Ninapenda kutumia wasaa huu kumuombea msamaha kijana Erik Kabendera kwa wote wenye mamlaka ya kikatiba na kisheria ambao kwa nanna moja walikwazwa, kujeruhiwa, kutofurahishwa ama kuumizwa na maandiko ya kijana huyu.
Ni kweli Kabendera alikengeuka aidha kwa kushawishika kwa fedha au kwa kutokuwa na taarifa kamili za kumuwezesha kufanya uchambuzi yakinifu na naamini lengo la wenye mamlaka lilikuwa ni kumfungua macho kijana huyu aone upande wa pili wa shilingi.
Natumai atakaporudi uraiani atakuwa amebadilika na kuwa na mtazamo chanya juu ya jitihada zinazofanywa na viongozi na Watanzania wengi wanaokesha wakifanya kazi kuhakikisha changamoto za wananchi zinatatuliwa na taifa letu kupiga hatua mbele.
Viongozi wetu ni watu waliopitia changamoto nyingi na mitihani mingi ya maisha na kuivuka ndio maana tumewaamini na kuwapa nafasi ya kutuvusha sisi kama taifa pale tulipokuwa tumekwama hivyo naamini kama watu wenye busara, huruma na upendo kwa wananchi wote watatafuta muafaka na kulimaliza jambo hili kwa moyo wa upendo ukizingatia kuwa Kabendera ni sawa tu na mtoto wao wa kumzaa.