Wanafunzi Babati watakiwa kuelimisha jamii kuhusu uhifadhi, mabadiliko ya tabianchi

Wanafunzi Babati watakiwa kuelimisha jamii kuhusu uhifadhi, mabadiliko ya tabianchi

Parabolic

JF-Expert Member
Joined
Dec 3, 2013
Posts
2,922
Reaction score
3,252
c91ebeec-ac0c-499e-83de-941de6cf9794.jpg



Babati.
Wanafunzi 40 wa shule za sekondari zilizopo katika eneo la Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori Burunge (Burunge WMA), wilayani Babati, Mkoa wa Manyara, wametakiwa kutumia elimu waliyoipata kuhusu uhifadhi na mabadiliko ya tabianchi kuelimisha jamii za vijijini.

Wanafunzi hao wametakiwa kuelimisha jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi, utunzaji wa mazingira na faida za uhifadhi wa wanyamapori baada ya kushiriki ziara ya mafunzo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Soma pia: Kamishna Mwishawa: Ongezeni wigo wa utoaji wa elimu ya uhifadhi kwa wananchi

Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Anna Mbogo, Oktoba 25, 2026, alipowapokea wanafunzi hao waliokuwa wakirejea kutoka ziara ya mafunzo ya siku tano iliyoandaliwa na Taasisi ya Chem Chem Association.

Mbogo amesema Wilaya ya Babati ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, lakini bado baadhi ya wananchi hawana uelewa wa kutosha kuhusu athari hizo na namna ya kukabiliana nazo.

7a82e714-256a-4782-b42e-5181272abde3.jpg

Amesema wanafunzi hao wanapaswa kushirikiana na walimu wao pamoja na wadau wengine kuhakikisha elimu waliyoipata inawafikia wananchi wengi zaidi.

“Tunashuhudia misimu ya mvua ikibadilika sana na joto kuongezeka. Hivyo, ninyi wanafunzi mmepewa elimu kuhusu masuala haya, ikiwemo utunzaji wa mazingira. Tunatarajia mtakaporejea vijijini kwenu, mtoe elimu hiyo kwa jamii,” amesema.

Amesema ziara hiyo, iliyowahusisha wanafunzi, watendaji wa Serikali na wazazi, itakuwa na manufaa makubwa endapo maarifa yaliyopatikana yatatumika kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.

8c731122-3da4-4de4-b73e-20fb7b59d2c3.jpg

“Mmepata fursa kubwa ya kutembelea na kujifunza Serengeti na Ngorongoro, lakini Watanzania wengi hawajapata nafasi hiyo, huku wengine wakilipa fedha nyingi ili kupata fursa kama hii. Sasa mkawa mabalozi wazuri wa kuendeleza uhifadhi na utalii,” amesema.

Mbogo ameongeza kuwa juhudi hizo zinaunga mkono msisitizo wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan wa kuendeleza sekta ya utalii na uhifadhi, akitaja pia filamu ya The Royal Tour iliyotumika kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chem Chem Association, Clever Zulu, amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine imefadhili ziara hiyo kwa mara ya pili ili kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo kuhusu uhifadhi na utalii, kisha kurejea katika maeneo yao na kuelimisha jamii.

“Chem Chem tunaamini kwamba ninyi bado ni watoto, lakini mkifahamu vizuri faida za uhifadhi na utalii, mtaweza kuwaelimisha wengine na kurithisha vizazi vijavyo maarifa kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira na wanyamapori,” amesema.

Afisa Wanyamapori wa Wilaya ya Babati, Christopher Laizer, amesema ziara hiyo imeongeza idadi ya mabalozi wa uhifadhi watakaosaidia kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda wanyamapori na kuendeleza utalii.

Amesema wanafunzi hao wana nafasi ya kutumia uzoefu walioupata kueleza kwa jamii faida za uhifadhi na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kulinda rasilimali za taifa.

Naye Afisa Miradi ya Maendeleo ya Jamii wa Chem Chem Association, Napendali Wazoeli, amewashukuru walimu, kampuni ya utalii ya Kanaga, taasisi ya Mkono kwa Mkono na Serikali kwa kushirikiana kufanikisha ziara hiyo ya mafunzo.

Baadhi ya wanafunzi na wazazi walioshiriki ziara hiyo wameishukuru Chem Chem Association na Serikali kwa kufanikisha mafunzo hayo, wakisema wamepata maarifa watakayotumia katika maisha yao na kuwafikishia wananchi wengine.

Wanafunzi Fatuma Shaban na Lulu John wamesema watatumia elimu waliyoipata kuelimisha jamii kuhusu uhifadhi, tabia za wanyamapori na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wamesema mafunzo hayo yamewaongezea uelewa kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira na wanyamapori, hivyo wako tayari kushiriki katika juhudi za kuhamasisha jamii kuhifadhi rasilimali hizo kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
 
Back
Top Bottom