu lake la msingi kwake yeye na vizazi vyake vijavyo kijamii, kiuchumi, kisiasa, kitamaduni, kimaendeleo- katika mawanda ya kwake na hata kimataifa?
Ukishamvurugia mtu utamaduni wake unakuwa umetoa roho yake ya kiutashi na kimtazamo. Anakuwa msukule. Bendera fuata upepo tu na atafanya cho chote utakachokitaka hata kama ni kibaya kwake na watu wake. Anakuwa hana misingi. Hana mifumo yake mwenyewe ya kujiendeshea maisha. Anakuwa tegemezi. Ndiyo maana wazungu na jamii nyingine zinazojitambua wako makini sana kulinda utamaduni wao na lugha zao. Waangalie Wajapani. Wachina. Wakorea. Wahindi...isipokuwa sisi.
Na ukiangalia vyema Wazungu walifanikiwa sana katika hili. Mtu mweusi yupo tu kama zombie. Hana utamaduni wake. Hana mifumo yake mwenyewe. Mtawaliwa wa kisaikolojia, kifalsafa, kiutashi na hata kiutu. Na dini ni nyenzo muhimu sana iliyofanikisha zoezi hili. Wangetaka kutafsri vitabu vingine wangeweza hasa katika mashule lakini kufanya hivyo kungemsaidia nani? Ingekuwa ni sawa na kujimaliza wao wenyewe na kwenda kinyume na lengo kuu lililokuwa limewaleta.
Kilio cha Ngugi na kundi lake ni kwa mtu mweusi kujitambua. Kurudi katika utamaduni wake. Kujaribu sana kujiundia mifumo yake mipya ya kuendeshea maisha yake. Kuiona thamani yake aliyokuwa nayo kabla hajakalishwa chini kisaikolojia. Afike mahali abadilishe mifumo hii aliyorithishwa. Mifumo ya elimu. Mifumo ya kisiasa isiyoendana na utamaduni na historia yake. Mifumo mipya ya kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia. Ni kwa kufanya hivyo tu ndiyo mvuvumko wa kweli utatokea kwa Afrika na pengine safari ya maana kuelekea kwenye maendeleo kikiki itaanza. Vinginevyo Afrika, pamoja na utajiri wake wote, itabakia tu ikizunguka katika mzunguko butu huu wa umasikini, siasa za hovyo, mifumo ya elimu iliyopitwa na wakati, ufisadi wa kinyama na madhila mengine lukuki....
(Nilikuwa na muda mrefu sijaandika gazeti humu.
Mama Mlonge si ajabu atakuja kunigombesha [emoji16][emoji16][emoji16])