Wazabuni 66 wajitokeza mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge

Wazabuni 66 wajitokeza mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge

Replica

JF-Expert Member
Joined
Aug 28, 2017
Posts
1,681
Reaction score
8,887
Takribani wazabuni 66 kutoka ndani na nje ya nchi wamejitokeza kununua Nyaraka za Zabuni za ujenzi wa mradi wa Umeme wa kiasi cha megawati 2100 katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) mkoani Pwani hadi kufikia tarehe 19 Septemba, 2017.


Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia Ujenzi wa Mradi wa kuzalisha Umeme wa Megawati 2100 katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) mkoani Pwani, Mhandisi Leonard Masanja, (katikati) akisikiliza jambo kutoka kwa Wazabuni walionunua nyaraka za ujenzi wa mradi huo. kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya manunuzi wa Wizara ya Nishati na Madini, Amon macAchayo.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia ujenzi wa mradi huo, Mhandisi Leonard Masanja wakati wa mkutano na wazabuni hao uliofanyika jijini Dar es salaam, Septemba 18, 2017. Mkutano huo ulilenga kutoa maelezo mbalimbali kuhusu mradi kwa wazabuni hao.

Hata hivyo, Mhandisi Masanja aliweka wazi kuwa, Serikali bado inaendelea na zoezi la kuuza nyaraka za zabuni hizo, ambapo tarehe ya mwisho ya kuzirudisha kwa ajili ya kuzifanyia tathmini na kumpata mshindi wa zabuni hiyo ni Oktoba 16, 2017.

Wazabuni (Kampuni na Wakandarasi) mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi walionunua Nyaraka za Zabuni( Tender Document) za Ujenzi wa Mradi wa kuzalisha umeme wa Megawati 2100 katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) wakisikiliza maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Mradi huo( hayupo pichani).

Akieleza kuhusu mkutano na wazabuni hao ambao ni makampuni na wakandarasi mbalimbali, Mhandisi Masanja alisema kuwa, wazabuni hao walipatiwa maelezo hayo baada ya kutembelea eneo la mradi na kujionea hali halisi ya eneo husika.

Aidha alisema kuwa, katika mkutano huo, wazabuni hao walipata fursa ya kuuliza maswali na kueleza changamoto mbalimbali walizoona kwenye eneo la mradi na katika nyaraka za zabuni ambapo baadhi ya maswali yao yalijibiwa papo hapo na mengine kuandaliwa na kusambazwa kwa wazabuni wote walionunua nyaraka za zabuni.

Wazabuni (Kampuni na Wakandarasi) mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi walionunua Nyaraka za Zabuni( Tender Document) za Ujenzi wa Mradi wa kuzalisha umeme wa Megawati 2100 katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) wakisikiliza maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Mradi huo( hayupo pichani).

Agosti 30, 2017, Serikali kupitia Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani ilitangaza zabuni ya kuanza ujenzi wa Mradi Mkubwa wa Umeme wa megawati 2100 katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji mkoani Pwani (Stiegler’s Gorge).

Dkt. Kalemani alifafanua kuwa tayari taratibu za awali zilikwishaanza ambapo wataalam wa ndani na nje walishakutana na kuchagua sehemu za kujenga mradi huo katika Mto Rufiji, Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) lilishaanza upembuzi yakinifu wa kujenga miundombinu ya kufikisha huduma umeme katika eneo la mradi utakotumika wakati wa ujenzi na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kujenga miundombinu ya Barabara.

Sambamba na hilo, Dkt. Kalemani aliweka wazi kuwa mkandarasi atakayepewa kazi ya kujenga mradi huo ni yule tu atakayeridhia kujenga mradi kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi ndani ya kipindi cha miezi 36.

Alisema kuwa tayari Serikali imetenga fedha za kutekeleza mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu baada ya kumpata mzabuni na kuanza ujenzi wake.

Mradi huo utakapokamilika utasaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma ya Umeme nchini.
 
Kuanza miradi kwa kutafuta kiki ni rahisi,katikati huwa inasimama kwa miaka.
Mingine iliyosimama ni pamoja na "nyumba za bure miaka 3 magomeni".
 
Hakika njia ya kuelekea uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025 itakuwa wazi baada ya kukamilika mradi huo wa umeme wa maji na ule wa reli ya kisasa ya train za umeme zinazochukua masaa sita tu kutoka Dar hadi Mwanza!

Watapiga makelele, usiwasikilize wala kugeuka nyuma ukawa jiwe. We songa, songa, songa
 
Kama kuna kampuni za Canada zilizo jitokeza nashauli zisipewe tenda yoyote ile
Si waamini tena wacanada, na nina hasira nao
Kwa kushikilia ndege zetu (bombardier) na kutuibia madini yetu
Kama unadhani Canada peke yake ndio wanauhusinao na ACACIA utakuwa unajidanganya. Humo wajumlishe na Marekani na Uingereza. Hao nao wasipewe chochote. Kule kunaweza kuwa ni usajili au makao makuu lakini mabepari kutoka pande za Ulaya na Amerika wapo.
 
Mradi kama huo ni vizuri wakapewa watu kutoka ulaya, namaanisha Ulaya Magharibi au USA. Project kubwa kama hizi kumpa Mchina kwa kigezo cha low cost zina madhara makubwa sana siku za usoni, Mchina kwenye project kama hizi hususani kwenye nchi kama zetu hizi hutia hasara kubwa sana ambayo ni ngumu kuiona kwa jicho la kawaida.

Kuwapa watu wa Ulaya Magharibi na USA project kama hizi inaweza kuwa na gharama kubwa kifedha lakini faida yake ni kubwa kwa mapana zaidi, uhakika zaidi wa utendaji wa mradi kwa miaka mingi, ajira zenye malipo mazuri na usalama kwa watu wetu, Watu wetu ni rahisi kujifunza teknolojia na kuwa na msaada kwa Taifa siku za usoni, Muuingiliano kwenye jamii zetu ni rahisi kwa wazungu kuliko wachina, supplier wazawa watapata kazi kirahisi kuliko kwa wachina ambao uzoefu unaonyesha wanaagiza kila kitu kutoka kwao, Uboreshaji wa mazingira husika ambapo uzoefu unaonyesha wachina hujenga mabanda ambayo hubomoka baada ya ujenzi.. Hydro-plant zote ambazo tunazo ujenzi kwa kiasi kikubwa kama sio chote ulifanywa na makampuni kutoka ulaya.

Kwenye ujenzi wa barabara kwa kiasi kikubwa tumejionea kazi chafu kutoka kwa Wachina kuliko kazi ambazo zimefanywa na makampuni kutoka Ulaya kama BAM, SOGEA SATOM, na Green Accre LTA. Pia uzoefu kwenye ujenzi wa barabara nyingi zilizojengwa awamu ya pili na ya kwanza umeonyesha ugumu wa hizi barabara ambazo nyingine mpaka leo zinadunda ukifananisha na zile za awamu ya tatu na nne ambazo kwa kiasi kikubwa zimetekelezwa na mchina kwa kigezo cha Unafuu.

Tutoe mawazo mbadala kulikomboa Taifa letu.
 
Back
Top Bottom