Yanga nao wamekuja na mechi dhidi ya As Vita siku ya Simba day jumapili hii. Wanasema ukimwaga ugali wao wanamwaga mboga
- Tunachokijua
- Klabu ya Simba itafanya tamasha lake la Simba Day Agosti 6, 2023 katika uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni Rasmi.
Aidha, Simba SC itacheza na timu ya Power Dynamos ya Zambia.
Katika kuelekea siku hii, kumekuwepo na uvumi kwenye mitandao unaosema mahasimu wao, timu ya Yanga SC itacheza na AS Vita Club, timu kutoka Kongo siku hiyohiyo hali iliyoamsha hisia tofauti miongoni mwa wadau wa soka.
JamiiForums imezungumza na Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe ili kupata uthibitisho wa taarifa hii. Amesema
“Kocha wetu anahitaji mechi mbili kabla ya Ngao ya Jamii, kuna uwezekano mechi moja ikachezwa asubuhi nyingine jioni au ratiba inaweza kuwa tofauti na hivyo.
“Kuhusu kucheza na AS Vita hawapo kwenye ratiba lakini kwa kuwa Benchi la Ufundi linahitaji mechi mbili kama nilivyosema lolote linaweza kutokea.”
Hivyo, kutokana na ufafanuzi huu wa Afisa Habari wa Yanga picha inayosambaa kuonesha Yanga ina mchezo wa kirafiki siku ya Jumapili ni ya uzushi.
Uzushi huu umeibuka siku kadhaa tangu Yanga SC ifanye tamasha lake maarufu kama Siku ya Mwananchi Julai 22, 2023 ambapo pamoja na mambo mengine, ilicheza mchezo wa kirafiki na timu ya Kaizer Chief kutoka Afrika Kusini na kuibuka na ushindi wa bao 1 kwa 0.