Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,922
- 3,252
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi (watano kulia) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa dini wakati wa Kikao Kazi kilichofanyika Makao Makuu ndogo ya wizara hiyo jijini Dar es Salaam. Watatu kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Maduhu Kazi. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Serikali imewaomba Viongozi wa Dini kuungana katika Kupigana Vita ya Mmomonyoko wa Maadili huku ikiweka wazi wajibu wa familia kutotekelezwa ipasavyo hali inayopelekea kuwepo kwa madhara ya mmomonyoko wa maadili huku makundi ya vijana yakijihusisha na dawa za kulevya,uporaji,ubakaji,utapeli na maasi hali itakayopelekea kuona ni halali kula jasho la mtu au kufanya mauaji ili kupata mali.
Rai hiyo imetolewa leo Aprili 11 na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mheshimiwa Patrobas Katambi wakati wa Kikao Kazi na Viongozi wa Dini ambapo agenda za Mmomonyoko wa Maadili,Amani na Utulivu,Matumizi sahihi ya Mitandao ya Kijamii zilitawala kikao hicho lengo ikiwa kulinda tunu ya amani iloyopo nchini.
“Hakuna bomu baya kuliko silaha za kivita kama mmomonyoko wa maadili,bomu hili linaathiri kila kukicha,nawaomba sana viongozi wa dini mtusaidie sana kupigana vita ya mmomonyoko wa maadili,familia hazitekelezi wajibu wake siku hizi kwa kiwango kikubwa hasa kwetu sisi vijana,nafurahia kuona wazee wetu mmetufikisha mpaka hapa leo Taifa limekua na amani na salama ni kwasababu ya maadili mliyokuwa nayo,vijana wenye maadili mazuri wapo hao sio tatizo kwasababu wanabeba ile hofu ya Mungu.Lakini tukiacha mmomonyoko wa maadili uendelee kushamiri katika jamii tafsiri yake hatutokuwa salama kwasabu baadhi ya vijana ambao hatutokua na mafunzo ya kiimani tutajiingiza kwenye dawa za kulevya,wizi,uporaji,ubakaji,utapeli na maasi na kuona ni halali kula jasho la mtu kwa kudhulumu kwa sababu ya mmonyoko wa maadili,tunapenda mali kuliko watu.”Amesema Katambi
Waziri Katambi ameongeza kuwa ameteuliwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwa daraja Kati ya Viongozi wa Dini na Serikali ambapo amewaambia milango iko wazi kwa viongozi hao kuongea na kushauriana na serikali ikiwemo utoaji wa maoni mbalimbali kwa serikali lengo ikiwa kudumisha tunu ya Amani na kuhakikisha kuwepo kwa Utulivu nchini.
“Nimebeba dhamana hii kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan na Nchi yetu kuwa kiungo muhimu cha mahusiano, Usalama, amani na maendeleo au Daraja la kuvusha mema.Hii Wizara(Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi)kimsingi ni dhamana yake kwasababu yeye ndio Amiri Jeshi Mkuu wa Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama,kwa msingi huo ni kwa neema ya Mungu na kwa mapenzi yake na ufunuo wake Mungu kupitia Rais wetu mpendwa, amenipa dhamana nisimame kwa niaba yake katika kuhakikisha ninakua karibu nanyi kama daraja la kuwasaidia katika majukumu yenu,katika kutekeleza sheria,taratibu lakini kufanya kazi hii ya Kimungu mkishughulika Kiroho kwa Koroani tukufu na Biblia takatifu nasi tukishughulikia Watanzania Kimwili kuleta Ustawi na maendeleo yao kupitia Katiba na Sheria,”
“…..Niliapa mbele ya Mwenyezi Mungu,nikaapa mbele ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuilinda na kuitetea ambayo ni ya kwetu sisi wote na nikaapa mbele ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwamba nitafanya kazi kwa uaminifu na uadilifu na kumshauri kwa hekima na busara ambayo lazima itoke kwa Mungu”amesema Katambi
Wakizungumza katika kikao kazi hicho kilichoitishwa na Waziri Katambi,viongozi wa dini wameishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kuwashirikisha katika mapambano dhidi ya mmomonyoko wa maadili ambapo wameahidi kutumia majukwaa katika nyumba za ibada kukemea mmomonyoko wa maadili katika jamii.
“Sisi Baraza la Waislam kupitia Mufti Mkuu wa Tanzania,Dkt.Abubakar Zubeir alishazindua Kitabu chenye anuani isemayo;Mmomonyoko wa Maadili Nani Alaumiwe?,kwahiyo tunakushukuru Waziri nawe leo umetuita na umetuomba tuwaunge mkono serikali kwenye vita dhidi ya mmonyoko wa maadili basi tukuahidi tutaendelea kukemea hilo katika nyumba zetu za ibada mbele ya waumini wetu,” amesema Sheikh Ali Hamis Ngeruko.