Field Marshall ES:
Matatizo ya watu wanaompenda Nyerere ni emotion issues. Hata Rev. Kishoka, mwanzilishi wa mada, naona naye yupo kwenye kundi hilo.
Mada hii ni ya Falsafa ya Ujamaa na Nyerere. Katika miaka ya utawala wake, Nyerere alifanya mambo mengi mazuri. Mengi ya hayo mazuri hayana uhusiano wowote na Ujamaa.
Kwa mfano kuwa mstali wa mbele katika ukombozi wa nchi za Kiafrika ni jambo moja kubwa sana. Lakini ule sio Ujamaa.
Kwa mfano Tanzania ilipata matatizo ya njaa mara nyingi wakati wa utawala wake. Na yeye hakuona aibu kutafuta chakula hata katika nchi za kibepari hili wananchi wake wapone njaa. Hicho ni kitendo kizuri lakini huo sio Ujamaa.
Mlolongo wa mambo mazuri unaweza kuendelea lakini hayana uhusiano wowote hule na Ujamaa.
Watanzania ni sawa na wamarekani wengi tunapokuja katika masuala ya kisiasa. Emotions zinatawala na hatuko independent kuchambua mada iliyo mkononi.
Mipango mikubwa ya Ujamaa ilikuwa katika kipindi cha miaka kumi tu 1967 mpaka 1977 tu. Na kwa nchi changa kama Tanzania mipango hiyo kwa pamoja katika kipindi kifupi ilikuwa ni kutwanga maji kwenye kinu.
Simeni hivi kwa sababu naangalia Ujamaa miaka zaidi ya 20 toka kushindwa kwake. Bali, kuna hoja nyingi zilizotolewa wakati hulehule wa mipango hili ambazo zilisema kuwa mambo haya hayawezekani.
Mfano ni Elimu ya UPE. Wataalamu wa mambo ya elimu walipendekeza mpango uwe wa miaka ishirini. Lakini Nyerere alikataa na kusema kuwa mpango huo unaweza kutekelezwa kwa miaka saba tu. Matokeo yake tuna mfumo mzima wa elimu wenye kujali wingi kuliko ubora.
Zakumi,
Sijawahi kusikia hata mara moja duniani kuwa emotional kuhusu kitu ni kosa. Kosa ni pale unaporuhusu emotion zikupofushe na kukosa mwelekeo kabisa kama tulivyoona hapo awali katika mjadala huu.
Mimi nimefaidikia na Ujamaa wa Nyerere na Azimio lake, ndio maana nipo hapa nilipo na nabaini ni vipi Ujamaa na Azimio lingefanikiwa zaidi au mapungufu yake.
Watanzania tunamlaumu sana Nyerere kutokana na Umasikini na kuzorota kwa maendeleo kisa eti ni Siasa za Ujamaa na Kujitegemea na Azimio la Arusha.
Nikijiuliza kilichotokea Marekani leo kwa Uchumi wake kuangamia katika mfumo wa Kibepari hata kurudi kwenye great depression na kilichofanywa na Serikali enzi zile na wanachokifanya sasa najiuliza ni kosa ni sera, itikadi za Kibepari au ni ukosefu wa uongozi mzuri na udhibiti?
Kwenye Azimio la Arusha ambalo ndio blue print ya Taifa baada ya Katiba yetu, tulikiri "ili tuendelee tunahitaji vitu vinne, Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora"
Kushindwa kwa Tanzania kuwa na maendeleo mazuri na ya uwiano ya kiuchumi hakutokani na Sera, Itikadi, Ujamaa au Azimio la Arusha.
Ni kutokana na uhaba na ufinyu wa vitu hivyo vinne tulivyosema kuwa ni muhimu ili tupate maendeleo.
Labda mtu atasema tungeongeza mtaji, lakini mtaji wetu ni watu na ardhi tuliyonayo.
Tukiangalia maana ya watu, si idadi pekee kutokana na Sensa. Watu ni wale wenye uwezo wa kufanya kazi, wenye upeo wa kuelewa majukumu na kuweza kutumia ubunifu, juhudi na hata maarifa ili kuwa wazalishaji mali.
