Rais Magufuli kama yu mzima wa afya njema, ni jambo jema. Hata kama tukitofautiana kifikra, kimatazamo au kiitikadi, siyo sababu ya kufurahia au kutaka mwenzio asiwepo Duniani.
Hatutaki Polisi waue raia, hatutaki wasiojulikana waue, wapoteze au wateke watu wanaoikosoa Serikali au viongozi kwa sababu tunataka kila mmoja aishi mpaka pale ambapo hatuna uwezo wa kuzuia kuondoka kwake Duniani. Hata mmoja wetu anapoondoka, tunasikitika na kuomboleza.
Kama hatutaki mtu mwingine yeyote aondoke Duniani, nina hakika kila mwanadamu mwenye mapenzi mema na binadamu wenzake, hawezi kufurahia kifo cha Rais Magufuli au kutaka Rais Magufuli afariki.
Mimi siyo shabiki wa Rais Magufuli wala CCM, lakini simchukii Rais Magufuli wala mwanaCCM yeyote, bali nayachukia matendo ninayoamini siyo ya haki. Uchaguzi wa mwakajana uliudhi kila anayelitakia mema Taifa hili, lakini hiyo siyo sababu ya kumtakia kifo yeyote. Uchaguzi wa 2020 ulikuwa hovyo kabisa, na kwa hilo Rais Magufuli hakulitendea haki Taifa letu.
Lakini kwa dhamira ya moyo wangu kabisa, nathubutu kusema, Rais Magufuli kuna mema mengi aliyoyafanya, na kuna baadhi ya makosa ameyafanya kwa sababu ya kuwa too ambitious katika kuitaka Tanzania ipate maendeleo ya ghafla. Siku Magufuli akiondoka Duniani, tukaja kuambiwa kila alilolifanya na maisha yake kwa ujumla, wengi tunaweza kushtushwa na ukweli, na tukamlilia wakati hayupo.
Kuna mambo ambayo, nadhani hayabishaniwi:
1) Magufuli angependa Tanzania iwe na maendeleo makubwa kwa muda mfupi, na kwa sababu ya dhamira hiyo kuna wakati amefanya makosa, ambalo siyo jambo la ajabu.
2) Mimi siamini kama Magufuli ni tajiri au mtu aliyejilimbikizia mali kupitia uongozi japo sifurahishwi na kila kitu kupelekwa Chato. Naambiwa anamiliki hoteli kule Chato, lakini hicho siyo kitu cha ajabu, na amejenga kabla ya kuwa Rais. Hata wabunge wana mahoteli.
3) Kuna wateule wake wengine wamefanya mambo mengi ya ajabu ajabu kwa kutaka kumfurahisha Rais, na yote anabebeshwa yeye, na huenda hakuwaagiza.
Mazuri mengi aliyoyafanya Magufuli, na ambayo tunaweza kuyathamini kwa sasa, mpaka yaondoke ni pamoja na:
1) Kutokomeza/kupunguza ujambazi. Hapo nyuma majambazi walitamba sana na ilikuwa kawaida sana kysikia vifo vilivyosababishwa na majambazi
2) Nidhamu ya wafanyakazi wa umma.
3) Ujenzi wa miundombinu msingi
4) Maamuzi ya haraka, hata kama kuna wakati yanakuwa na makosa.
Kubwa kabisa baya ambalo nililisemea sana ni kuruhusu wasiojulikana waue, washambulie, wateke na kupoteza watu. Hilo nililiona ni baya kuliko yote. Mengine yanavumilika, na wala hatumtegemei kutokosea maana naye ni mwanadamu. Ninachoshukuru, matukio hayo kwa sasa yamekoma, na tunaomba hali iendelee hivyo hivyo. Tubishane na kukosoana kwa hoja, na siyo kutekana au kuuana.
Lakini pamoja na yote hayo, tumtakie afya njema na maisha marefu Rais Magufuli. Mimi ni kati ya watu ambao , kwa yale mema aliyoyafanya, kwa kuzingatia ubinadamu wetu, nitahuzunika sana kama Rais Magufuli akitangulia mbele za haki. Tutaendelea kumkosoa pale tunapoona amekosea ili ikiwezekana arekebishe. Tutaendelea kusema kuwa uchaguzi wa 2020 aliuharibu, na kumtaka kuhakikisha hilo halitokei tena, ila kumtakia kifo HAPANA. Kama mimi nitamtakia kifo mwanadamu mwanzangu, nitakuwa na tofauti gani na wale wasiojulikana ambao wanafurahia kuua, kuteka na kupoteza watu?
Popote alipo, awe ana afya njema au anaumwa, Rais Magufuli namwombea afya njema na maisha marefu. Arudi kazini, atafakari maeneo uliyofanya vizuri ili ayaendeleze, alipokosea ajisahihishe na kujirekebisha, asikilize mawazo ya watu, anaweza kuyapokea au kuyakataa, lakini siyo kutumia vyombo vya dola kuwadhibiti wenye mawazo tofauti. Aoneshe mfano wa uvumilivu, usikivu, kujirekebisha, lakini asiwe legevu kwenye mambo ambayo anaamini ni sahihi ja ya msingi alimradi hamwonei wala kumpendelea mtu au kikundi fulani.