Natamani ningekutana na huu Uzi kabla ya June 2021. Ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kupanda ndege. Nilipokuja kuusoma kwa mara ya kwanza, nafikiri mwanzoni mwa mwaka Jana(2022) kama siyo mwishoni mwa mwaka 2021, nilicheka sana. "Washamba" wanafanana. Kama ningeusoma kabla, ningepata maarifa ambayo yangesaidia kupunguza "ushamba"
Ilikuwa Alhamisi Usiku, 30/06/2021. Nilikuwa natoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam kwa ndege ya ATCL.
Alfajiri ya siku hiyo, nilipigiwa simu na mmoja wa watu wangu wa karibu lakini sikuipokea. Nilihisi kuwa pengine huenda kashafahamu kuwa siku hiyo napanda ndege. Sikutaka aniambie chochote kuhusiana na ndege, asije akanivunja moyo kusafiri kwa ndege. Nilikuja kumpigia baada ya kufika Dar es Salaam.
Nilifika mapema sana Airport. Ilibidi nikae kwa massa kadhaa kwenye mgahawa ulio pale Uwanjani, nafikiri unaitwa JAMBO CAFE, kusubiria muda wa kuripoti kuwadia.
Nikiwa hapo, nilianza kuingiwa na hofu, kiasi cha kuishiwa na hamu niliyokuwa nayo ya kupanda ndege. Nilitamani kuahirisha. Hata hivyo, nilijipa moyo, nikajisemea moyoni liwalo na liwe lakini ndege lazima nipande.
Nilitamani nikae kiti cha dirishani ili niwe ninachungulia mandhari ya ardhini nikiwa angani, na kwa bahati nzuri, ikawa hivyo. Nilikaa kiti cha dirishani, lakini siku "enjoy" kama nilivyokuwa nikitarajia. Nilitishwa na umbali tuliokuwepo angani.
Dakika chache baada ya ndege kuruka, nilipochungulia chini kupitia dirishani, taa za majengo zilionekana kwa mbaali. Sikuwa na hamu ya kuendelea kufanya hivyo. Niliamua kukafunga kabisa kale "kapazia" ka dirishani ili nisiendelee kupaona chini. Ule umbali ulikuwa unanitisha. Ila abiria wenzangu walikuwa na amani sana. Kuna waliokuwa wakichezea simu zao na wengine kompyuta pakato zao, na wengine walikuwa wakipiga stori kwa furaha kabisa. Mimi nilikaa kimya, kama vile sitaki kuongea, kumbe nilikuwa nimegubikwa na hofu.
Mkao na ukimya wangu, ulikuwa kama wa mtu anayetafakari jambo kwa kina . Lakini sikuwa natafakari, nilikuwa nimezama katika maombi, japo yalikuwa ni maombi ya kimya kimya. Niliomba safari nzima, kuanzia ndege iliporuka uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume Hadi ilipotua Dar.
Wakati ndege inatua, nilifikiri huo ni uwanja mwingine huko Zanzibar, kwa hiyo baada ya kushusha au kupandisha abiria wengine, tungeendelea na safari hadi Dar. Lakini kumbe sivyo, tulikuwa tumewawasili jijini.
Tulipotangziwa kuwa hapo tulipo ni Uwanja wa Ndege wa Dar Es Salaam, kwangu ilikuwa ni furaha isiyo na kifani.
Sikutarajia ingetuchukua muda mfupi kiasi hicho. Tulitumia kama dakika kumi na mbili hivi angani. Mimi nilitarajia tungekaa angani kwa dakika kama 30 hivi.
Njiani baada ya kutoka Airport, nilikuwa nikitabasamu na wakati mwingine kucheka mwenyewe, kila nilipokumbuka heka heka za kuanzia maandalizi hadi nilipokuwa kwenye ndege.
Bora tu ilikuwa ni one way, pengine kesho yake ningetakiwa kupanda tena ndege, sijui ingekuwaje. Huenda ningekataa. Hata wiki mbili baadaye, bado sikuwa tayari. Hofu bado ilikuwepo.
Ilinichukua zaidi ya mwezi mmoja hiyo hali ya hofu kunitoka. Ilipoisha, shauku nayo ilirejea.
Kwa kweli, usafiri wa ndege ni mzuri sana!
Hongera zake mkuu Clasi! Uzi wake umekuwa burudani na "darasa" kwa wengi, Mimi nikiwa mmoja wao!!!