Watu hawa wasingeweza kupata maarifa na uwezo wa kuwa na juhudi, ubunifu, na ufanisi kama wasingeelimishwa. Ndio maana jambo la kwanza lililofanywa wakati wa Azimio ni pamoja na kutaifisha mashule ili Serikali na mtaji wake mdogo itoe na kusambaza maarifa kwa wananchi wake ili wawe tayari kimawazo na kwa ufanisi kuwa wazalishaji na kushiriki katika kuchangia ujenzi wa Taifa kwa umahiri na utaalamu na si kwa mbinu za kijima.
Utakumbuka miaka ile ya awali Nyerere alisema, wakati wenzetu wanapaa, sisi tunatembea, inabidi tukimbie (not sure the exact phrase, mwenye nayo na aibandike hapa) kuwafikia. Sasa namna ya kuwafikia mojawapo ni kuboresha watu kwa kuwapa elimu na afya ili waweze kushiriki katika ujezi wa TGaifa, iwe ni kwenye Kilimo, Ufugaji, Biashara, Viwanda au shughuli nyinginezo.
Tunapokuwa kwenye Ardhi, Tanzania tunabahati ya kuwa na rasilimali nyingi za kutosha kutufanya tuwe Taifa linalojitosheleza. Ndio kwa awali tulipokea misaada ili tupate nafasi ya kujizindua kwa kuwa mkoloni alituacha kwenye uchumi na uzalishaji duni. Ukiangalia Kenya na hata Uganda wakati wanapata Uhuru na kufananisha na Tanzania kiuchumi, utagundua kuwa Tanzania tulikuwa nyuma sana kuliko wenzetu. Hata Msumbiji na Kongo, zilikuwa zimeshapata miuondombinu mizuri ya uzalishaji mali, iwe ni barabara, nishati, ujenzi wa miji, mashule, zahanati, viwanda na mengineyo. Sisi tulikuwa na miundombinu ya kujishikiza na Muingereza alituachia viraka alivyoanzisha Mjerumani!
Siasa safi, tulikuwa nayo, na ndio chimbuko la kutaka kujenga nchi ya Kijamaa na Kujitegemea. Maazimio yote uliyoyataja pamoja na sear nyingine ni msingi wa Siasa Safi.
Siasa Safi ni kile kinachoundwa na Chama na uongozi wa Chama. Ndio ushindani wa vyama vingi uliondolewa na TANU (not Nyerere alone) kutokana na mazingira tuliyokuwa nayo nyakati hizo na yaliyokuwa yanatokea si Tanzania tuu, hata kwenye nchi jirani.
Bahati yetu nzuri, hatukufikia hatua ya Marekani ya Civil War kati ya Yankees na Confederates, North na South, maana historia ilishatufundisha kwenye uchanga wa Taifa, mkoroganyo wa itikadi ni sumu na tayari tulishaona matokeo ya kukosekana na mshikamano wa kisiasa kutokana na vita baridi. Hivyo kuepoka vurugu hizo kwenye uchanga wetu ukiambatanisha na unyonge na umasikini, uamuzi wa TANU ambayo ilikuwa chama Tawala kufuta mfumo wa vyama vingi ili kujenga stability, ulikuwa ni haki kwa nyakati hizo.
Suala halikuwa ni kuuwa ushindani, bali kuzuia na kuiepusha Tanzania kuingia katika misukosuko ya kiitikadi kama nchi nyingine zilizyoingia na kupata matatizo.
Lakini ushindani ulibakia ndani ya Chama tawala TANU na ni humo ndani yake ambao ilitegemewa kuwa wale wenye msimamo tofauti na sera na fikra za Mwenyekiti, ama wangewasilisha na kutetea maoni yao na kuyaoanisha na mfumo tuliokuwa tunaujenga na si kufanya mambo kwa uhaini.
Kuna listi ambayo Kuhani kaiweka hapa ya watu takribani 12 ambao eti walipingana na TANU (yeye anasema ni Nyerere) ambao waliposhindwa hoja walifukuzwa uanachama na wengine kuwekwa vizuizini. Swali linabakia hata Kambona aliyekimbilia Uingereza, je yeye alipinga Ujamaa na alikuwa na sera gani kwa Mtanzania? Hata hao wengine ambao kuna wengine walikimbila nje ya nchi, ni sera na itikadi gani walizokuwa nazo ambazo walizifanyia kazi na hata kujaribu kuziuza kwa Watanzania na wakashindwa kutokana na Watanzania kuamini ujamaa?
