Hakuna mtihani wala nini, hakuna cha kupanda daraja na hapo kwenye hiyo ajali kuna watoto wadogo ambao hawajui hata maana ya dhambi na kutubu.
Mimi Muislam ndio naamini hivyo. Maisha hayaishii hapa. Kwako kama unaamini kuwa maisha yanaishia hapahapa, unaamini hakuna maisha ya barzakh, unaamini hakuna kufufuliwa na kulipwa, hilo ni tatizo kwako, Allah akuongoze.
Hao watoto Allah atawalipa
Sisi Waislam tunamdhania dhana njema Mola wetu. Na tuna jihimiza subra.
155. Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanao subiri
156. Wale ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea
(Qur'an 2: 155- 156)
Sisi hatumdhanii Mola wetu dhana mbaya. Tunamdhania dhana nzuri. Na wala hatusemi ila analoliridhia Allah; Hakika sisi ni wa Allah na hakika sisi kwake Yeye tutarejea.
Kutoka kwa Suhaib -Radhi za Allah ziwe juu yake- Amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu -rehema na amani ziwe juu yake:
"Ajabu iliyoje ya jambo la muumini, hakika jambo lake lote ni kheri, na hakuna hilo kwa yeyote ila kwa muumini, akipatwa na jambo lenye kufurahisha anashukuru ikawa hilo ni kheri kwake, na akipatwa na madhara anasubiri likawa hilo ni kheri kwake."
[Sahihi] - [Imepokelewa na Imamu Muslim] - [صحيح مسلم - 2999]
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mtihani utaendelea kumpata Muumini mwanamume na Muumini mwanamke katika nafsi yake na watoto wake, na mali yake mpaka akutane na Allaah akiwa hana dhambi)) [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan Swahiyh].
Kutoka kwa Anas kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Anapompendelea mja Wake kheri, Humharakishia adhabu duniani. Na Allaah Anapomtakia mja Wake shari Humzuilia dhambi zake hata Amlipe Siku ya Qiyaamah)). Na amesema (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Hakika malipo makubwa kabisa yapo pamoja na mtithani mkubwa, na hakika Allaah Anapopenda watu Huwapa mtihani. Basi atakayeridhika atapata radhi (za Allaah) na atakayechukia atapata ghadhabu)) [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan]
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mfano wa Muumini ni kama mti ulio na rutuba, upepo unaupiga huku na kule, na ataendelea Muumini kufikwa na mitihani. Na mfano wa mnafiki ni kama mti wa seda [aina ya mti wa mbao ya mkangazi], hautikisiki hadi ung’olewe wote mara moja)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Kutoka kwa Sa’iyd bin Abi Waqqaasw (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nilisema: “Ee Rasuli wa Allaah! Watu gani wanaopata mitihani migumu zaidi? Akasema: ((Manabii, kisha mfano wake, na mfano wake. Hupewa mtihani mtu kulingana na Dini [imani] yake. Ikiwa Dini yake ni imara, mtihani wake huwa mkubwa. Na ikiwa Dini yake ni dhaifu hupewa mtihani kulingana na Dini yake. Husibiwa sana na mtihani mmojawapo hadi atatembea ardhini bila ya kuwa na dhambi)) [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan Swahiyh, Ibn Maajah, na Al-Albaaniy kadhalika kasema ni Swahiyh].
Kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Muislamu hatopatwa na tabu, wala maradhi, wala hamu wala huzuni wala udhia wala ghamu [sononeko] hata mwiba unaodunga isipokuwa Allaah Humfutia madhambi yake kwa sababu ya hayo)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Hivyo sisi Waislam tunamdhania kheri Mola wetu, na tunasubiri na kutaraji malipo kutoka kwake