TUMSIKITIKIE MBOWE KWANZA AU TUWASIKITIKIE VIONGOZI WA DINI?
Na Thadei Ole Mushi.
Zambia iliwahi kupata Rais anayeitwa Fredrick Chiluba. Huyu jamaa aliwaingiza Viongozi wa Dini mtegoni kweli kweli, alipoingia madarakani alipokuwa akikosea walikuwa wanakuja juu haswa na kutoa matamko na makanyo yaliyotikisa nchi.
Chiluba akaona isiwe tabu akaanzisha urafiki na wao na akawa anawaita Ikulu ya Zambia kula dhifa mbalimbali na walipokuwa wakiondoka aliagiza wapewe Bahasha zenye Dola nyingi kila mmoja wakawa wanamwita Chiluba Mr Envelope.
Viongozi wengine wa Dini walienda mbali zaidi wakawa wanawaombea Ndugu zao vyeo Kwa Chiluba na akawa anawapatia Kwa hiyo nchi ikakosa taasisi muhimu sana ya kuonya, kurekebisa au hata kushauri Mamlaka pale inapokesea. Chiluba akawa anakosea wao wanampongeza na kusema nchi inasonga Mbele Kwa Kasi nzuri kumbe Zambia ilikuwa inadidimia kila siku.
Hapa kwetu jambo Hilo liliwahi kutokea kipindi Cha JPM. Nani anakumbuka matamko ya viongozi wa Dini kwenye ya Kwaresma ? hasa tukitilia mkazo waraka wa 2018 kutoka Kwa Kanisa Katoliki Ukiwa na ujumbe wa "uminywaji wa Demokrasia nchini na uhuru wa vyombo vya habari" .. kama hukumbuki nikupe link ujikumbushe..
Kanisa Katoliki Tanzania limetoa waraka kwa ajili ya kuwaandaa waamini wake kwa ajili ya kipindi cha Toba, kinachoanza rasmi Jumatano ijayo tarehe 14 Februari 2018 [ambayo ndiyo siku ya wapendanao, Valentine. tusherehekee kwa Toba eeeh tafadhalini!]. Kipindi hicho hujulikana pia kama...
Waraka huu ulitoka wakati nchi ikiwa hakuna vyama vya Siasa vilivyoruhusiwa kufanya Mikutano, waandishi wa habari wakiwa taabani na taharuki za hapa na pale watu wakiwa wanapotea na kutokuonekana tena.
Baada ya hapo hatujui viongozi wetu wa Dini waliishia wapi ila nilikuwa nikiwaona mara kwa mara wakitokea Ikulu na sifa kede kede kuhusu Serikali. Nilifika mahali binafsi nikaandika waraka wa kuwaombea Maaskofu wetu ambao walikuwa wamepatwa na upofu na hawakuweza kuona Tena Mbele ya meza za watawala. Fuata Link kuona makala hiyo..
https://www.facebook.com/
Kwa nini nimekumbuka yote hayo Leo?
Wiki Hii nimepata jumbe nyingi Sana inbox watu wakitaka nizungumzie kuhusu Kesi ya Ugaidi ya Mbowe kuzungumzwa kwenye Bunge la EU.
Nitasema Kwa kifupi kabisa.
Tanzania Kwa Mtizamo wangu imekosa watu wanaoheshimika kuishauri Serikali. Nilitamani kuhusiana na hii Kesi ya Mbowe Mamlaka (Serikali) ishauriwe na watu wa ndani sio wa nje ya nchi. Kwa bahati mbaya Sana kwa Sasa Tanzania haina Makundi mawili muhimu.
1. Hatuna mwanasiasa anayeheshimika na anayeweza kuishauri Serikali hasa wastaafu wetu. Ninachokiona Kwa wastaafu wetu na wao wanapigania matumbo yao kama sisi tunavyopigania hivyo wapo busy kutafuta Fursa na kuwatafutia watoto wao nafasi za Uongozi.
2. Hatuna Kiongozi wa Dini yeyote mwenye uwezo au kuheshimika anayeweza kugonga mageti ya Ikulu na kwenda kutoa Ushauri Kwa maslahi Mapana ya Taifa letu. Badala yake na wao wamekuwa wakitetea Matumbo yao binafsi kama na sisi tunavyotetea ya kwetu.