Ukichunguza, hao 12 na waliofuatia, hawakuwa na Sera au Itikadi yeyote wala utashi wa kimapinduzi na falsafa kuliongoza Taifa. Wao walichokuwa nacho ni kuupinga Ujamaa, Azimio na Nyerere lakini hawakuwa na lolote la kumuuzia Mtanzania apate chaguo. Maana kama walikuwa na sera au falsafa, wakati masharti yalipolegea 1992, wangerudi wakiwa na nguvu kubwa ya ushawishi na kutuuzia sera ambazo zilikimbizwa na Nyerere kwa miaka 25.
Leo hii mawazo na Siasa zao tulizonyimwa na TANU 1965-67 zingekuwa ndio chimbuko la kweli la upinzani Tanzania.
Uongozi bora, hapa ndipo tatizo kubwa lilipo kwa Tanzania. Si nyakati zile tulipoimba ili tuendelee na kulikumbatia Azimio na Ujamaa, bali ni mpaka leo.
Hatuwezi kumlaumu Nyerere, Mwinyi, Mkapa au Kikwete pekee kwa kuwa eti wao walikuwa ni Maraisi na Wenyekiti wa Chama tawala.
Uongozi si wa mtu mmoja ni jumuisho la watu na wanakuwa na mtu mmoka amnaye ni kinara na msimamizi ambaye anabeba sauti za Chama na Serikali.
Kama yalivyotokea kwa Nyerere, hata Kikwete amerithi ugonjwa huo wa kukuta kuwa yeye ni Kiongozi na walio wasaidizi wake, hawana ufanisi, juhudi, hawajitumi na si wakweli kuwa wako pamoja na nahodha wao.
Tofauti ya Nyerere na waliomfuatia hasa Mkapa na Kikwete, ni kuwa alikuwa na uwezo wa kushawishi na alilena kulitumikia Taifa na si Chama au kikundi maalumu cha marafiki.
Bibi Ntilie kanukuu vizuri waraka wa Nyerere dhidi ya "Wazungu Weusi" viongozi ambao walijiona kuwa wao ndio wenye haki na mamlaka pekee ya kuila ile keki ya Taifa.
Wengi wao ama kutokana na udhaifu wa upeo wa kielimu na Utendaji, walifikai kuharibu kabisa maana ya Ujamaa, Azimio na hata utimilizaji wa Sera.
Tatizo letu hata leo ni kufikiri kuwa kazi hii ni ya Rais pekee, na wengine waachiwe huru na hawapaswi kuwajibishwa.
Tofauti yetu leo na wakati wa Nyerere hata Mwinyi ni kuwa sisi kama Taifa, tumeamka na kuwa makini kukemea juhudi za kuua maendeleo zinazofanywa na viongozi wetu huku wakishirikiana na mafisadi.
Naamini kama Nyerere angekuwa kwenye madaraka leo hii, asingelipuuzia vilio vya wananchi na hata nguvu zetu kuwajibisha Viongozi na Serikali jinsi Mkapa na Kikwete walivyofanya kwa ufanisi wa hali ya juu. Hilo ndilo linalomtofautisha Nyerere na waliomfuatia hasa Mkapa na Kikwete.
Tunamsingizia kuwa Nyerere ni haambiliki kwa kuwa ni viongozi walewale "wazungu weusi" ambao waliwekewa vipengele maalum kwenye Azimio la Arusha kuwadhibiti ambao walishindwa kufanya kazi zao na kutimiza majukumu na ili kukwepa lawama na kuwajibika, wakamtuhumu Mwalimu kwa kila kitu.
Ni mpaka pale tutakapokuwa na tabaka la viongozi bora wenye maadili, wenye upeo, wepesi wa kufanya maamuzi magumu, wenye kujituma, ufanisi na kujihakiki na kuwjibika, ndipo Tanzania inaweza kuamka tena na kuwa Taifa la Kijamaa na Kujitegemea na tutaweza kuushinda Umasikini, Unyonge, Maradhi na Ujinga.
La sivyo, hata huu uchumi tulionao wa soko huru na utandawazi ni kazi bure, kwa kuwa tunajua kuwa si Sera au Itikadi za siasa zinazorudhisha maendeleo nyuma bali ni sisi kama Watu na Viongozi.
Hivyo emotion zangu ni kutokana na kuwa tunaukwepa ukweli wa mambo na kukimbilia kulundika lawama kwa mtu mmoja huku wa kuwajibika ni sisi sote.