Moto ni moja ya vitu vya asili vyenye nguvu sana. Moto mkubwa wa msitu unaweza kubadili ardhi, kuathiri mimea na wanyama wa porini, kuhatarisha uhai na kuharibu mali.
Wanyama wanaoishi Australia kama vile koala na possum wenye mikia yenye manyoya mengi ni wachache na huenda wakaangamia wote ikiwa makao yao yatateketezwa.
Asilimia 75 ya misitu ya mvua, asilimia 66 ya pori, jamii 19 za wanyama, na jamii 68 za mimea ya asili katika bara la Australia zimetoweka katika muda wa miaka 200 iliyopita. Jamii nyingi kati ya hizo hazipatikani kwingineko ulimwenguni.
Mnamo Desemba 1997, eneo lenye ukubwa wa zaidi ya eka 600,000 liliteketezwa wakati mioto mingi iliposambaa katika vitongoji vya Sydney, Australia, na katika miji kadhaa midogo karibu na milima ya Blue Mountains
Karibu nusu ya mioto hiyo haikuweza kuzimwa. Msimamizi wa idara ya wazima-moto alisema kwamba hajawahi kamwe kuona mioto mibaya hivyo katika muda wa miaka 30.
Mamia ya watu walilazimika kuhama, na baadhi ya nyumba ziliteketea. Watu wawili walikufa. Kuanzia mwishoni mwa mwezi wa Desemba 2001, mioto ya msitu ambayo yasemekana iliwashwa kimakusudi iliharibu misitu yenye ukubwa wa eka milioni 1.9.
Mioto inaweza kusambaa kwa sababu ya hali mbalimbali. Hali moja ya asili inayosababisha mioto ni mabadiliko ya hali ya hewa yanayohusiana na mkondo wa El Niño
Mara kwa mara, mkondo huo husababisha joto kali na ukame ulimwenguni pote. Eneo lolote lililokauka kwa sababu ya mkondo wa El Niño linaweza kuteketea mara moja.
Miti inapokatwa, miale ya jua hupenya misitu na kukausha majani hayo na vijiti hivyo. Cheche ya moto inapoanguka kwenye majani hayo na vijiti hivyo vikavu, moto huzuka na unaweza kusambaa kwa urahisi.
Matatizo ya kiuchumi yanaweza pia kuzidisha visa vya mioto mikubwa. Kwa mamia ya miaka, wakulima nchini Indonesia wamekuwa wakikata na kuteketeza vichaka ili kuboresha ardhi yao, bila kuharibu mazingira