Nakuandikia Waziri wangu wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda,
Mnamo mwezi Disemba, 2022 wewe Mhe Waziri ulitoa kauli:
Waziri Mkenda: Ajira ya Chuo Kikuu isiwe kuangalia GPA pekee lazima wapimwe, wafanye na usaili.
Mimi ni mstaafu chamani na Serikalini. Pamoja na kwamba nami pia nimehitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa shahada zangu mbili za sheria, watoto wangu wawili nao wamehitimu Chuoni humo: mmoja amehitimu sheria kama mimi na mmoja amehitimu uchumi. Wa mwisho wangu naye amejiunga pale kwa shahada ya masuala ya biashara.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni chuo kikuu kikongwe na bora kuliko vingine kwa Tanzania na kwingineko. Kinastahili heshima kubwa na tunakipenda. Lakini, kwasasa kinaelekea kukwama. Kinaelekea kubaya. Kinaongeza programu mbalimbali za kimasomo lakini hakiajiri Wahadhiri wa kutosha. Kinapata vibali vya kuajiri lakini hakiajiri.
Sababu kubwa zaidi ya zote ni GPA ya 3.8 au zaidi kwa Shahada ya Kwanza. Kupata au kukosa GPA hiyo katika Shahada ya Kwanza humtoa au humwingiza mhusika kwenye kuweza kupata ajira ya Uhadhiri. Hata watanzania na wasio watanzania wenye Shahada za Umahiri na Uzamivu lakini wasio na 3.8 Shahada ya Kwanza hawaajiriki.
Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ilishatoa Muongozo juu ya sifa za Wahadhiri Vyuo Vikuu. Sifa inayoainishwa kwenye Muongozo wa TCU ni GPA ya kuanzia 3.5 kwa Shahada ya Awali/Kwanza. UDSM imekuwa ikiiacha mbali sifa hii kutoka TCU na kutaka 3.8 na zaidi. Zote, lakini, ni GPA za Daraja la Pili la Juu (Second Upper Division).
Kung'ang'ania 3.8 sasa kunaipa tabu UDSM. Inakosa Wahadhiri. Inaathirika kitaaluma kwakuwa Wahadhiri wachache waliopo wanaelemewa na majukumu mengi na makubwa na hivyo huduma za kitaaluma zinayumba. UDSM inashindwa kupata Wahadhiri kwa kwakuwa tu waombaji 'walitenda dhambi' ya kukosa 3.8 kwenye Shahada zao za awali.
Ifike wakati 3.8 isiwe kikwazo cha kuajiri na kusongesha mbele gurudumu la kitaaluma. UDSM ishauriwe na kuelekezwa kufuata Muongozo wa TCU huku ikichuja waombaji wake kwa umahiri wao katika kufundisha au kwenye usaili wa namna nyingine. Nayaongea haya kwakuwa kwasasa UDSM inakosa waombaji na matangazo ya ajira yanarudiwa:
University of Dar es Salaam-. UDSM isaidiwe!
GPA kubwa si kigezo pekee cha uelewa na uwezo wa Mhadhiri kufundisha!
Mzee Tupatupa wa Lumumba, Dar es Salaam