KUTOLEWA GEREZANI
Taarikh 10 Januari 1967 ikiwa taarikh 28 Ramadhani kiasi cha saa 10 za alasiri, wafungwa wote tuliokuwa tukiitwa "wafungwa wa kisiasa" tuliyokuwepo katika gereza la Langoni tulikusanywa, na waliletwa pamoja na sisi wenzetu kutoka gereza la Kinu Moshi. Haikupita muda ila tuliyaona magari mawili ya magereza yametufikilia. Sote tulipakiwa na kupelekwa Makao Makuu ya Magereza, Kiinua Miguu (Mjini).
Tulifika huko na kin'gora cha magharibi kinalia. Tulitawadha na baada ya kumaliza kusali, tulifuturu kwani sote tunamshukuru Mwenye Enzi Mungu tulikuwa tukifunga. Baada ya kumaliza kufuturu, tuliachwa kukaa katika njia ya kupitia baina ya vyumba na vyumba. Tuliachwa hapo mpaka baada ya kusali Taraweh ndipo tulitiwa vyumbani na kufungiwa ndani. Taarikh 11 Januari ikiwa taarikh 29 Ramadhani, kiasi cha saa tatu za asubuhi, Karume na kikosi chake cha Baraza la Mavamizi walifika hapo gerezani, walitukuta tumewekwa tayari, tukingojea maamuzi yao juu yetu