MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ametaka umri wa kugombea urais ushushwe kutoka miaka 40 hadi kufikia 35.
Zitto ambaye amekuwa akihusishwa na harakati za kuusaka urais mwaka 2015, huku kigezo cha umri kikitajwa kuwa kikwazo, alitoa kauli hiyo jana wakati akitoa maoni yake kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyofika jana mjini hapa kukusanya maoni ya wabunge.
Akitoa maoni yake, Zitto alisema ni ushamba kwa nchi kama Tanzania kuweka umri mkubwa kama sifa ya kugombea urais.
"Umri wa kugombea urais, Rwanda wenzetu wanaruhusu miaka 35, Burundi miaka 35, Kenya miaka 35, Marekani miaka 35, Afrika Kusini miaka 35…Sisi ni ushamba tu, hakuna sababu ya kuweka umri mkubwa," alisema Zitto ambaye wakati akianza kuchangia alitania akisema kuwa itakapofika mwaka 2015 atakuwa na umri wa miaka 39.
Mbali na Zitto, wengine waliounga mkono hoja hiyo ni pamoja na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM), Mbunge wa Tarime, Chacha Nyambari Nyangwine (CCM), Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangwala (CCM), Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Prudenciana Kikwembe (CCM) na Mbunge wa Kasulu Vijijini, Agripina Buyogera (NCCR-Mageuzi).