Naamini tungekuwa na watu wanaoheshimika toka Makundi mawili niliyotaja viongozi wetu wangelipata washauri Wazuri Sana. Na usingekuwa lazima tukatetewe na watu wa Magharibi kuhusu mambo yetu ya Ndani.
Kilichotokea ni Ombwe ambalo inabidi lijazwe na wenzetu huko Ulaya.
David McCalister ni nani?....
Huyu ndiye aliyekuwa anapambana Sana kuhusu Kesi ya Mbowe kwenye Bunge la EU. Huyu ni mwanachama wa Chama Cha CDU huko Ujerumani. Ni Mbunge wa EU toka 2014...
CDU ni nini?
CDU ni Chama Cha Kisiasa huko Ujerumani ambacho ni Rafiki mkubwa wa CHADEMA ambayo Mwenyekiti wake ameshikiliwa Kwa Ugaidi.
Nini nakiona?
CDU inakisaidia Chadema kufanya Siasa nje ya Tanzania na ndani ya Bunge la EU. Kwa vyovyote vile matokeo ya mjadala huu hautakuwa na impact nzuri Kwa Taifa letu ambalo Rais wetu ametaka Kwa nguvu kufufua Diplomasia ya Uchumi ambayo ilikuwa imeshakufa.
TUWAOMBEE VIONGOZI WETU WA DINI.
Tuwaombee Maaskofu wetu, Mashekhe na viongozi wengine wa Dini wapate kibali Mbele ya Mamlaka.
Wanaweza kujifunza kwa Wenzao..... Wafuatao.
Kitabu cha Injili ya Marko sura ya Sita mstari wa Kumi na saba unaelezea kisa cha Yohane Mbatizaji kufariki.
Mfalme Herode alikuwa akimwogopa sana Yohanne mbatizaji. Hii ni kwa sababu Yohane alikuwa akimweleza wazi wazi Mfalme Herode pale alipokosea.
Mara ya Mwisho Yohane Mbatizaji alimkanya na kumwambia wazi wazi Kuwa Herode alifanya vibaya kumuoa mke wa ndugu yake aliyekuwa akiitwa Herodia. Huyu Herodia alikuwa mke wa Filipo ndugu yake Herode.
Ndio maana siku siku ya sikukuu ya Herode ya kuzaliwa baada ya binti yake Herode ambaye alizaa na huyu Herodia kucheza vizuri na baba yake kumwambia achague Zawadi mama yake binti huyu alipendekeza mtoto wake achague kichwa cha Yohane kwa kuwa alikuwa kauzibe katika penzi lao na Herode.
Mtume Paulo alichukiwa sana na wagalatia kutokana na maudhui ya mahubiri yake kuwa ya kweli. Hakuna mtume aliyekuwa na maadui wengi kama Paulo soma wagalatia 4:16 Paulo analalamika kuwa kwa nn watu wanamchukia na kumfanya adui yao kwa kusema ukweli?
Yeremia aliwahi kuingia kwenye mzozo na viongozi wa Dini kwa kusema ukweli, walimshtaki na kutaka auawe kabisa kwa kuwa alisema kweli Soma Yeremia 26 mstari wa saba.
Timotheo rafiki yake mkubwa na Paulo, kwa wale ambao walikuwa hawajui Timotheo alikuwa amefungwa na Paulo Gereza moja ila baadaye alitangulia kutoka. Mara kwa Mara alikuwa akienda kumsalimia Paulo Gerezani ndiye aliyekuwa akichukua barua za Paulo kwa makundi mbalimbali ndio hizi zinazoitwa Waraka za Paulo.
Paulo aliwahi kumwandikia yeye Mwenyewe Timotheo barua (Waraka) katika barua hiyo Sura ya tatu Paulo anamwambia Timotheo kuwa mtu akitamani kazi ya uaskofu atamani kazi njema, awe ni mtu asiyelaumika, Mume wa mke Mmoja, mwenye kiasi na busara, asiwe mwenye kupenda fedha, asiwe mlevi, hapa Paulo aliwaasa kweli tabia za viongozi wetu wa Dini.
Tumuombe Sana Mungu atupatie Viongozi wastaafu wenye Busara, atupatie Viongozi wa Dini wenye Hekima na Busara ili wazishauri Mamlaka Kwa Busara na Hekima ili Haki itendeke wakati wote na Taifa letu lisonge Mbele.
Tukiri Iman za Ubatizo wetu!!!
Ujumbe toka kwa Ole Mishi.