Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Turudi kwenye hadithi yetu. Ikatokezea mwaka huo huo wa 1985, dada yangu Fatma akaolewa, na ikasadifu kuwa aliyemuoa ni mtoto wa kaka yake Bi Aweina, yaani mke wa Maalim Seif. Kwa hivyo, wakati Fatma alipojifungua mtoto wake wa kwanza mwaka 1986, Bi Aweina akaja nyumbani kwetu kumjulia hali mzazi, tena naye akiwa na mtoto wa mikononi. Nakumbuka akiitwa Sharifa.
 
Siku hiyo nikatamani kumuuliza Bi Aweina yote niliyokuwa nikisikia (au nikiyadhania kichwani mwangu tu) kuhusu mumewe. Sikuwa nimesahau kuwa nilitaka kuwa kama mumewe. Nikawa siondoki kizingitini kwenye mlango wa chumba cha mzazi pale nyumbani lakini wapi! Siku nzima ikapita nikijiimania na kushika hiki mara kile. Nikashikwa na haya za kitoto.
 
Hongera kamanda [emoji122][emoji122][emoji122]
 
Baada ya kumaliza kukaguwa, akataka kukutana na wananchi wa vijiji vinavyozunguka bonde hilo kusikiliza malalamiko yao. Miongoni mwao, baba yangu alikuwa na malalamiko ya kuchukuliwa ardhi yake na JKU tena kwenye eneo ambalo hata halikuwa bondeni. Kipande cha ardhi ya Mti Mkuu. Aliposimama kulalamikia hilo, Maalim Seif akauliza endapo baba yangu alishawasilisha malalamiko hayo kwa serikali za wilaya na mkoa. Alipojibu ameshafanya hivyo kipindi kirefu, na akaulizwa Maalim Masoud Omar ikiwa amechukuwa hatua gani, Maalim Masoud akafanya kosa la kudanganya kuwa eti hajawahi hata mara moja kusikia jambo hilo.
 
Duh! Baba yangu akainuka kama aliyepigwa uchapu: β€œBwana Masoud wataka tusutane!?” Maalim Seif akatambuwa haraka kuwa Maalim Masoud amedanganya na baba anasema kweli na bila ya kuyaendeleza malumbano, akaamuru kuwa suala hilo limalizwe haraka. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Baada ya mwezi mmoja tukawa tumerejeshewa sehemu kubwa ya ardhi hiyo ingawa nyengine waliamuwa kuwa wangetulipa fidia ya Fedha kwa kuwa walishaitumia kujenga Msikiti na hospitali. Baba akaamuwa kusamehe hiyo. Lakini ukweli kwamba tulipata ardhi yetu hiyo ilibakia kuwa alama ya kudumu nafsini mwangu kwa Maalim Seif utotoni mwangu.
 
Siku nyingi baadaye, maisha yalikuja kunikutanisha uso kwa uso na Maalim Seif, katika mazingira ya kinyumbani, nikiwa barobaro mzima lakini mgonjwa mikononi mwa familia ya Bwana Hamad Rashid Mohammed, Mikocheni, Dar es Salaam, ambayo ikishughulikia matibabu yangu ya kuanguka mkarafuu mwaka 1993.
 
β€œHuyu ni nani?” Maalim Seif alimuuliza mwenyeji wake, Bwana Hamad Rashid, usiku mmoja alipokuwa amekuja kuitembelea familia hiyo. β€œNi kijana wa Sheikh Ali Said, yupo hapa kwa matibabu. Anatibiwa na Dokta Sharif.” Huyu Dokta Sharif ni mtoto wa kaka yake, Maalim Seif, Bwana Ismail Sharif (Allah amrahamu) na alikuwa mtaalamu wa mifupa katika Hospitali ya Muhimbili.

Sheik Ali ni kaka yangu, Ali Said Omar, anayeishi Dubai na ambaye alikuwa rafiki wa wote hao na alinikabidhisha kwa Bwana Hamad ili anisaidie kupatiwa matibabu. Miongoni mwa hadithi zangu nilizokuwa nasimulia nyumbani Pemba baada ya kutoka matibabu, ilikuwa ni hiyo ya usiku huo kumuona na kumpa mkono Maalim Seif.
 
