Atimka jana usiku, Nchunga asema wamemalizana na Timbe
Kocha Kostadin Papic
Kocha Kostadin Papic aliondoka jana usiku kurejea kwao Serbia huku akisema kuwa tangu aanze kazi ya ukocha hajawahi kupata usumbufu kama alioupata katika klabu ya Yanga.
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana kutokea kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mara baada ya kukaguliwa mizigo yake tayari 'kukwea pipa', Papic alisema kuwa ameshawahi kufundisha klabu kubwa za mataifa mbalimbali zikiwemo za Afrika Kusini, Nigeria na Ghana, lakini kote huko hajawahi kukumbana na usumbufu wa kiwango anachokumbana nacho Yanga.
Aliongeza Papic kuwa kuna mambo mengi yanayofanyika Yanga si ya kuisaidia timu, kinyume na kote alikowahi kufundisha soka katika maisha yake ya ukocha.
"Nikifika kule (Serbia) ndio nitaamua hatua ya kuchukua dhidi ya uongozi wa Yanga ambao umenifanyia mambo mengi ya kukiuka mkataba," alisema Papic.
Rekodi za Papic zinaonyesha kuwa kabla ya kutua Yanga misimu miwili iliyopita na kutwaa nafasi iliyoachwa wazi na mtangulizi wake, Mserbia Dusan Kondic, aliwahi pia kuzifundisha klabu za Kaizer Chiefs na Orlando Pirates za Ligi Kuu ya Afrika Kusini, vigogo Asante Kotoko na Hearts of Oak za Ghana na Enugu na Enyimba za Nigeria.
Wiki iliyopita, kocha huyo aliwasilisha barua ya kujiuzulu nafasi ya ukocha wa Yanga baada ya kutofautiana na uongozi wa klabu hiyo kuhusiana na mambo kadhaa ya kitaalam, likiwemo suala la kuletewa kocha msaidizi Fred Felix Minziro pasi na yeye kushirikishwa.
Wakati huohuo, uongozi wa Yanga umesema kuwa tayari umemalizana na kocha Mganda Sam Timbe anayetazamiwa kutwaa nafasi ya Papic katika kuifundisha timu yao.
Akizungumza na NIPASHE jana jioni, Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga alisema kuwa walikutana na kocha huyo jana na kujadiliana naye kwa kina kabla ya kuafikiana na kwamba sasa, wanasubiri baraka za kamati yao ya utendaji ili wamuajiri.
"Tumekutana leo (jana) na kocha Timbe na tayari tumemalizana naye. Kuna nafasi kubwa ya yeye kuwa mrithi wa Papic, ila ni lazima kwanza suala hili tulifikishe kwenye kamati ya utendaji," alisema Nchunga.
Alisema kuwa kutokana na umuhimu wa jambo hilo hilo, kamati ya utendaji itakutana wakati wowote kuanzia leo ili kulijadili na kulitolea uamuzi.
Aliongeza kuwa Timbe ataondoka leo kurudi kwao Uganda ambako atakwenda kujiandaa na kusubiri kuitwa ili aanze kazi ya kukinoa kikosi chao kinachowania ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na pia kikikabiliwa na mechi ya ugenini ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Dedebit ya Ethiopia.
Nchunga alisema kutokana na uzoefu alionao kocha huyo, uongozi unaamini anaweza akaisaidia timu yao ambayo Jumamosi ilipata sare ya nyumbani ya 4-4 dhidi ya Dedebit.
Katika hatua nyingine, Nchunga alisema kuwa mjadala kuhusu Papic wameshaufunga na sasa wanaangalia mambo mengine.
Hata hivyo, alisema walimtaka Papic atoe ufafanuzi kuhusu usajili wa Mghana Kenneth Asamoah na pia kipa aliyekosa namba kwenye kikosi chao, Mserbia Ivan Knezevic, kwani wote wameisababishia Yanga hasara kubwa.
Taarifa nyingine zilidai jana kuwa Yanga waliweka mitego hadi uwanja wa ndege ili kuzuia jaribio lolote la Papic kuondoka kabla ya kuwakabidhi ripoti ya usajili, fedha zilizotumika na suala la Asamoah na Knezevic. Hata hivyo Papic aliondoka.