Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Nairobi, Kenya. Wanaharakati wa haki za binadamu nchini Kenya wameandamana katika mitaa ya Nairobi wakitaka Serikali ya Uganda kumuachilia mara moja kiongozi mkongwe wa upinzani, Dk Kizza Besigye, huku wakitaka pia Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki kuwaachilia viongozi wa upinzani wanaoshikiliwa, akiwemo Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.
Maandamano hayo yaliyofanyika Alhamisi, Septemba 3, 2026, yaliandaliwa na Pan-African Solidarity Network, muungano wa mashirika na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu. Takribani watu 30 walishiriki maandamano hayo, wakipita katikati ya jiji la Nairobi na baadaye kuelekea Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Mambo ya Nje, ambako waliwasilisha hati za madai kwa Serikali ya Kenya.
Waandamanaji walimtaka Rais wa Kenya, William Ruto, kutumia nafasi yake na mahusiano ya kidiplomasia kushinikiza kuachiliwa kwa Besigye, Lissu na viongozi wengine wa upinzani wanaoshikiliwa kwa sababu za kisiasa katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.
Kwa upande wa Besigye, wanaharakati wameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu hali yake ya afya, wakitaka aachiliwe bila masharti ili aweze kupata matibabu maalumu.
Soma pia: Dkt. Kizza Besigye mpinzani wa Museveni kwa sasa yuko hali mahututi
Besigye, ambaye amekuwa kizuizini nchini Uganda tangu Novemba 2024, anakabiliwa na mashtaka ya uhaini. Alikamatwa akiwa Nairobi na baadaye kuonekana nchini Uganda, jambo ambalo limeibua mjadala mkubwa kuhusu mazingira ya kuhamishwa kwake kutoka Kenya kwenda Uganda.
Wanaharakati wanaitaka Serikali ya Kenya kufanya uchunguzi huru kuhusu tukio hilo, wakitaka kubainisha nani aliyeomba, kuidhinisha na kuwezesha kuhamishwa kwa Besigye kwenda Uganda. Pia wanataka hatua zichukuliwe dhidi ya maafisa waliohusika iwapo itabainika kuwa sheria zilikiukwa.
Mbali na Besigye, jina la Tundu Lissu lilitajwa katika maandamano hayo kama sehemu ya kile wanachokieleza kuwa ni wimbi la ukandamizaji dhidi ya viongozi wa upinzani barani Afrika.
Lissu, Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania, amekuwa rumande tangu Aprili 2025 akishtakiwa kwa uhaini. Kesi yake inaendelea katika Mahakama Kuu ya Tanzania na kwa sasa ipo katika hatua ya utetezi.
Wanaharakati hao wametaka pia viongozi wengine wa upinzani wanaoshikiliwa au kukabiliwa na mashtaka katika nchi za Afrika Mashariki waachiliwe, wakisema kukamatwa kwa viongozi wa kisiasa kwa sababu ya misimamo yao kunadhoofisha demokrasia na utawala wa sheria katika bara hilo.
Katika maandamano hayo, wanaharakati waliitaka Serikali ya Kenya kutoa msimamo kuhusu namna nchi hiyo inavyoshughulikia masuala ya haki za binadamu katika ukanda wa Afrika Mashariki. Pia waliitaka Kenya kutumia ushawishi wake wa kidiplomasia kushinikiza Uganda na Tanzania kuheshimu haki za viongozi wa upinzani na kuwaachilia wanaoshikiliwa.
Msemaji wa mtandao huo, Mulinge Muteti, alisema suala la Besigye haliwezi kutenganishwa na hali ya viongozi wengine wa upinzani katika ukanda huo, akitaja pia Lissu na wapinzani wengine wanaokabiliwa na vifungo au mashtaka.
Wanaharakati wametoa siku saba kwa Serikali ya Kenya kuchukua hatua kuhusu madai yao, wakisema watapanua kampeni hiyo iwapo hakutakuwa na majibu ya kuridhisha.
Baadhi yao wametishia kuchukua hatua kali zaidi ikiwemo kuandaa maandamano mapya na kushinikiza hatua dhidi ya balozi za Uganda na Tanzania nchini Kenya, pamoja na kuathiri shughuli za kiuchumi katika mipaka ya nchi hizo iwapo Besigye na Lissu hawataachiliwa.
Kwa wanaharakati hao, suala hilo si la Uganda au Tanzania pekee, bali ni changamoto kwa nchi zote za Afrika Mashariki katika kulinda haki za binadamu, uhuru wa kisiasa na demokrasia.
Wamesema kesi za Besigye na Lissu zinaonyesha umuhimu wa nchi za ukanda huo kuheshimu taratibu za kisheria na kuhakikisha mashtaka dhidi ya wapinzani wa kisiasa hayawezi kutumika kama njia ya kuwanyamazisha.
Maandamano ya Nairobi hivyo yamepanua mjadala wa Besigye kutoka kuwa suala la ndani la Uganda na kulifanya kuwa sehemu ya kampeni pana ya kikanda inayotaka kuachiliwa kwa viongozi wa upinzani wanaoshikiliwa katika Afrika Mashariki, wakiwemo Kizza Besigye wa Uganda na Tundu Lissu wa Tanzania.