Siku nyengine nyingi zikapita tena na mengi yakajiri hapo katikati yake, mengine yakiingia na mengine yakitoka kwenye maisha ya mwanzo wa ujana, likiwemo la kuondokewa na baba yangu, mwaka 1995. Nadhani hata zile ndoto za kitoto za kutaka kuwa kama Maalim Seif nazo zikawa zimeyeyuka na maisha. Kisha ukaja Muafaka wa I mwaka 1999, nami nikiwa tayari ni mpigapicha wa kujitegemea. Siku yenyewe ya Muafaka nilipata fursa ya kuingia jengo la Baraza la Wawakilishi mchana wake na usiku wake nikawa miongoni mwa waliohudhuria chakula ya Ikulu.
 
Kule Baraza la Wawakilishi, Maalim Seif alikuwa amevaa kanzu, koti na kofia, akiwa amekaa benchi moja na Mzee Shaaban Khamis Mloo (Allah amrahamu). Nikawapiga picha. Akaniangalia sana kama ananikumbuka (au nikadhani kuwa ananiangalia na ananikumbuka).
Usiku wake pia, nikampiga picha akiwa na Dk. Salim Ahmed Salim (wakati huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika), Jakaya Kikwete (akiwa Waziri wa Mambo ya Nje) na nilikuwa miongoni mwa waliowahi kuchukuwa ile picha maarufu ya yeye na Dk. Salmin Amour wakikumbatiana, ambayo asubuhi yake ilikuwa sehemu ya picha za magazeti nikiwa nimeiuza kwa bwana mmoja anaitwa Charles aliyekuja Zanzibar kutoka Dar es Salaam
 
Tangu siku hiyo, nikajijuwa kuwa mimi napenda kumpiga picha Maalim Seif. Napenda kuichukuwa taswira yake na kuihifadhi. Je, ile ya kuwa nataka kuwa kama yeye ilikuwa na maana hii? Maisha ya kikazi yalikuja kunikutanisha tena kwa ukaribu na Maalim Seif miaka minne baadaye, na kwa takribani miaka saba mtawaliya (2003 hadi 2010) nikapata heshima ya kuwapo alipo kwenye shughuli za kisiasa na kijamii. Nina fakhari sana kwamba mvulana yule wa miaka minane kule Mchangani, ndiye aliyekuja kupata fursa ya kuwa karibu na shujaa wake akienda mote Unguja na Pemba na Bara na hata kutumwa naye hili ama lile, akifunzwa namna ya kuwa mtu ambaye leo anaweza kuandika hiki unachokisoma akijiamini. Na muda wote nikawa nafanya kile nikipendacho zaidi nafsini mwangu – yaani kuichukuwa taswira yake.
 
Hapa ninapoandika, nadhani nina kama picha 1,000 ambazo nimempiga Maalim Seif kwenye maeneo tafauti ndani ya Tanzania, baina ya mwaka 1999 na 2015 (nilikuwepo kwenye uchaguzi wa 2015 kama mwandishi wa habari na hivyo kupata fursa ya kuchukuwa taswira nyengine baada ya miaka mitano kupita tangu niondoke kuhamia Ujerumani).
 
Lakini kwa sababu ya athari ambayo amekuwa nayo kwenye maisha yangu, sikuwa nachukuwa taswira kwa kamera tu, bali pia kwa kuandika kuhusu yeye - ama iwe makala magazetini na mitandaoni au ushairi. Na hapo ndipo panapoingia sababu ya mimi kumzawadia diwani yangu ya N’na Kwetu ambayo ndani yake muna tungo zinazomuhusu ama moja kwa moja ama kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Nilipokutana naye na kumkabidhi, hata hivyo, sikumuambia lipi ni lake. Natarajia alijuwa mwenyewe.
Nadhani umbali huu ndivyo ninavyoweza kuwa kama yeye, umbali wa kumuhifadhia taswira yake. Lakini sio kwenye ile taswira ya awali ya nguvu na alama ya nguvu halisi ambayo nilikuwa nayo utotoni, kijiji kwetu Pandani - Mchangani.
Allah amrahamu kipenzi chetu! Amin.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…