Nmependa Dada Ndalichako alivyo kazia hapa.
‘Marufuku wanafunzi kwenda na limao, tangawizi vyuoni, shuleni’
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema ni marufuku kwa wanafunzi kwenda shule na malimao, tangawizi na spiriti pamoja na shule kutoza wanafunzi malipo ya ziada.
Aidha, amesema yeyote ambaye atabainika kukiuka maelekezo ya serikali, kwa kutoza wanafunzi malipo ya ziada, atachukuliwa hatua ikiwamo kufutiwa usajili. Serikali kupitia Rais John Magufuli ilitangaza wiki iliyopita kwamba vyuo vyote nchini pamoja na wanafunzi wa kidato cha sita watarejea masomoni kuanzia Juni Mosi, mwaka huu, baada ya nchi kuwa na unafuu mkubwa wa maambukizi ya virusi vya corona vinayosababisha ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19).
Profesa Ndalichako alitoa kauli hiyo jana kutokana na tatizo lililoibuka hivi karibuni kwa baadhi ya shule, kutoa mwongozo wa vitu ambavyo wanafunzi wanatakiwa kwenda navyo na kutakiwa kulipa ada.
Alisema ni marufuku kwa wanafunzi kwenda na spiriti shuleni, kwani inaweza kuchoma shule na mabweni na pia inaweza kutumika kama kilevi.
“Watu waache kutumia tatizo la corona kama kitegauchumi, watu wanaanza kuagiza hela za ziada za kazi gani, wanafunzi walikuwa wamekwishalipa ada kabla ya kufunga shule na walienda nyumbani kwa sababu kulikuwa na changamoto ya mlipuko wa ugonjwa corona,” Profesa Ndalichako aliwaambia waandishi wa habari jana.
“Serikali imefanya juhudi na maambikizi yamepungua na ndio maana imeamua kufungua shule na vyuo, wanafunzi wanaenda kuendeleza pale pale walipoachia kwa fedha zao zile zile, hakuna malipo ya ziada.
“Nitumie nafasi hii kukemea shule ambazo zinataka kutumia corona kama kitegauchumi, hapa hakuna kitegauchumi, tulikuwa na tatizo kama taifa, tumeungana pamoja, tumeweka na maombi na Mungu wetu ametusikia, sasa tusianze kuumizana kwa sababu ambazo hazina msingi wowote,” aliongeza.
Aidha, alisema wizara itafuatilia shule zitakazotumia janga la corona kama kitegauchumi na kuwa yeyote atakayebainika kufanya hivyo, atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufutiwa usajili.
“Wizara itafuatilia, shule ambazo zinataka kutumia janga la corona kama kitega uchumi kuweka michango michango ambayo haina uhalali wowote…wizara itachukua hatua ikiwa ni pamoja na kuzifutia shule usajili, kwa sababu tumekuwa tukiwaambia kila mara watu wanaoendesha shule wanatoa huduma kwa Watanzania wasiwe na roho ya kukomoana, imekuja changamoto ya corona watu wameona ni fursa, hili jambo halikubaliki,” alisema.
Aidha, alisema kwa wanafunzi ambao mpaka shule zinafungwa walikuwa hawajakamilisha ada, kufanya hivyo ili fedha hizo zitumiwe na shule kujiendesha.
“Wanafunzi ambao hawakuwa wamekamilisha kulipa ada, walipe ili shule ziweze kujiendesha vizuri, lakini wale ambao mpaka shule zinafungwa walikuwa wamelipa warejee shuleni kuendelea na masomo kama kawaida,” alisema.
Alisisitiza kuwa hata pale wanafunzi wengine watakapofungua shule, utaratibu utakuwa huo huo wa kutokuwa na malipo ya zaida.
“Ni lazima tuwaondolee hofu wananchi, unaposema mwanafunzi aje na limao ya unga, sijui hata inauzwa maduka gani, sasa tunapotoa taratibu ambazo hata utekelezaji wake unakuwa mgumu unazidisha hofu kwa jamii.
“Au unapomwambia mwanafunzi aje na kilo mbili za tangawizi mwanafunzi anayekwenda kukaa shuleni mwezi mmoja na wiki mbili, hilo koo lake litakuwa salama? Tuangalie pia na afya za watoto kwa kuzingatia kuwapa watoto vyakula vyenye vitamin C kwa wingi,” alieleza Waziri wa Elimu.
Alisisitiza kuwa ni vyema vyuo na shule, kuzingatia mwongozo uliotolewa na Wizara ya Afya ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa corona pindi watakapofungua shule. Alisema matumizi ya vitakasa mikono ni kitu cha zaida, na si lazima mwanafunzi kuwa navyo.
Credit: Habari leo